Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi Nape Nnauye akizungumza na waandishi wa
habari leo, katika Ukumbi wa Sekretarieti, Ofisi Ndogo ya Makao Makuu
ya CCM, Mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam.Picha na Bashir Nkoromo
--
--
NA MWANDISHI WETU
CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM) kimesema bado
kina imani na Tume ya Mabadiliko ya Katiba nchini, katika mchakato
unaoendelea wa kupata katiba mpya.
Imesema licha ya CCM kutofautiana
kimawazo katika baadhi ya maeneo katika rasimu ya kwanza ya katiba
iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, lakini haina ugomvi na tume
hiyo.
Hayo yamesemwa na Katibu wa NEC, Itikadi
na Uenezi Nape Nnauye wakati akizungumza na waandishi wa habari katika
ukumbi wa Sekretarieti, Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Mtaa wa
Lumumba jijini Dar es Salaam.
"Tunawaheshimu sana wajumbe wa tume
hii, na kwa kweli tunamatumaini nao sana kuwa watatimiza wajibu wao kwa
weledi mkubwa", alisema Nape.
Nape alibainisha kwamba pamoja na
maeneo mengine ya rasimu ya kwanza ya katiba , CCM ina mawazo tofauti
kwenye suala la Muundo wa Muungano ambapo wakati rasimu inapendekeza
muundo wa serikali tatu, CCM yenyewe inapendekeza serikali mbili.
"Kama mnavyoona katika hili, wakati tume
inapendekeza muundo wa serikali tatu sisi CCM tunapendekeza muundo wa
serikali mbili, lakini hii haitufanyi tuwapuuze au tugombane na wale
wenye mawazo tofauti na yetu", alisema Nape na kuongeza;
"Kumekuwepo na ripoti na makala kadhaa
zinazojaribu kuonyesha kama vile kuna mvutano kati ya tume na CCM, au
CCM na wengine wenye mawazo tofauti na CCM. Ukweli ni kuwa hali hiyo
inayojaribu kujengwa kwa nguvu si ya kweli. Tuache hoja zishindane kwa
hoja na nguvu ya hoja ndio iwe msingi wa ushindani".
Nape alitaka ushindani uwe kwenye hoja bila kushutumiana ili jatimaye mawazo ya wengi yasikilizwe na kuzingatiwa.
Alisema, CCM inasisitiza kuwa itaheshimu
mawazo ya Watanzania, kwani katiba inayotengenezwa ni ya watanzania
wote bila ya kujali itikadi zao.
"Naomba nichukue nafasi hii kuwashukuru
wale wote wanaounga mkono baadhi ya hoja za CCM hasa hoja ya serikali
mbili. Tumeshuhudia maoni ya wajumbe wengi wa mabaraza na wananchi kwa
ujumla wakiunga mkono mawazo haya ya CCM ya muundo wa muungano wa
serikali mbili na hoja kadhaa zingine", alisema Nape na kuongeza;
"CCM tunapenda kuwashukuru wote. Tujadili kwa kuvumiliana, tukipendana na kuheshimiana. Tanzania yenye neema tele inawezekana".
Post a Comment