Kiingilio cha chini katika mechi ya mchujo ya
Kombe la Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN) kati ya Tanzania (Taifa
Stars) na Uganda (The Cranes) itakayochezwa Jumamosi (Julai 13 mwaka huu) kwenye
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ni sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya
kijani.
Viti vya kijani katika uwanja huo wenye uwezo
wa kuchukua watazamaji 60,000 viko 19,648. Kwa upande wa viti vya rangi ya bluu
ambavyo viko 17,045 kiingilio ni sh. 7,000. Kiingilio kwa viti vya rangi ya
chungwa ambavyo viko 11,897 ni sh. 10,000.
Viingilio
vya daraja la juu ni kama ifuatavyo; VIP C yenye watazamaji 4,060 ni sh. 15,000
wakati sh. 20,000 ni kwa VIP B yenye watazamaji 4,160. VIP A yenye watazamaji
748 kiingilio chake ni sh. 30,000.
Mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya mwisho
kuwania tiketi ya kucheza fainali hizo zitakazofanyika mwakani nchini Afrika
itachezeshwa na mwamuzi Thierry Nkurunziza kutoka Burundi. Mechi ya marudiano
itachezwa jijini Kampala kati ya Julai 26 na 28 mwaka huu.
Tiketi kwa ajili ya mechi hiyo itakayoanza saa
9 kamili alasiri zitaanza kuuzwa siku moja kabla ya mchezo (Ijumaa) katika vituo
vifuatavyo; Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, mgahawa wa
Steers ulioko mtaa wa Ohio/Samora, Oilcom Ubungo, Kituo cha Mafuta Buguruni, Dar
Live Mbagala na BMM Barbershop iliyoko Sinza Madukani.
Katika
vituo hivyo tiketi zitauzwa katika magari maalumu. Magari hayo pia yatafanya
mauzo ya tiketi uwanjani siku ya mechi.
Tunapenda kuwakumbusha watazamaji kutonunua
tiketi mikononi mwa watu au katika maeneo yasiyohusika ili kuepuka kununua
tiketi bandia, hivyo kukosa fursa ya kushuhudia mechi
hiyo.
Post a Comment