Dar es Salaam. Kamati ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC), imesema itawafikisha kwenye Kamati ya Maadili ya Bunge, Waziri
wa Ujenzi, Dk John Magufuli, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu
na Bunge), William Lukuvi na Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe
akiwatuhumu kwa kulidanganya Bunge.
Mjumbe wa Kamati
ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee akitoa
hoja yake wakati kamati hiyo ilipokutana na Shirika la Nyumba nchini (NHC)
jijini Dar es Salaam jana. Kulia ni Mbunge wa viti Maalum (CHADEMA) Suzan
Kiwanga. Picha na Rafael Lubava
Hatua hiyo ilitangazwa jana na Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe baada ya kumhoji Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Herbert Mrango kuhusu hati ya mashaka waliyoipata kutoka kwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), mwaka wa fedha 2011/2012.
Hatua hiyo ilitangazwa jana na Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe baada ya kumhoji Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Herbert Mrango kuhusu hati ya mashaka waliyoipata kutoka kwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), mwaka wa fedha 2011/2012.
Kamati hiyo ilieleza kuwa kwenye Bajeti ya
mwaka huo kiasi cha Sh348,075,000,000 fedha za ndani zilizokuwa zimetengwa chini
ya fungu lililotajwa kuwa ni la mradi maalumu (Special Road Construction
Project) hazikutumiwa kwa malengo yaliyoelezwa bungeni.
“Ni vizuri leo uiambie kamati fedha hizi
ziliombwa kwa kitu gani na zilitumika kwa jambo gani. Tunajua kwamba fedha hizi
zilipunguzwa kiasi cha Sh95 bilioni na kupelekwa Wizara ya Uchukuzi, zilibakia
Sh252.975bilioni katika kifungu hicho lakini kuna bilioni 100 zimetumika
visivyo,” alisema Zitto, ambaye pia ni Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini
(Chadema).
Alisema katika majumuisho ya Bajeti ya wizara
hiyo, Dk Magufuli na Dk Mwakyembe wakati huo akiwa Naibu Waziri wa Ujenzi na
Lukuvi walitoa maelezo yasiyo ya kweli bungeni kuhusu fedha.
Alikariri maneno yaliyorekodiwa kwenye Hansard
ya Bunge yaliyosemwa na viongozi hao watatu.
“Tunaomba fedha Sh252 bilioni kwa ajili ya
kuanzia kazi za ujenzi wa barabara,” Zitto alisema akikariri maneno ya Dk
Magufuli wakati anawasilisha bajeti.
“Fedha hizi zitachangia miradi ya wafadhili,”
haya yalikuwa maneno ya Dk Mwakyembe wakati akifanya majumuisho.
“Hizi ni fedha kwa ajili ya counterpart fund,”
alimkariri Lukuvi wakati akichangia hotuba ya wizara hiyo.
Zitto alisema CAG alihoji mwaka huu kuhusu
matumizi ya fedha hizo na alitoa taarifa akidai kuwa fedha hizo zilikuwa miradi
hewa na kasma kivuli.
Zitto alisema kuwa Dk Magufuli na Katibu Mkuu
wake walipohojiwa walidai kutumia fedha hizo kulipa madeni.
“Kwa nini mlidanganya Bunge? Mliomba fedha za
kuanza miradi maalumu. Hamkuomba fedha za madeni. Kwa nini mliunda kasma kivuli
na kuifuta baada ya pesa kulipwa?” Zitto alimhoji Balozi Mrango.
Katika majibu yake, Balozi Mrango alisema kwa
nia njema, fedha hizo zilitumika kuwalipa makandarasi waliokuwa wamechachamaa,
huku baadhi yao wakisisitiza kusitisha kuendelea na miradi. Hivyo wakalazimika
kuomba fedha kwa njia hiyo ili miradi kuendelea katika maeneo mbalimbali ya
nchi.
Zitto hakuridhishwa na majibu hayo akisema
hapakuwa na haja ya kutumia fedha hizo kuwalipa makandarasi wakati kulikuwa na
kasma yao ya awali. Alisema kama kulikuwa na haja hiyo, wizara isingeita mradi
rasmi.
“Jambo hili siyo sahihi hata kidogo
kulidanganya Bunge na hadi sasa wewe na waziri wako hamuonyeshi kukubali kosa
hili, hata Waziri Lukuvi naye alisisitiza bungeni kwamba fedha hizo zinaombwa
ili kutekeleza mradi maalumu lakini sasa imebainika sivyo, kwa mujibu wa Kanuni
za Bunge tutawafikisha kwenye Kamati ya Maadili ili wahojiwe nao wajieleze kwa
kulidanganya,” alisema Zitto.
Pia kamati hiyo imeitaka wizara hiyo kutoa
ufafanuzi wa kina kuhusu matumizi ya Sh100 bilioni zilizotumika kinyume na
maombi yaliyowasilishwa kwenye Bajeti ya mwaka huo wa fedha.
CAG ameshauri madeni yote ambayo Wizara ya
Ujenzi inadaiwa yaorodheshwe ili yawe wazi kuepuka migongano katika matumizi ya
fedha.
Alipoulizwa kuhusu madai hayo, Lukuvi alisema
haelewi chochote na kusisitiza kuwa akipata taarifa rasmi za Kamati ya PAC,
atatoa ufafanuzi.
Halmashauri zinavyotafuna mabilioni
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali
za Mitaa (LAACc), imeeleza namna mamilioni ya fedha za Serikali zinavyoibwa
kutoka Hazina kupitia halmashauri za wilaya huku Ilala ikitajwa kuongoza kwa
ufisadi huo.
Mwenyekiti wa LAAC, Rajab Mbarouk Mohammed
aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba Hazina imekuwa ikipeleka fedha kwenye
halmashauri zikiwa zimezidi na kwamba kiasi kinachozidi hakirudishwi badala yake
huliwa.
Alisema kamati hiyo imefanya uchunguzi kwenye
halmashauri 43 na kubaini kwamba mtindo huo ndiyo unaotumika kuiba fedha za
Serikali.
“Mwaka 2011/12 kiasi cha Sh1.5 bilioni
zilipelekwa zikiwa zimezidi kwenye halmashauri hizo lakini hazikurudishwa Hazina
kama inavyoonyesha kwenye ripoti ya CAG.
Alisema kati ya kiasi hicho, Halmashauri ya
Manispaa ya Ilala ilipewa ziada ya Sh213 milioni ikifuatiwa na Geita iliyopewa
Sh129 milioni.
“Fedha hizo za mishahara zilipelekwa kwenye
halmashauri hizo na Hazina kimakosa zikiwa zimezidi lakini watendaji wa
hawakuzirudisha kama wanavyotakiwa kisheria badala yake zikayeyuka,”
alisema.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa uchunguzi huo pia
ulibaini kwamba katika halmashauri hizo 43 kiasi cha Sh693 milioni hulipwa
mishahara hewa ambayo wafanyakazi wake walishakufa na wengine kustaafu.
Alisema Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema
ililipa mishahara hewa yenye thamani ya Sh79.4 milioni ikifuatiwa na Ukerewe
iliyolipa Sh57.5 milioni.
Kwa upande wa fedha za miradi ya maendeleo,
mwaka 2011/12, Hazina ilipeleka katika Halmashauri ya Mbarali, Mbeya Sh724
milioni kwa ajili ya Mradi wa Maendeleo ya Elimu Sekondari wakati mradi huo
ulikuwa ukihitaji Sh70 milioni tu.
“Kiasi cha Sh654 milioni zilipelekwa kimakosa
na Hazina lakini badala ya kurudishwa zilitumiwa katika mazingira ya
kutatanisha,” alisema.
Alisema Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe
ilipelekewa ziada ya Sh500 milioni na Mvomero ilipewa Sh85 milioni. “Kuna
mtandao mkubwa wa Hazina na halmashauri ambao ukiachwa utaendelea kupoteza fedha
nyingi za walipakodi,” alisema.
Chanzo - Mwananchi
Chanzo - Mwananchi
Post a Comment