******
Simiyu. Kwa wengi taarifa za ukosefu wa madawati kwenye shule za
umma na haswa zile za msingi, siyo za kushangaza. Tumezoea kusikia
shule ikiwa na upungufu wa madawati kadhaa lakini siyo kutokuwa na
dawati kabisa kwa miaka takribani 40.
Shule ya Msingi ya Mwaswale iliyopo Tarafa ya
Bumela Wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu, ina historia ndefu ya ukosefu wa
madawati kwa kipindi cha miaka 40 sasa.
Tatizo hilo limekuwa ni kero ya muda mrefu hali
inayowafanya wanafunzi na walimu wake kukata tamaa ya kuendelea na
masomo katika shule hiyo.
Mwaswale ina wanafunzi 1,268 ambao wanalazimika kuketi kwenye mawe kwa sababu ya ukosefu wa madawati.
Shule hiyo ilianzishwa mwaka 1973 ikiwa madawati
80, baada ya muda mfupi yaliharibika na kuifanya kubaki kama makumbusho
kutokana na wanafunzi wake kukalia mawe au matofali.
Mwandishi wa makala hii alipofika shuleni hapo,
alishuhudia wakiwa wameketi kwenye mawe na matofali yaliyopangwa katika
mstari na kuleta mtiririko.
Baadhi ya wanafunzi wanasema hali hiyo inatokana
na wazazi wao kutoshiriki kuchangia maendeleo ya elimu huku wengine
wakiilaumu serikali kwa kushindwa kufuatilia hiyo.
Steven Kwabi anasema licha ya familia nyingi
kujihusisha na kilimo wilayani humo, wazazi hawana mwamko katika suala
la maendeleo ya elimu.
Mwanafunzi huyo anaiomba serikali na wadau wengine
kuwasaidia kupata madawati hali itakayowasaidia kuwaepusha na magonjwa
yatokanayo na vumbi.
“Tukipata madawati tutaepuka magonjwa kama mafua
na hata kifua kikuu, pia itatusaidia kuandika vizuri tofauti na sasa
tunavyoandikia kwenye magoti,” aliongeza.
“Wazazi hawataki hata kuchangia Sh100 za huduma ya
uji kwa miezi sita, akiulizwa anasema mbona shule ya jirani hawanywi
uji,” anasema Kwabi.
Naye Mabula Masunga anayesoma darasa la tano
shuleni hapo, atajisikia vizuri kama shule yake itasaidiwa madawati ili
nao wasome kwa furaha kama watoto wa shule nyingine.
Post a Comment