Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

Al Shabab yalipua tena Kenya ... Hali ni tete

 


*Kituo cha polisi chashambuliwa
*Wawili wauawa, magari 11 yachomwa
*Magaidi walikodi Westgate kuficha silaha

WAKATI mapya yakiibuka kuhusu shambulio la kigaidi dhidi ya Kituo cha Biashara cha Westgate mjini Nairobi, watu wanaoshukiwa kuwa magaidi wameshambulia kituo cha polisi katika mji wa Mandera na kuua maofisa wawili wa polisi jana asubuhi. Tukio hilo lililotokea katika mji huo ulio karibu na mpaka wa Somalia pia lilijeruhi maofisa wengine watatu huku magari 11 yaliyokuwa kituoni hapo yakiteketezwa kwa moto.

Shambulio hilo ambalo ni la pili katika siku moja baada ya watu wenye silaha kuua mtu mmoja na kujeruhi wengine katika mji wa Wajir juzi usiku, ni mlolongo wa matukio ya ugaidi yanayofanywa na wanamgambo wa Somalia wa Al-Shabaab.

Washambuliaji walirusha roketi katika Ofisi ya Mkuu wa Polisi mjini humo na kuiteketeza kabla ya kutoroka katika tukio lililotokea saa 9.00 alfajiri.


Ofisa wa Polisi Kanda ya Kaskazini Mashariki, Charlton Mureithi alisema watu hao wenye silaha walivamia wakati sehemu kubwa ya maofisa wa kituo hicho wakiwa wamelala.

“Wamesababisha uharibifu mkubwa na vifo kabla ya kutoroka, lakini tuna matumaini watakamatwa,” alisema.

Washambuliaji waliripotiwa kuwashtukiza maofisa waliokuwa kituoni hapo wakiwa hawajui hili wala lile na kuwapiga risasi kwa karibu.

“Waliyamwagia petroli magari yaliyokuwa kituoni na kuyateketeza kwa moto. Baadaye walirusha bomu la kutupa kwa mkono kuelekea jengo la kituo kabla ya kutoroka,” Mureithi alisema.

Maofisa waliojeruhiwa walitarajiwa kupelekwa mjini Nairobi kwa matibabu zaidi baadaye jana.

Katika shambulio jingine lililotokea mjini Wajir, mtu mmoja aliuawa na wengine wanne kujeruhiwa baada ya bomu na risasi kurushwa katika umati na watu wenye silaha saa 1.00 usiku juzi.

Mmoja wa washambuliaji ambaye alijeruhiwa na bomu la kutupwa kwa mkono lililoripuka, alikamatwa baadaye na anaisaidia polisi.

Wakati huo huo, mapya yameibuka kuhusu shambulio la ugaidi katika jengo la Westgate baada ya kubainika kuwa magaidi walikodi duka moja katika jengo hilo kwa miezi mitatu, kitu kilichowawezesha kulisoma vema.

Taarifa hizo zinakuja huku maofisa wa usalama wa Uingereza wakihaha kupata ukweli wa uhusika wa raia wake katika shambulio hilo akiwamo mwanamke anayejulikana kama Mjane Mweupe, Samantha Lewthwaite, ambaye alikuwa mke wa mtu aliyejitoa mhanga katika shambulio la Julai 7, 2005 nchini Uingereza, Jermaine Lindsay.

Timu za uchunguzi za Uingereza, Marekani na Israel zinaendelea kushirikiana na Wakenya kusaka ukweli juu ya uraia wa magaidi kupitia vinasaba vya damu (DNA) na alama za vidole.

Shauku kubwa ya timu hiyo ni kubainisha iwapo mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 29 kutoka Aylesbury, Buckinghamshire, ni miongoni mwa waliokufa.

Mashuhuda mbalimbali wameeleza kumwona mwanamke wa kizungu akiamrisha wenzake akiwa na bunduki huku wengine wakisema hakuwa na bunduki ila aliongozana na vijana wawili wenye silaha.

Lewthwaite anatafutwa Kenya akidaiwa kushiriki mashambulio kadhaa ya ugaidi kwa hoteli za utalii na migahawa nchini humo.

Mipango ya shambulio dhidi ya hoteli za mataifa ya Magharibi mjini Mombasa inasemekana inafanana na ule wa Westgate, ambao umeripotiwa kupangwa wiki au miezi kadhaa katika ardhi ya Somali na kundi la Al Shabab.

Imeripotiwa kwamba wapiganaji wa kigeni wanaozungumza Kiingereza walichaguliwa kwa uangalifu na mipango ya kukisoma kituo hicho pia ililenga mabomba ya kupitishia hewa.

Timu hiyo ya magaidi ilipita kwa urahisi bila kubainika katika mpaka wa Kenya, ambako mara nyingi hulindwa na walinzi wanaolipwa mishahara midogo au yenye walinzi wanaonuka rushwa.

Baada ya mipango yao kwenda vema walikodi kwa mkataba wa miezi mitatu duka moja la nguo za wanawake siku moja au mbili kabla ya shambulio, wakilitumia kufichia silaha zao nzito.

Mmoja wa magaidi ameripotiwa kushuhudiwa akitoroka pamoja na walionusurika baada ya kubadili nguo katika duka hilo.

Gaidi mmoja aliyekuwa na silaha kali ndiye aliyekuwa kikwazo kwa vikosi vya usalama vya Kenya baada ya kuwazuia kupanda katika ghorofa ya pili kwa karibu saa 24 kabla ya jengo hilo kudhibitiwa saa 11 .45 asubuhi Jumanne.

Gaidi huyo alipigwa risasi na mlenga shabaha wa Kenya alipotanguliziwa bomu.

Katika harakati za kufanikisha operesheni yao, Jeshi la Kenya lilizima taa na video za usalama (CCTV) ambazo magaidi walikuwa wakizitumia kabla ya kuwaua washambuliaji waliobaki.

Wakati hayo yakijiri, picha mpya za video zimepingana na kauli ya Jeshi la Kenya kuwa ghorofa ya tatu ilianguka baada ya magaidi kuteketeza moto magodoro yaliyokuwa eneo hilo.

Picha hizo zilionyesha shimo katika paa la juu baada ya ghorofa ya tatu kuporomoka wakati askari wa Kenya waliporusha roketi katika harakati za kumaliza mapambano na magaidi. Roketi hilo lilisambaratisha nguzo ya sakafu hiyo ya tatu baada ya kuelemewa na uzito.

Kupitia mtandao wa Twitter, Al Shabab, lilidai jeshi la Kenya ndilo lililoporomosha jengo hilo baada ya kukata tamaa kuhusu njia ya kuwakamata au kuwaua magaidi waliobakia pamoja na mateka.

Magaidi hao pia walizituhumu mamlaka za Kenya kuwa zilitumia kemikali za sumu kuwashinda wapiganaji wake, madai ambayo serikali imekana vikali.

Habari nyingine zinasema, watalaamu wa Kenya na wa kigeni jana walikuwa wanaendelea kufanya uchunguzi katika jengo la Westgate huku kukiwa na sintofahamu kuhusu idadi ya watu waliouawa katika tukio hilo lililodumu kwa siku nne.

Hadi sasa watu 67 wanathibitika waliuawa katika tukio hilo.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya, Joseph ole Lenku alisema hafikirii kama idadi ya waliokufa itaongezeka kwa kiasi kikubwa, lakini anaamini kuwa miili itakayopatikana katika mabaki hayo ni ya magaidi pekee.

Hata hivyo, Chama cha Msalaba Mwekundu cha Kenya kilisema watu 61 bado hawajulikani waliko.

Wakati huohuo, Kenya jana iliendelea na siku tatu za maombolezo kwa watu waliokufa katika shambulio hilo.

Mazishi ya mwandishi wa habari wa televisheni na redio ambaye alikuwa mjamzito, Ruhila Adatia-Sood ni miongoni mwa yaliyofanyika jana.

Bendera ziliendelea kupepea nusu mlingoti huku ulinzi ukiwa umeimarishwa mjini Nairobi. Maofisa usalama walikuwa wakiwapekuwa watu kwa vifaa maalum kabla ya kupanda mabasi ya abiria.

Huku kukiwa na wasiwasi mkubwa kuhusu uwezo wa Kenya wa kuwa na tahadhari dhidi ya matukio ya aina hiyo, zipo taarifa kuwa mbinu za nchi hiyo za kukabili na kupambana na ugaidi zinaangaliwa upya.

Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top