Mkuu
wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Wizara ya Ushirikiano wa
Afrika Mashariki Bi Vedastina Justinian akiongea na waandishi wa habari
kuhusu hatua iliyofikiwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki katika majadiliano ya kuanzisha umoja wa fedha. katikati ni
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari Bi. zamaradi Kawawa,kulia niMchumi
mwandamizi wa Wizara ya hiyo Bw. Emmanuel Mbwambo.
Picha na Frank Mvungi-Maelezo.
……………………………………………………………………………….
Ibara ya 5(2) ya Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki inabainisha kuwa Umoja wa Fedha ni hatua ya tatu ya Mtangamano wa Afrika Mashariki. Madhumuni ya Umoja wa Fedha ni kujenga ukanda tulivu wa kifedha (monetary and financial stability zone)
utakaoharakisha kusaidia ukuaji wa biashara na shughuli za kiuchumi
ndani ya Jumuiya. Katika kufikia malengo haya ya Umoja wa Fedha Nchi
Wanachama, ikiwemo Jumuiya ya Afrika Mashariki, hukubaliana yafuatayo:-
- Kuongeza kiwango na kasi ya mtangamano wa masoko ya fedha na mitaji (deepen financial market integration);
- Kuhuisha sera za kibajeti za nchi Wanachama (harmonisation of national fiscal policies);
- Kuwa na utaratibu wa kuendesha shughuli za uchumi bila kukinzana na malengo ya Umoja wa Fedha;
- Kuunda Benki Kuu moja ya Jumuiya (EACB) itakayosimamia Sera moja ya fedha (single monetary policy) na sera moja ya viwango vya ubadilishanaji fedha (exchange rate policy); na
- Kuanzisha sarafu moja ya Jumuiya;
2.0 HATUA ILIYOFIKIWA
Mchakato wa
uundaji Umoja wa Fedha wa Afrika Mashariki ulianzishwa na Kikao cha 15
cha Baraza la Mawaziri la Afrika Mashariki kilichofanyika mwezi Machi,
2008 baadaye kuidhinishwa na Kikao cha Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya
Afrika Mashariki (Summit). Utafiti wa Umoja wa Fedha ulifanyika,
kukamilishwa na taarifa ya utafiti kujadiliwa na Nchi Wanachama kupitia
Baraza la Mawaziri la Jumuiya ambalo liliunda Kikosi Kazi cha
Majadiliano ya Umoja wa Fedha mwezi Machi, 2010 na Baraza la Mawaziri la
Kisekta la Umoja wa Fedha liliundwa mwezi Novemba, 2010 na kupewa
jukumu la kusimamia majadiliano ili kukamilishazoezi hilo. Hata hivyo,
majadiliano hayo hayakuweza kukamilika mwezi Desemba, 2012 kutokana na
Nchi Wanachama kuhitaji muda zaidi wa kujadiliana na kufikia makubaliano
katika maeneo kadhaa nyeti ikiwemo vigezo vya kuhuisha uchumi mpana (Macroeconomic Convergence Criteria).
Hivyo, Viongozi Wakuu wa Jumuiya walipokutana tarehe 31 Novemba, 2012 waliongeza muda wa majadiliano. Napenda kuwafahamisha kuwa majadiliano hayo sasa yamekamilika
ambapo Rasimu ya Itifaki ya Umoja wa Fedha iliidhinishwa katika Mkutano
wa Dharura wa 27 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya uliofanyika kuanzia
tarehe 17 – 18 Julai, 2013. Hatua inayoendelea ni Itifaki hiyo kupitiwa
na Baraza la Mawaziri la Kisekta la Sheria ili kujiridhisha kama Rasimu
inakidhi matakwa ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Kisheria.
Aidha Rasimu inategemewa kuwasilishwa kwa Viongozi Wakuu wa Jumuiya mwezi Novemba, 2013.
3.0 MAMBO MUHIMU YA KUZINGATIWA
Msingi Mkuu wa Umoja wa Fedha ni Nchi Wanachama kufikia Vigezo vya Kuhuisha Uchumi Mpana (Macroeconomic Convergence Criteria). Vigezo ni:-
- Kiwango cha Juu cha Mfumuko wa Bei kisichozidi asilimia 8 (Ceiling on Headline Inflation of 8%);
- Kiwango cha Juu cha Nakisi ya Bajeti ikijumuisha misaada kisichozidi asilimia 3 ya Pato la Taifa (Fiscal Deficit ceiling including grants of 3% of GDP);
- Kiwango cha Juu cha Deni la Taifa kisichozidi asilimia 50% ya Pato la Taifa (Ceiling on Public Debt of 50% of GDP); na
- Akiba ya Fedha za Kigeni ya kutosheleza mahitaji ya miezi minne na nusu (Reserve cover of 4.5 months of imports).
Tofauti na Itifaki nyingine za Jumuiya
Rasimu ya Itifaki ya Umoja wa Fedha inaainisha kuwa endapo Nchi Tatu
zitafikia vigezo hivyo, Jumuiya ya Afrika Mashariki itaanza kutekeleza
Umoja wa Fedha kwa kuingia kwenye ukanda wa Sarafu Moja, na nchi
nyingine wanachama zitajiunga baadaye, kadiri zitakavyoweza kutimiza
vigezo husika.
Pamoja
na Rasimu ya Itifaki ya Umoja wa Fedha, Jumuiya ya Afrika Mashariki
imeandaa Mpango Kazi wa Utekelezaji wa Umoja wa Fedha. Mpango Kazi huo
umezingatia hatua zinazohitajika katika utekelezaji wa hatua za awali za
Mtangamano, uainishaji wa vigezo vya uchumi mpana (Macroeconomic Convergence Criteria),
na uanzishaji wa Taasisi na Sheria stahiki. Kulingana na Mpango kazi
huu Jumuiya inatarajia kukamilisha yaliyaonishwa katika Mpango kazi na
kuwa na sarafu Moja ya Jumuiya ifikapo mwaka 2024.
Imetolewa na:
WIZARA YA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI
Post a Comment