Kampuni ya DSTV imesema haitaonyesha mechi za Simba na Yanga baada ya kutofikia makubaliano na Shirikisho la Soka Tanzania TFF.
Kauli ya DSTV imekuja baada ya kuwepo na maswali
mengi juu ya kuonyeshwa live kwa mechi za Ligi Kuu na kituo hicho ambapo
wameonekana kushikwa na kigugumizi kwa madai kwa sasa hawana
makubaliano yoyote na TFF kwa sababu ambazo wamekiri zipo nje ya uwezo
wao.
Akizungumza jana na waandishi wa habari Meneja
Masoko wa kampuni hiyo Ronald Shelukindo alisema kuwa awali waliweza
kuonyesha mechi hizo kutokana na kuwa na mawasiliano mazuri na TFF,
lakini kwa sasa hawana makubaliano yoyote ambayo amedai hawezi kuyaweka
hadharani kwa sasa.
“Ni kweli kuna baadhi ya mechi za Ligi Kuu za hapa
nyumbani tulikuwa tunaweza kuzionyesha, kutokana na makubalino miongoni
mwetu na TFF lakini kwa sasa hatuwezi kufanya hivyo kwa sababu zilizo
nje ya uwezo wetu ambazo hatuwezi kuzielezea kwa sasa,” alisema
Shelukindo.
Aidha, Shelukindo alisema katika hatua nyingine
katika msimu mpya wa soka wataanza kuonyesha mechi mbalimbali za Ligi ya
Uingereza na nyinginezo kwa miaka mitatu mfululizo.
Alisema wakati ligi mbalimbali za Ulaya zikitaraji
kuanza mapema mwezi huu amewataka wateja wao kulipia huduma hiyo ili
waweze kufuatilia kwa ukaribu mechi hizo huku wakiweka punguzo la
asilimia kumi kwa wateja watakaolipia bili zao kabla ya kuisha kwa za
awali.
Tayari kampuni ya Azam tv imeingia mkataba na
klabu 13 za ligi kuu Tanzania bara kwa ajili ya kuonyeshwa live katika
msimu ujao wa ligi hiyo inayotaraji kuanza mapema mwezi huu. MWANANCHI
Post a Comment