SERIKALI imesisitiza kuwa itatoza Sh 1,000 kwa
kila kadi ya simu inayotumika lakini pia inaangalia utaratibu wa kufanya
makato hayo kwa njia ambayo haitamuumiza mtumiaji wa
simu.
Akizungumza jana jijini Dar es salaam, Waziri wa
Fedha,Dk William Mgimwa alisema kuwa kupitia tozo hizo wanatarajia kukusanya Sh
bilioni 160 kwa mwaka
“Kupitia wawakilishi wenu na sisi serikali kuwa
sikivu, tulishauriwa na ikaonekana kwamba kuna uwezekano wa kupata chanzo
kingine cha mapato kupitia kadi za simu” alisema
Alisema katika mapendekezo yaliyokuwa yametolewa
serikali ilishauriwa kutoza Sh 1,450 katika kila kadi ya simu lakini baada ya
kukaa na kushauriana serikali iliona ni vyema ikatoza Sh 1,000 ili kila
mwananchi aweze kumudu gharama ambapo kwa mwaka kila mmiliki wa kadi ya simu
atatozwa sh 12,000.
Alisema baadae serikali ilipokea mapendekezo
mbalimbali ili kuangalia kama hilo linaweza kutekelezeka na walipita ngazi zote
kabla halijapelekwa katika kamati za Bunge na kushauriwa kwamba tozo hilo
linaweza kufanyika kwa lengo la kukuza uchumi hasa maeneo ya
vijijini.
“Tathmini zote zimefanyika kikamilifu na baadae
suala hilo likafikishwa Bungeni ambapo pia napo lilikubalika... inawezekana watu
wanalalamika lakini ngazi zote suala hilo lilipopita lilikubalika na ikaonekana
ni sawa kutozwa sh 1,000 kwa kila kadi ya simu”
alisema.
Alisema kutokana na hilo kwa kutwa nzima kadi ya simu
itatozwa Sh 33.35 au Sh 100 kwa siku tatu ambapo serikali inaangalia utaratibu
mzuri ambao hautamuumiza mtumiaji wa simu.
Dk Mgimwa alisema fedha hizo zitakazokusanywa
zitaongeza upatikanaji wa maji vijijini, umeme pamoja na kuboresha miundombinu
katika maeneo ya vijijini.
Habari Leo
Post a Comment