Ofisa Masoko na Uhusiano wa Mpango wa
Taifa wa Damu Salama, Bw. Rajab Mwenda akizungumza na waandishi wa
habari jana kutoa takwimu za makusanyo ya damu kwa mwezi Aprili mpaka
Juni mwaka huu ambapo ulivuka malengo kwa asilimia 111 kutoka chupa
36,278 mpaka 38,948. Kulia ni Ofisa Msaidizi wa Masoko na Uhusiano Bi.
Rayah Hamad (Picha na Mpiga picha maalum).
*******
MPANGO wa Taifa wa Damu Salama umevuka
lengo la makusanyo ya damu katika kipindi cha mwezi Aprili hadi Juni
mwaka huu kwa kukusanya chupa za damu 38,948 ambazo ni asilimia 111
ikilinganishwa na chupa 36,278 zilizokusanywa kutoka Januari hadi Machi
mwaka huu.
Ofisa Masoko na Uhusiano wa Mpango wa
Damu Salama, Bw. Rajab Mwenda akizungumza jana Dar es Salaam alisema
kanda inayongoza kwa uchangiaji ni Mashariki na Kanda ya Ziwa.
Alisema mafanikio hayo yametokana na
uanzishajiwa mpango wa damu salama wa kampeni ya kuhamasisha uchangiaji
damu kwa hiari katika jamii na kushirikisha wadau.
Bw. Mwenda alisema maadhimisho ya siku
ya wachangia Damu duniani ambapo lengo la kukusanya chupa za Damu 8,500
kutoka kanda sita za mpango wa Taifa wa damu salama liliwekwa na mpango
ulifanikiwa kukusanya jumla ya chupa 8,683
Alisema Mpango wa Damu salama
kushirikiana na wadau mbalimbali kama asasi za kiraia nayo imeongeza
makusanyo ya damu toka vituo vidogo vya kuchangia damu Mnazi Mmoja
jijini Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma kutoka chupa za damu 2,560
mpaka chupa 3,151 kufikia Aprili hadi Juni mwaka huu.
Aliwaomba wadau kuendelea kuelimisha
na kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kuchangia damu kwa hiari kwa
kutumia vyombo vya habari, mitandao ya jamii na vipeperushi.
Bw. Mwenda alisema ushirikiano ni
mdogo kati ya wahamasishaji wa Mpango wa damu salama na viongozi wa
Taasisi mbalimbali, matumizi mabaya ya damu kidogo inayopatikana katika
hospitali zetu na miundo mbinu hafifu hususan barabara mbovu wakati wa
ukusanyaji na usambazaji wa damu.
Alisema changamoto nyingine ni uuzwaji
wa chupa za damu kunakofanywa na baadhi ya watumishi wa hospital ambao
si waaminifu hivyo kukatisha tamaa wachangia damu kwa hiari.
Bw. Mwenda alisema Serikali kupitia
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ilianzisha Mpango wa Taifa wa Damu
Salama mwaka 2005 ili kuhakikisha uwepo wa damu salama na ya kutosha kwa
wote wanaohitaji.
Alisema shughuli za mpango ni pamoja
na uhamasishaji jamii kuhusu uchangiaji damu wa hiari, ukusanyaji
upimaji na usambazaji wa damu salama mahospitalini.
"Mpango wa Taifa wa Damu salama
unafanya kazi kwa kushirikianana kitengo cha kuzuia magonjwa (CDC) na
wadau wengine wa Chama cha Msalaba Mwekundu na Jeshi la Ulinzi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ)" alisema Bw. Mwenda.
Alisema Mpango wa Taifa wa Damu salama
uliweka lengo la kupunguza maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU) katika
damu iliyokusanywa asilimia 1.1 kwa kipindi Aprili- Juni ikilinganishwa
na asilimia 1.2 kipindi cha Januari hadi Machi baada ya kujikita katika
suala la uhamasishaji na kutoa damu toka kwa jamii ambayo ni salama,
kuboresha dodoso la wachangiam damu na kuendelea kuelimisha jamii kuhusu
umuhimu wa kuchangia damu na wachangiaji kujiepusha na tabia hatarishi
ili wawe wachangiaji wa kujirudia.
Post a Comment