Ndugu zangu,
Kwa mwanadamu, mila yake ndio dini
yake ya kwanza. Kwa Mwarabu na Mzungu sawia, Uislamu na Ukristo uliingia
katika jamii hizo na kuzikuta jamii hizo zikiwa na mila zao.
Na sisi Waafrika vivyo hivyo, tuna
mila zetu. Uislamu na Ukristo ni imani za kimapokeo. Hakuna dhambi kwa
mwanadamu kupokea imani mpya. Hata hivyo, ni vema kwa anayeipokea akawa
pia amejitambua, kuwa naye pia ana mila zake. Na mwanadamu anayeikana
asili yake ni mtumwa.
Uafrika ni imani. Uafrika umejijenga
katika upendo na ujamaa. Ndio maana Mwalimu aliijenga TANU na nchi yetu
katika misingi ya Ujamaa wa Kiafrika, hivyo basi itikadi. Ni tofauti
kabisa na Ukomunisti.
Mathalan, Afrika unapokuwa safarini na
jua likazama, basi, Mwafrika hutafuta yalipo makazi ya watu. Afrika
safari zetu nyingi ni za miguu, na kwa kawaida hatutembei usiku.
Na jua likizama na ukakutana na
Mwafrika mwenzako kwenye mji wake, husemi kuwa unataka kusaidiwa pa
kulala na mengineyo. Kwa mila zetu, utasema; " Mwenzenu niko safarini na
jua limezama nikiwa hapa".
Kwa Mwafrika, hapo umehitaji msaada.
Mwenyeji ataandaa pa wewe kulala. Utaandaliwa chakula na hata maji ya
moto ya kuoga. Atakayefanya ukarimu huo hatajali kama wewe ni Mkristo,
Muislamu, au wa kabila tofauti na yeye.
Na asubuhi kukipambazuka, utapewa
kijana wa kukusindikiza kilomita zipatazo mbili. Uendelee na safari
yako. Ndio, Uafrika ni imani iliyojengeka katika misingi ya upendo,
umoja na kusaidiana bila kubaguana.
Na katika hili la misuguano ya kiimani
kwenye jamii. Misuguano inayotokana na dini hizi za kimapokeo; Uislamu
na Ukristo. Imefika mahali, kwa makusudi kabisa, tuandae mitaala ya
kufundisha mashuleni maarifa ya imani tofauti za humu duniani.
Huko mashuleni watu wote wafundishwe,
na waalimu mahiri, juu ya masuala ya imani za humu duniani, ikiwamo
dhana ya Uafrika kama imani pia.
Maana, mingi ya misuguano hii inatokana na watu kukosa maarifa, au kuwa na maarifa haba sana.
Naam, Afrika jua linapozama unamtafuta Mwafrika mwenzio, bila kujali dini au kabila lake.
Ni Neno La Leo.
Maggid,
Iringa.
Maggid,
Iringa.
Post a Comment