Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF), Leodegar Tenga amesema hakuna hila yoyote katika marekebisho ya Katiba
kwa vile yametokana na maagizo ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu
(FIFA).
Akizungumza na Wahariri wa Michezo kwenye
ofisi za TFF, Dar es Salaam leo (Julai 9 mwaka huu), Rais Tenga amewahakikishia
wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Dharura kuwa dhamira ya marekebisho hayo ni nzuri,
kwani lengo ni kila mtu apate haki yake.
Amesema
Mkutano huo utakaofanyika Jumamosi (Julai 13 mwaka huu) utakuwa na ajenda moja
tu ya kuingiza Kamati ya Maadili, na Kamati ya Rufani ya Maadili katika Katiba
ya TFF kama ilivyoelekezwa na FIFA ili baadaye uanze mchakato wa
uchaguzi.
“Katika kuunda Kamati ya Maadili tumeangalia
ile ile ya FIFA, tusitengeneze kitu kipya, yaondolewe yale yanayotakiwa
kuondolewa, na yaongezwe yale yanayotakiwa kuongozwa. Kwa sababu tumeangalia
mazingira kwa Tanzania ni tofauti na Ujerumani au nchi za sehemu zingine,”
amesema.
Rais Tenga amewataka wajumbe wafike kwenye
Mkutano wakiwa na mtazamo wa kujenga, kwani kuna maagizo ya FIFA ambayo
wanatakiwa kuyatekeleza ili wasonge mbele.
“Tutawaeleza
kwanini hili limewekwa na lile limeondolewa. Mpira unataka unit (kitu kimoja),
ni mchezo wa kila mtu. Baada ya hapa tunaanzisha mchakato wa uchaguzi. Watu
wanaingia wakiwa wamoja, wanatoa hoja wanasikilizwa. Wanahukumiwa kwa hoja,”
amesema na kuongeza utatolewa muda wa kutosha wajumbe ili wayaone na kuelewa
marekebisho hayo.
Rais
Tenga pia alizungumzia kipindi hiki cha usajili na kutaka klabu ziwaachie
wataalamu wa mpira wa miguu kwani ndiyo wanaojua upungufu wa timu, hivyo
wanaweza kusajili wachezaji sahihi.
Amesema
tatizo kubwa la klabu za Tanzania ni kuwa timu zao hazina uwezo wa kuhimili
dakika 90, hivyo watu wanapaswa pia kuzungumzia aina ya mazoezi ambayo timu zao
zinafanya badala ya kubakia kutaja tu majina ya wachezaji wanaotaka
kusajiliwa.
Post a Comment