Kikosi cha
Stars kilichopambana na The Cranes
Mechi ya
kwanza mchujo ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa
Ligi za Ndani (CHAN) kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Uganda (The Cranes)
iliyochezwa jana (Julai 13 mwaka huu) imeingiza sh. 113,268,000 kutokana na
watazamaji 17,121.
Tiketi za
kushuhudia mechi hiyo ziliuzwa kwa sh. 5,000, sh. 7,000, sh. 10,000, sh. 15,000,
sh. 20,000 na sh. 30,000.
Mgawanyo wa
mapato hayo ulikuwa kama ifuatavyo; asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani
(VAT) ni sh. 17,278,169.49 wakati wa gharama za uchapaji tiketi ni sh.
7,809,104.
Asilimia 15
ya uwanja sh. 13,227,108.98, asilimia 20 ya gharama za mechi sh. 17,636,145.30
na asilimia 5 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh.
4,409,036.33.
Asilimia 60
ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) sh. 52,908,435.91 na Chama cha
Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 2,645,421.80 ambayo ni asilimia
5 kutoka kwenye mgawo wa TFF.
TAIFA STARS
KAMBINI TENA JULAI 4
Timu ya
Taifa (Taifa Stars) imeondoka leo asubuhi (Julai 14 mwaka huu) kwenda Mwanza
ambapo itapiga kambi ya siku kumi kujiandaa kwa mechi ya marudiano dhidi ya
Uganda (The Cranes) kutafuta tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa Wachezaji
wa Ndani (CHAN) zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini.
Stars
inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imeondoka kwa ndege ya PrecisionAir
na itafikia hoteli ya La Kairo wakati mazoezi yatafanyika Uwanja wa CCM Kirumba
kulingana na programu ya Kocha Mkuu Kim Poulsen.
Wachezaji
walioko katika kikosi hicho ni Juma Kaseja, Aggrey Morris, Mwadini Ally, Ally
Mustafa, Shomari Kapombe, Kevin Yondani, Erasto Nyoni, Haroub Nadir, Mwinyi
Kazimoto, Frank Domayo, Mrisho Ngasa, Khamis Mchana, Amri Kiemba, Salum
Abubakar, Simon Msuva, John Bocco, Vincent Barnabas, Mudathiri Yahya, Athuman
Idd na Haruni Chanongo.
Mechi ya
marudiano itachezwa kati ya Julai 26 na 28 mwaka huu kwenye Uwanja wa Nelson
Mandela ulioko Namboole nje kidogo ya Jiji la Kampala. Tarehe rasmi itapangwa na
Shirikisho la Vyama vya Mpira wa Miguu vya Uganda (FUFA) siku kumi kabla ya
mechi.
TENGA
AWASHUKURU WAJUMBE WA MKUTANO MKUU TFF
Rais wa
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amewashukuru wajumbe
wa Mkutano Mkuu kwa michango yao, na utulivu waliouonesha katika kupitisha
marekebisho ya Katiba ya TFF ya 2013.
Amesema
marekebisho hayo yatawasilishwa kesho (Julai 15 mwaka huu) kwa Msajili wa Klabu
na Vyama vya Michezo kwa ajili ya kupitishwa ili mchakato wa uchaguzi uweze
kuanza mara moja.
“Tutamuomba
Msajili atusaidie kusajili haraka Katiba yetu ya 2013 ili tuingie katika
mchakato wa uchaguzi. Kama tulivyotangaza awali tumepanga kufanya uchaguzi
Septemba 29 mwaka huu, na tusingependa tarehe hiyo ipite,” amesema Rais Tenga
wakati akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kikao cha Kamati ya
Utendaji.
Katika
kikao chake, Kamati ya Utendaji imepitisha Kanuni za Maadili, Kanuni za
Nidhamu, na marekebisho kwenye Kanuni za Uchaguzi yanayotokana na kuundwa kwa
Kamati ya Maadili.
Boniface
Wambura
Ofisa
Habari
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Post a Comment