Na HEZEKIEL
GIKAMBI akiwa Bukoba, Tanzania
Msomi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma amependekeza
mwandishi mashuhuri Shaaban Robert atunukiwe shahada ya Udaktari ya Sanaa katika
Lugha na Fasihi ya Kiswahili. Athumani Ponera alitoa pendekezo hilo kwenye
kongamano la kuadhimisha miaka 50 tangu kufariki kwa Roberts.
Bw Iqbal Shaaban
Roberts, mwanawe mwandishi maarufu wa riwaya na mashairi Shaaban bin Roberts
katika kongamano la kumbukumbu lililoandaliwa mjini Bukoba nchini Tanzania
kuadhimisha miaka 50 tangu kufariki kwa babake. Picha/Hezekiel
Gikambi
KONGAMANO la kumbukumbu za miaka 50 la kumuenzi
Shaaban Robert linaloendelea mjini Bukoba, nchini Tanzania lilipata nguvu mpya
hii leo kupitia kwa wasilisho la msomi Athumani Ponera wa Chuo Kikuu cha Dodoma
aliyetoa pendekezo la kumtunuku mwandishi mashuhuri Shaaban Roberts shahada ya
Uzamivu (Udaktari) ya Sanaa katika Lugha na Fasihi ya Kiswahili.
Mwandishi huyu maarufu wa riwaya na mashairi
Sheikh Shaaban Suleiman Ufukwe bin Roberts al-maarufu Shaaban Robert
anatambulikana kote ulimwenguni kama jemedari wa kukitetea Kiswahili na baba wa
Fasihi ya Kiswahili.
Wapenzi wa Kiswahili, wanafunzi, walimu pamoja
na wasomi kutoka vyuo mbali mbali nchini Kenya Tanzania, Ghana na Uganda
walishangilia hoja za Bwana Ponera ambazo mwishowe zilijikuta katika maazimio ya
Kongamano liliandaliwa kumuenzi msomi huyu aliyeaga Dunia miaka 50
iliyopita.
Maadhimisho hayo yalifanyika katika ukumbi wa
St.Francis mjini Bukoba, mkoani Kagera, nchini Tanzania kwa ushirikiano kati ya
Chama cha Usanifu wa Kiswahili na Ushairi Tanzania (UKUTA) , Baraza la Kiswahili
la Taifa (BAKITA), Ofisi ya Utamaduni Mkoani Kagera na Taasisi ya Taaluma za
Kiswahili TATAKI, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Bwana Ponera ambaye pia ni
mwanafunzi wa shahada ya udaktari katika Fasihi ya Kiswahili na mhadhiri katika
Chuo Kikuu cha Dodoma, Watanzania wengi waliojitolea kuleta mchango mkubwa kwa
taifa wamesahauliwa.
Alisema kuwa kuna orodha ndefu ya mashujaa
waliosahauliwa na hata kuanza kutoweka katika akili za wanajamii licha ya kuwa
waliitangaza nchi yao kupitia fani mbalimbali.
Alitoa mifano ya watu waliotunukiwa shahada za
aina hiyo kwa mchango wao katika jamii nchini Tanzania kama Daktari Rashid
Mfaume Kawawa na Rais Jakaya Mrisho Kikwete. Nchini Kenya pia, tulishuhudia Rais
Mstaafu Mwai Kibaki na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga wakitunukiwa shahada
za heshima na vyuo kadhaa humu nchini na hata nje ya nchi.
Ilisemekana kuwa Shaaban Roberts alikuwa na
mchango mkubwa kisiasa alipoonesha uzalendo wake katika kupigania nchi yake
dhidi ya ukoloni na wakoloni, kijamii kwa kuwa na tabia ya uchangamfu, heshima
na upendoa kwa watu waliomzunguka bila kubagua rangi, umri wala jinsia na pia
kiutamaduni kwa kuwa mwalimu na mtetezi wa sanaa ya lugha kwa kubobea katika
maongezi yake na kuyayakinisha katika maandishi yake.
Kongamano hili pia liliazimia Kiswahili
kutumika kufundishia katika vyuo vikuu na sekondari kama ilivyoazimiwa miaka
hamsini iliyopita. Wataalamu wa Kiswahili wakiongozwa na Prof Mugyabuso
Mulokozi, Prof. Aldin Mutembei na Prof Rubanza, wote wa chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, walipendekeza utafiti ufanywe ili kutambua kwa nini utekelezaji wa
azimio hilo uliokwisha fikiwa tatizo liko wapi?
Maadhimisho Kenya
Ili kumuenzi Shaaban Robert iliazimiwa pia ni
vyema sasa kutenga chumba kimoja kwa ajili ya kuweka kumbukumbu zake kumuenzi
katika shule yenye jina lake,(Shule ya sekondari ya Shabani Robert) jijini Dar
es Salaam na pia ikaafikiwa kwamba maadhimisho ya kumbukumbu ya Shaaban Robert
yafanywe kwa zamu katika kanda mbali mbali za Afrika.
Washiriki wa Kongamano hili waliunga mkono
kauli ya kufanya maadhimisho ya Shaaban Roberts nchini Kenya kama
ilivyopendekezwa na mwandishi wa Kiswahili Ustadh Wallah bin Wallah
aliyehudhuria.
Baadhi ya mawasilisho waliowasisimua washiriki
ni pamoja na lile la mhariri wa gazeti la mapenzi ya Mungu Sheikh Mahmood Hamsin
Mubiru aliyetoa mifano ya beti za Mashairi bila kusoma kokote na kueleza
alivyotangamana na watu walioishi na marehemu Shaaban Roberts alipokuwa akieleza
jinsi Shaaban alivyohusiana na Washairi wenzake.
Makala ya Prof. Ken Walibora yaliyowasilishwa
na mwandishi wa Makala hii pia yalizua mjadala mkubwa kwa kuwa alionyesha jinsi
wanariwaya wa sasa wameeathiriwa na Shaaban Robert na hata akakiri kuwa mwenyewe
ameathiri na Gwiji huyu mtangulizi.
Katika kufunga rasmi kongamano hili, Katibu
Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) Dkt. S.S.Sewangi, aliwashukuru
Sheikh Msakanjia wa Chama cha UKUTA, TATAKI na Mwalimu Wallah bin Wallah na
wadau wote waliofanikisha Kongamano hilo.
Via - swahilihub.com
Post a Comment