SIKU chache baada ya kukamatwa kwa
askari 'feki' wa Usalama Barabarani mwenye cheo cha Sajini, akifanya kazi ya
kuongoza magari eneo ya Tabata Kinyerezi, Dar es Salaam, mambo mapya yamezidi
kubainika juu ya sababu za mtu huyo kujiingiza katika kazi hiyo bila kutambuliwa
na Jeshi la Polisi.
Habari zilizolifikia gazeti hili kutoka vyanzo vya
kuaminika, zinasema trafiki huyo 'feki', ambaye inadaiwa jina lake halisi ni
James Juma Hussein (45), mkazi wa Kimara Matangini, alianzia kazi hiyo mkoani
Singida kabla ya kujipa uhamisho wa kikazi kwenda Dar es Salaam.
Chanzo chetu kilieleza kuwa, trafiki huyo alikuwa na
shemeji yake aliyeitwa Shaban ambaye aliajiriwa na Jeshi la Polisi Kitengo cha
Usalama Barabarani aliyekuwa akifanyia kazi mkoani
Tabora.Vyanzo vyetu viliongeza kuwa, baada ya shemeji yake
kufariki mkoani Tabora, trafiki huyo alipata mwanya wa kuchukua nguo za kazini
alizokuwa akizitumia shemeji yake.
Inadaiwa trafiki huyo 'feki', aliwahi kupata mafunzo ya
upolisi katika Chuo cha Polisi Moshi (CCP), mkoani Kilimanjaro lakini
alifukuzwa.Chanzo hicho kiliongeza kuwa, baada ya ndugu wa trafiki
huyo kufariki dunia, trafiki 'feki', alikuwa akifanya kazi hiyo bila ndugu zake
kujua akianzia mkoani Singida bila kushtukiwa.
"Jamaa aliamua kujirithisha kazi ya shemeji yake, alikwenda
Singida na kufanya kazi hiyo kwa muda usiojulikana," kilisema chanzo
chetu.Chanzo hicho kiliongeza kuwa, kutokana na uchache wa
matrafiki mkoani Singida, aliingiwa hofu ya kuweza kujulikana; hivyo aliamua
kujipa uhamisho wa kwenda jijini Dar es Salaam.
"Akiwa Dar es Salaam, alifanya kazi hii kwa muda mrefu bila
kujulikana hadi alipokamatwa wiki iliyopita akiwa eneo lake la kazi akiongoza
magari," kilisema chanzo hicho.Mtoa habari huyo alisema polisi walianza kumtilia shaka
trafiki huyo kutokana na adhabu zake alizokuwa akizitoa kwa madereva.
"Tulianza kuwa na hofu naye kwa sababu yeye adhabu zake kwa
kila dereva aliyekuwa akimkamata alimtoza sh. 20,000 hadi 25,000," kilieleza
chanzo hicho.Sababu nyingine iliyowafanya polisi wamtilie shaka ni
utamaduni wake wa kuondoka mapema kwenye kituo cha kazi ambavyo alikuwa
akijipangia mwenyewe.
"Trafiki akiwa kazini, inabidi awe kituoni kwake kuanzia
asubuhi hadi jioni muda wa kazi unapomalizika, tulishangaa kuona mwenzetu
anaingia kazini asubuhi na kuondoka kabla ya muda wa kazi," kiliongeza chanzo
hicho.Inadaiwa trafiki huyo alikuwa akifanya hivyo baada ya
kukamilisha mahesabu yake aliyokuwa amejiwekea ambapo hali hiyo iliwafanya
polisi waanze kujiuliza maswali na ndipo walipoanza kumfuatilia.
Baada ya kufuatiliwa bila yeye kujua, walibaini hata
upigaji wake wa saluti ni utata mtupu ambapo kutokana na hali hiyo, waliweka
mtego na kufanikiwa kumkamata.
Hadi sasa anaendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi ambalo
limeahidi kutoa taarifa kamili baada ya uchunguzi wao
kukamilika
Post a Comment