Na Julius
Kithuure, Nairobi
Hali nyumbani kwa Edward Mule Yesse katika eneo
la makaazi la Buru Buru huko Nairobi ilikuwa ya machozi ya furaha, nyimbo za
kusifu, kukumbatiana na karamu ya nyama choma.
Edward Mule Yesse
(katikati), alipigwa picha akiwa na baba yake na mke wake, akiwasili nyumbani
karibu na Nairobi baada ya miezi zaidi ya 18 ya kuwa kwenye kifungo cha
al-Shabaab huko Somalia. [Julius Kithuure/Sabahi]
Mule, kama anavyojulikana na familia yake na
marafiki zake, alitekwa tarehe 11 Januari, wakati wapiganaji wa al-Shabaab zaidi
ya 100 walipofanya ghasia katika kambi ya Utawala ya Polisi huko Gerile, katika
wilaya ya Wajiri kusini nchini Kenya, ambapo alipelekwa kama ofisa wa
wilaya.
Mule, kwa sasa ana umri wa miaka 32, alitekwa
pamoja na Fredrick Irungu Wainaina mwenye umri wa miaka 57, karani wa usajili
kwenye wizara ya Uhamiaji na Usajili wa Watu.
"Tuliwekwa kwenye chumba kisicho na mwanga katika
kipindi chote hiki," Mule aliwaambia waandishi wa habari waliokusanyika nyumbani
kwake Alhamisi (tarehe 1 Agosti). "Hakukuwa na anasa ya mwanga wa jua.
Kwa kweli, macho yangu yanauma, yanakaza kwa
sababu ya kuwekwa chumba chenye giza kabisa. Hata kuoga, tulioga kwenye giza
nene, na kupokea simu zao, wahudumu wetu wa al-Shabaab walitufunika macho yetu
na nguo nzito iliyokunjwa."
Mule (wa pili
kutoka kushoto) akiungana tena na familia yake: baba Edward Yesse (kushoto),
mkewe Mona (wa pili kutoka kulia) na mama Emma Yesse. [Na Julius
Kithuure/Sabahi]
"Ingawaje al-Shabaab hawakututesa, walitutisha
na kutuogofya," alisema, akiongezea kwamba al-Shabaab mara zote walitudhihaki
kwa kifo. "Kwa kweli, mara moja walituvua nguo na kutuambia kuwa muda wetu wa
kuchinjwa umewadia. Ilikuwa mpaka mabosi wao waingilia kati kusimamisha kipindi
cha kutisha."
Mule alisema alipata malaria akiwa kifungoni,
lakini al-Shabaab walimpatia matibabu. Alisema wanamgambo hao kwa kawaida huwapa
wali na nyama kula lakini chakula kilikuwa hakitoshelezi.
Kuteswa kiakili ilikuwa si ya kuvumilika na
kuteswa kimwili kwa kushikiliwa katika sehemu isiyo na mawasiliano ilikuwa jambo
la kitia kihoro," Mule alisema.
Al-Shabaab waliwaachia Mule na Wainaina Jumanne
baada ya majadiliano na serikali ya Kenya, mara baada ya familia za mateka
kadhaa wa Kenya kutoa wito kwa serikali kuchukua hatua.
Mke wa Mule, Mona Garisse, familia yake pamoja
na ndugu, marafiki na majirani wote walikusanyika kumkaribisha nyumbani.
Wakati akisubiri mwanaye wa kiume kurudi
nyumbani Alhamisi, mama wa Mule Emma Yesse alipatwa na hisia kali. Uso wake
ulighubikwa na machozi, mara chache akipata tabasamu wakati akiangalia picha ya
mwanaye iliyokuwa kwenye fremu.
Sabahi ilikaa chini na baba wa Mule, Edward
Yesse, kuzungumza juu ya mateso ya familia.
Sabahi: Je, unajisikiaje kuungana tena na
mwanao?
Edward Yesse: Maneno hayawezi kuelezea furaha
na faraja ninayohisi. Sikuweza kuepuka kulia wakati nilipomwona Mule.
Nimefarijika na nina amani.
Sabahi: Hukuweza kumwona Mule hadi siku tatu
baada ya kuachiwa kwake. Kwa nini hakuungana na familia yake mara tu baada ya
kuachiwa kutoka kifungoni?
Yesse: Haikuwezekana kuja nyumbani moja kwa
moja. Kulikuwa na taratibu za kufuatwa, kama vile usalama [kufanyiwa usaili] na
kufanyiwa uchunguzi wa afya na kisaikolojia.
Sabahi: Je, ilikuwa vigumu kusubiri taratibu
hizi baada ya kuwa na kuvumilia?
Yesse: Mule kwa sasa yuko hapa pamoja na sisi
na hili ndilo lililo muhimu zaidi. Alisema alikuwa kwenye makao makuu ya
Upelelezi wa Usalama wa Taifa mahali alipokuwa akisubiri taratibu za kufanyiwa
usaili.
Sabahi: Ni lazima kwamba ulikuwa wakati mgumu
kwa familia yako wakati Mule alipokuwa akishikiliwa mateka . Uliwezaje kukabili
hali hii?
Yesse: Mke wangu, familia yangu na mimi
tulikuwa tukisali mara nyingi. Tukimuomba Mungu kugusa nafsi za watekaji
wasimdhuru kijana wangu.
Pia nilikuwa na shajara ambamo niliandika hatua
zote ambazo mimi na serikali tulizichukua kumuokoa. Pia niliandika maneno yote
niliyozungumza na watekaji na walichoniambia. Nitamuonyesha mtoto wangu maelezo
haya katika shajara. Ni kumbukumbu ya kutia huzuni.
Sabahi: Sasa unajisikiaje?
Yesse: Sasa nina amani na furaha lakini nina
wasiwasi kwa sababu kuna familia nyingine ambazo zina uchungu kwa sababu vijana
wao ni mateka nchini Somalia. Moyo na mawazo yangu yanaenda kwa familia za
wanajeshi waliotekwa na mashirika ya misaada. Ninawaomba al-Shabaab kuonyesha
huruma na upendo kwa waliotekwa na kuwaachia bila ya masharti.
Sabahi: Je, ulilipa fidia yoyote kwa
al-Shabaab?
Yesse: Ninataka kulieleza hili kwa uwazi:
Familia yangu haikulipa hata senti, wala serikali ya Kenya. Ningeweza kupata
wapi kiasi hicho kikubwa cha fedha? Kijana wangu na mtekwaji mwenzake,
[Fredrick] Irungu Wainaina, waliachiwa bila ya malipo.
Sabahi: Lakini al-Shabaab walidai fidia ili
kuwaachia.
Yesse: Ndiyo. Kwa hakika, walitoa madai ya
fidia ya Dola 250,000. Hata hivyo, kiuhakika niliwaambia kwamba siwezi kupata
hizo fedha. Miujiza hutokea na hatimaye Mungu aliwagusa watekaji.
Sabahi: Ni nani unayemshukuru kwa hatimaye
kuachiwa kwa kijana wako?
Yesse: Ninamshukuru Rais wa Kenyat Uhuru
Kenyatta, Makamu wake William Ruto, na idadi ya wazee wa ukoo wa Somalia
wanaoheshimika. Pia naishukuru idara yetu ya upelelezi kwa kuwa na mawasiliano
ya karibu na watekaji.
Sabahi: Ulichukua hatua gani baada ya
al-Shabaab kutoa video ambapo walitishia kumuua Mule?
Yesse: Al-Shabaab ni kikundi cha waasi wenye
siasa kali ambachohapo awali kimekuwa kikiwakata vichwa watu wasio na hatia.
Wamewaua mamia kupitia ulipuaji wa mabomu na kupigwa risasi na ninahofia mabaya
zaidi kutokea.
Wakati hatima ya mtu inapokuwa mikononi mwa
kikundi hicho hatari, lolote linaweza kutokea. Ukweli kwamba al-Shabaab
wamemuachia kijana wangu bila ya kumdhuru inaonyesha bado wana roho ya
ubinadamu.
Sabahi: Nini ni ujumbe wako kwa
al-Shabaab?
Yesse: Kwanza, ninawashukuru kwa kutomdhuru
kijana wangu kwa namna yoyote. Ninawasihi kuacha vurugu nchini Somalia na
kwingineko. Hakuna mafanikio yanayopatikana kupitia katika risasi, ugaidi na
utekaji. Nina uhakika wanaweza kuweka silaha chini na kufuata jitihada
zinazofanywa na serikali ya Somalia na jumuiya ya kimataifa kuleta amani na
utulivu nchini Somalia.
Sabahi: Je, utamruhusu kijana wako kurudi
kufanya kazi Wajir?
Yesse: Oh, ndiyo. Mule ni mtu mzima. Ni Mkenya
mzalendo. Bahati nzuri, kama alivyosema waziri wa Mambo ya Ndani Ole Lenku,
kijana wangu itabidi apate ushauri nasaha wa kina kabla ya kurejea kazini katika
kituo cha kazi atakachochagua.
Sabahi: Ujumbe wowote kwa wazazi wa mateka
wengine?
Yesse: Ndiyo. Wakati wowote kuna matumaini
mwisho wa matatizo. Wazazi wenzangu katika hali ngumu kama hiyo wanapaswa
kumwamini Mungu, kuomba faraja yake katika sala na kuamini kwamba serikali
inajua mambo mazuri kwa ajili ya nchi. Wakati wote serikali ina maslahi mazuri
kwa raia wake licha ya matatizo kama hayo.
Sabahi: Sasa wakati msukosuko huu umepita
kwako, unapanga kusheherekea vipi?
Yesse: Ninaandaa karamu kubwa kwa ajili ya Mule
wiki hii wakati wanafamilia wengine, ndugu na marafiki wanapofika kumuona.
Chanzo - sabahionline.com
Post a Comment