Mwenyekiti wa Kamati ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Edward
Lowassa akizungumza wakati wa majadilino yaliyohusu namna ya kuingiza suala la
wazee katika ajenda mpya za Maendeleo baada ya mwaka 2015. Mkutano huo
ulioambatana na chakula cha mchana ulifanyika siku ya Jumatano hapa Makao Makuu
ya Umoja wa Mataifa na ulioandaliwa na United Nations Foundation kwa
kushirikiana na Mashirika mengine ya Kimataifa. katika mchango wake, Mhe.
Lowassa amesisitiza umuhimu wa ubia kati ya serikali na sekta binafsi katika
kuzikabili changamoto za ongezeko la idadi ya wazee duniani. Inasemekana miaka
michache ijayo idadi ya wazee duniani itazidi idadi ya watoto wadogo chini ya
miaka mitano. Pamoja na Mhe. Lowassa wengine waliochangia majadiliano hayo ni
Bi. Ann Pawliczko kutoka UNFPA wa pili kutoka kushoto, Bw. Jack T. Watters
kutoka Pfizer, Bw. Paul Ong HelpAge International, Bw. Sharig Khoja kutoka
United Nations Foundation, aliyeketi karibu na Mhe. Lowassa ni Bi. Jane Barratt
aliyeratibu majadiliano hayo.
Mhe. Lowassa akipeana mkono
na mmoja wa waandaji wa majadiliano hayo kuhusu Wazee, takwimu kutoka Shirika la
Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu ( UNFPA) zinazonyesha kwamba mwaka 1950 idadi
ya wazee duniani waliokuwa na miaka 60 au kuzidi ilikuwa milioni 205, 2012 idadi
hiyo iliongezeka hadi kufikia 810 milioni. Inakadiriwa kwamba idadi hiyo
itaongezeka hadi kufikia Bilioni 1 si zaidi ya miaka kumi ijayo na ifikapo mwaka
2050 idadi ya wazee wenye umri wa miaka 60 na kuendelea itafikia bilioni 2.
Aidha duniani kote wanawake ndio wanaokadiriwa kuishi umri mrefu zaidi kuliko
wanaume.
Sehemu ya washiriki wa
majadiliano hayo wakiwamo pia Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao katika Umoja wa
Mataifa.
Mhe. Edward Lowassa
akibadilishana mawazo na Balozi wa Zimbabwe katika Umoja wa Mataifa, Bw.
Chitsaka Chipaziwa.
Mh. Lowasa akiwa na mmoja
wa washiriki wa majadiliano kuhusu mstakabali wa wazee.
Na Mwandishi
Maalum
Mwenyekiti wa Kamati ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Edward
Lowassa ( Mb) amesisitiza haja na umuhimu wa kuwapo kwa ubia kati ya serikali
na sekta binafsi katika kuzikabili changamoto zinazotokana na ongezeko kubwa la
idadi ya wazee.
“ Maisha Zaidi ya miaka 60
hayapashwi kuwa ya utegemezi, unyonge, kutojiweza au kutokuwa na matumaini.
Wazee bado na wanao mchango mkubwa ndani ya jumuiya, jamii, na familia zao
ili mradi tu wawezeshwe”.
Na kwa sababu hiyo anasema
Mhe, Lowassa, juhudi mbalimbali zinazofanywa na serikali katika nchi
zilizoendelea na zinazoendelea Tanzania ikiwamo za utoaji wa huduma za msingi
kama vile Afya , pensheni na uwezeshwaji zinapashwa kuchagizwa na sekta
binafsi.
Mwenyekiti wa Kamati ya
Mambo ya Nje, na Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Edward Lowassa(Mb ), ameyasema hayo
siku ya jumatano hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa wakati aliposhiriki
majadiliano kuhusu namna gani suala la Wazee linavyoweza kuingizwa katika
ajenda za maendeleo baada ya mwaka 2015.
Majadiliano hayo
yaliandaliwa na United Nations Foundation kwa ubia na International Federation
of Ageing, Help Age International, AARP, Global Coalition on Aging, mHealth
Alliance na Pfizer
“Kama kundi hili la wazee
likiwezeshwa na kusaidiwa ipasavyo , linaweza kuipatia jamii soko jipya,
ujasiriamali, utoaji wa maamuzi, utoaji wa huduma na utalaamu anuai katika
maeneo ya sayansi, teknolojia na upatanishi” anasema
Lowassa.
Na kuongeza, ili hayo yote
na mengine mengi yaweze kufanikiwa panahitajika bajeti ya kutosha kwa ajili ya
kundi hilo la jamii ikiwa ni pamoja na kuimarisha mifumo ya pensheni, huduma za
afya ambazo zitakidhi mahitaji ya wazee, huduma za kisaikolojia na huduma za
ulinzi jamii.
Hata hivyo anasema,
inasikitisha kwamba, katika nchi nyingi za Afrika na nyinginezo hata zile
zilizoendelea bado haziwezi kutoa huduma za uhakika na zenye viwango vya
kukidhi mahitajio ya wazee.
“Mara nyingi huduma
kwaajili ya wazee inabidi zishindane na huduma za makundi mengine kama vile
ongezeko la vijana wasiokuwa na ajira, upunguzaji wa vifo vya watoto wachanga
na wanawake wajawazito. Hata hivyo pamoja na changamoto zote hizi za vipaumbele
hatuwezi kuendelea na utaratibu huu wa kuchagua. Lazima tutumie maandalizi ya
ajenda za maendeleo baada ya 2015 kuwahudumia wazee” anasisitiza
Lowassa.
Akasema Jumuiya ya
Kimataifa inatakiwa kujikumbusha na kujifunza kwa kosa la kutoingiza suala la
Wazee katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Millenia ( MDGs)
yanayoelekea ukingoni, kwa kuhakikisha kwamba Wazee wanaingizwa katika malengo
mapya ya maendeleo baada ya 2015 kwa kuwa ni suala ambalo
haliepukiki.
Akizungumzia hatua
mbalimbali zinazochuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika
kuwahudumia wazee, Mhe. Lowassa anasema kama ilivyo kwa nchi nyingine, Tanzania
nayo inakabiliwa na ongezeko la idadi ya wazee.
Kwa mfano, amesema asilimia
4.5 ya idadi ya watu, ni watu walio na umri wa miaka 65 wastani wa juu zaidi
kuliko ule wa asilimia 3.6 Afrika Kusini mwa Jangwa la
Sahara.
“ Asilimia 80 ya watu hawa
wanaishi vijijini na maisha yao yanategemea kilimo. Serikali inajitahidi kadri
iwezavyo kutoa huduma za msingi kwa kundi hilo ingawa pia, na kama ilivyo kwa
nchi nyingine, tunakabiliwa na changamoto nyingi kukidhi mahitaji yote ya
wazee”. Akabainisha.
Akatumia pia fursa hiyo
kuyashukuru mashirika ya kimataifa kama vile Help Age International ambalo
limekuwa likiendesha shughuli zake nchi nchi tangu mwaka
1993.
Akatoa mfano kwa kusema
Shirika hilo, mwezi Juni mwaka huu kwa kushirikia na Pfizer limezindua mpango
wa miaka miwili wa kupunguza athari zitokanazo na magonjwa yasiyoambukiza (NCD)
ambayo yamekuwa yakiwaathiri wazee.
Akasema utoaji wa huduma
hiyo unakwenda sambamba na juhudi za serikali katika kukabiliana na magonjwa
hayo.
Akatoa wito kwa mashirika
mengine kuiga mfano huo na kwamba serikali itakuwa tayari kushirikiano
nayo,Takwimu kutoka Shirika la
Umoja wa Mataifa la Idadi ya watu ( UNFPA) zinaonyesha kwamba, katika kila
sekunde watu wawili duniani wanaadhimisha miaka 60 ya kuzaliwa kwao, na kwa
mwaka karibu watu milioni 58 wanaadhimisha miaka 60 ya
kuzaliwa.
Aidha katika kila watu
nane, mmoja ana miaka 60 au zaidi na makadirio yanaonyesha kwamba ifikapo
mwaka 2050 katika kila watu watano mmoja atakuwa na miaka 60 au
zaidi.
Ongezeko la idadi ya wazee
duniani linachangiwa na mambo mengi, ikiwa ni pamoja na ongezeko la umri wa
kuishi ambapo katika nchi 33 raia wao wanaishi zaidi ya miaka 80 wakati miaka
mitano iliyopita nchi ambazo umri wa kuishi ulifika miaka 80 zilikuwa 19
tu.
Post a Comment