HATIMAYE vita iliyokuwa ikipiganwa ndani ya familia
ya Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, kuhusu mahali
panapostahili kuwa eneo la kuzikia miili ya wanafamilia hiyo imefikia
mwisho, baada ya Mahakama Kuu ya Mthatha iliyoko Jimbo la Eastern Cape,
kutoa hukumu inayoelekeza yawe katika makazi ya Mandela yaliyoko
kijijini Qunu.
Hukumu hiyo ilitolewa juzi na Jaji Lusindiso Pakade wa Mahakama Kuu
ya Eastern Cape, aliyekuwa akisikiliza shauri lililofunguliwa mahakamani
hapo na mtoto mkubwa wa kike wa Mandela, Makaziwe, aliyekuwa akipinga
hatua ya Mandla ambaye alichukua uamuzi wa kufukua miili ya watoto
watatu wa Mandela akiwamo baba yake mzazi, kutoka katika makaburi ya
familia yaliyoko Qunu na kwenda kuizika katika makazi yake ya kichifu
yaliyoko Mzove.
\
Jaji Pakade katika hukumu yake ya juzi, alikiita kitendo cha Mandla
kufukua miili hiyo kutoka kaburini na kwenda kuizika upya bila ridhaa ya
wanafamilia, kuwa hakikubaliki hivyo miili hiyo ifukuliwe na kurudishwa
ilipozikwa awali.
Katika kile kilichoonekana kuwa ni vita ya kugombania uhalali wa
kutwaa madaraka ya kusimamia mazishi ya Mandela baada ya kifo chake,
Mandla alitangaza kutokubaliana na hukumu hiyo na haraka haraka
mwanasheria wake alikata rufaa ya kuipinga. Hata hivyo, rufaa hiyo ilitupiliwa mbali na hivyo kutoa mwanya wa
kufukuliwa kwa mabaki ya miili hiyo kwa ajili ya kurejeshwa kijijini
Qunu.
Baada ya sekeseke hilo kwisha mahakamani hapo, Makaziwe aliyekuwa
akiongoza kundi la wanafamilia 16 kudai miili ya Makgatho, Thembekile na
Makaziwe, aliyodai iliibwa na Mandla usiku na kwenda kuizika katika
himaya yake, alisema atasimamia irejeshwe katika eneo la makaburi la
Mandela.
Makaziwe alikaririwa akieleza kuwa, kama baba yake (Mzee Mandela)
angezikwa nje ya eneo la Qunu ambalo kama alivyoelekeza mwenyewe, mifupa
yake ingetikisika kutoka kaburini.
Makaziwe, mtoto wa mke mkubwa wa Mandela, marehemu Evelyne, akiwa
sambamba na mama zake wa kufikia, Winnie na Graca Machel, pamoja na
ndugu zake wengine, aliwaongoza kwenda kuhifadhi mabaki ya miili ya
ndugu zake katika chumba cha kuhifadhia maiti ambako itafanyiwa
uchunguzi kabla ya kwenda kuzikwa upya katika makaburi ya Qunu.
Kurejeshwa kwa mabaki ya miili hiyo kijijini Qunu, kumetafsiriwa kuwa
ni hatua muhimu ya kuondoa utata uliokuwa umejitokeza kuhusu eneo
ambalo Mandela atazikwa baada ya kufa.
Pamoja na mvutano huu, Mandela mwenyewe alikwishaeleza kuwa, siku
akifariki, azikwe nyumbani kwake Qunu sambamba na yalipo makaburi ya
watoto wake.
Aidha, uwepo wa Winnie na Graca mahakamani wakiwa sambamba na
Makaziwe katika mapambano ya kuhakikisha sauti ya Mandela inasikilizwa
na kufuatwa, kumetafasiriwa kuwa ni uamuzi wa busara waliochukua ili
kulinda heshima ya familia katika kipindi hiki kigumu ambacho rais huyo
mstaafu yuko mahututi hospitalini.
Wakati hayo yakijiri, makundi tofauti tofauti ya wakazi wa vitongoji
mbalimbali vya Soweto, jana yalikuwa yakiendesha ibada za nyimbo za
shukurani kwa Mungu kwa kuinusuru familia ya Mandela na ugomvi wa eneo
la kuzika miili ya marehemu wa familia hiyo.
Nyimbo hizo zilikuwa zikiimbwa kwa lugha za Kizulu, Kixhosa na
Kiswana, huku baadhi ya vikundi vikiwa na mabango yaliyokuwa na ujumbe
wa kutoa shukurani kwa Mungu kwa kusimamia pamoja na wanafamilia ya
Mandela iweweze kumaliza ugomvi wao uliokuwa ukitishia heshima ya
familia na taifa.
Ikiwa ni siku ya 28 leo tangu Mandela alipolazwa katika Hospitali ya
Medi Clinic, mjini Pretoria akisumbuliwa na ugonjwa wa mapafu, hali yake
bado ni mbaya kwa kuwa bado anaendelea kupumua kwa msaada wa mashine.
CHANZO: www.mtanzania.co.tz
Post a Comment