Madhumuni makubwa ya maisha ya
mwanadamu ni kufanya juhudi za kutafuta namna ya kuyaelewa mazingira
yake na hivyo kupiga hatua za maendeleo. Juhudi hizo za mwanadamu ndicho
chenye kujulikana kama ' Elimu'. Naam, mwanadamu anapaswa aitafute
elimu, na hivyo basi, maarifa.
********
Shule yaweza kutafsiriwa kuwa ni '
maabara' ambamo hutengenezwa ' chanjo' ya maradhi ya kimaisha kwa
mwanadamu. Wale wenye maarifa na busara za kuandaa ' chanjo' hiyo ndiyo
wanaoitwa walimu.
Maana, shule ni mahali pa kujifunzia,
ambapo yote yenye kuhusiana na maisha ya sasa na hata yajayo
hufundishwa. Ni mahali ambapo hupatikana tafsiri za vitu na matukio
katika jamii. Ni mahali ambapo, mbali ya mambo mengine, mwanafunzi
anapaswa kusaidiwa kupata maarifa ya kujitambua na kuyatambua mazingira
anamoishi.
Tunaweza kabisa kusema, kuwa shule ni
mahali pa ' ibada' na ' viongozi watakatifu' wenye kupaswa kuongoza '
ibada' hizo ni Walimu.
Hata hivyo, kinachofanyika shuleni
hakiwezi kuachwa tu kwa mwalimu. Mzazi ana nafasi kubwa ya kumjenga
mtoto wake aje kuwa mtu wa vitabu. Hakika, maarifa mengi yanapatikana
vitabuni. Binafsi naamini, kuwa moja ya uamuzi mzuri niliyopata
kuyafanya ni hili la kutojihusisha na siasa za majukwaani ili kuwa na
muda zaidi na watoto wangu.
Hakika, miaka kumi ya mwanzo ya makuzi
ya mtoto ni muda muhimu sana katika makuzi yake. Hapo ndipo unajengwa
msingi wa mtoto maishani.
Mzazi unatakiwa kuwa karibu na mtoto
katika miaka yake kumi ya mwanzo, lakini, hata baada ya hapo, kabla
mtoto hajatimiza miaka kumi na minane, bado mzazi unatakiwa kuwa karibu
na mtoto wako. Kujenga misingi ya uhusiano wa mtoto na mzazi, awe mzazi
wa kike au kiume.
Mara nyingi tumefanya makosa kudhani
kuwa uhusiano yanayopaswa kujengwa ni kati ya watu wazima. Kati ya mke
na mume na kati ya mzazi na wazazi wengine. Tunayasahau uhusiano kati ya
mtoto na mzazi.
Tunafanya makosa kuwaachia yaya wa
nyumbani jukumu la kulea watoto wetu. Tunafanya makosa pia, kuwaachia
walimu tu, jukumu la kufuatilia mienendo ya elimu ya watoto wetu.
Wazazi wa kiume tumekuwa mfano mbaya sana wa kuliacha jukumu la kulea kwa mzazi wa kike.
Hakika, mtoto, awe wa kike au kiume,
anahitaji sana kuwa karibu na mzazi wa kiume pia. Kuwa na uhusiano ya
kirafiki pia. Kazi ya mzazi haipaswi kuwa ni ya kukaripia watoto tu,
bali kuwa rafiki nao, kuwa na muda wa kucheka nao. Kubwa zaidi, uwa
tayari kujifunza kutoka kwa watoto.
Mtoto anaweza kuwa mwalimu mzuri kwa mzazi, kama mzazi atamwandalia mtoto mazingira ya kuifanya kazi ya ualimu kwa mzazi wake.
Niwe mkweli, kuwa nimejifunza mengi kutoka kwa watoto wangu kama wao wanavyojifunza kutoka kwangu.
Nilipata kumkuta mtoto wangu akisoma
kitabu . Nikamwomba anisimulie kidogo juu ya anachosoma. Alipoanza
kunisimulia, basi, nilijikuta nataka kumsikiliza zaidi. Kinahusu mtoto
ambaye wazazi wake walitengana. Mzazi mmoja anaishi Marekani na mwingine
Canada.
Mtoto huyu aliondoka kwa mama yake Marekani ili aende kumwona baba yake Canada. Alipanda ndege ndogo. Alikuwa yeye na rubani tu.
Huko angani rubani akapatwa na mshtuko
wa moyo. Mtoto huyu akalazamika kuongoza ndege hiyo. Aliongoza huku
ndege ikipotea angani. Mwisho ndege ikaishiwa mafuta, maana hakujua hasa
namna ya kuongoza ndege.
Ndege ikaanguka ziwani. Bahati njema
mtoto aliweza kuogelea na kunusurika. Akalikuta pango, hapo akaanza
kutafuta mbinu za kuishi akisubiri msaada wa kuokolewa... Kisa
kinaendelea..!
Tunajifunza nini?
Umuhimu wa wazazi kuwajengea watoto
wetu utamaduni wa kujisomea. Mimi niliwasomea vitabu watoto wangu tangu
wangali wadogo sana. Hivyo, nikawajengea hamu ya kusoma.
Si ajabu, kuwa leo wanasoma vitabu
kiasi cha hata kuweza kunisimulia ya kwenye vitabu ambavyo nisingeweza
kuviona maishani mwangu. Kuna ninayojifunza. Hivyo, watoto wangu
wanakuwa walimu wangu pia.
Naam, mtoto wako ni mwalimu wako pia, hivyo, ili awe mwalimu mzuri zaidi, tunapaswa kumjenga aje kuwa mtu wa vitabu.
Nahitimisha.
chanzo:mwananchi
Post a Comment