Mfanyabiashara wa kampuni ya uwekezaji ya
Tanzanite One inayochimba madini eneo la Mirerani, wilayani Simanjiro, Willy
Mushi, ameuawa kwa kupigwa risasi na watu wanaoaminika kuwa ni wachimbaji wadogo
baada ya kukutana mgodini chini ya ardhi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Manyara, Akili Mpwapwa, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo alilosema lilitokea
saa 6:00 usiku wa kuamkia jana.
Kamanda Mpwapwa alisema tayari ametuma
timu ya upelelezi inayoongozwa na Ofisa Upelelezi wa Mkoa wa Arusha kuchunguza
zaidi tukio hilo.
Marehemu alipigwa risasi mbili kufuani upande wa
kushoto alipoongozana na mfanyakazi mwenzake, Kennedy Masimbaji, kukikagua eneo
la mgodi unaoingiliana na migodi ya wachimaji wadogo.
“Tulipofika kwenye mitobozano ambako kumepangwa mifuko
ya viroba vya mchanga kutenganisha mgodi wetu na ile ya wachimbaji wadogo,
ghafla tukashambuliwa kwa risasi ambazo zote zilimuingia marehemu kifuani na
kufariki dunia papo hapo,” alisema Masimbaji.
Mfanyakazi
mwingine wa Tanzanite One, Leonard Paul, alisema tukio hilo ni mwendelezo wa
mashambulizi yanayodaiwa kufanywa na wachimbaji wadogo dhidi ya wafanyakazi wa
mwekezaji pindi wanapokutana chini ya ardhi.
Alidai kuwa siku kadhaa
zilizopita, uongozi ulilazimika kusimamisha kazi kutoa fursa ya polisi
kuchunguza migogoro ya mitobozano. “Serikali lazima sasa ichukue hatua kuzuia matumizi
ya silaha za moto chini ya migodi,” alisema Paul.
Kwa mujibu wa mdogo
wa marehemu, Tumsifu Mushi, marehemu ameacha mjane na watoto wanne na taratibu
za mazishi zinaendelea.
Loading...
Post a Comment