Dar es Salaam/Zanzibar. Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko, Jaji
Joseph Warioba amesema Watanzania hawatatendewa haki kama itapatikana
Katiba Mpya ambayo haijatokana na maoni yao. “Hakikisheni Katiba Mpya
inayopatikana ni ya maoni ya wananchi,” alisema jana muda mfupi baada ya
kumaliza mkutano wake na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana.
Jaji Warioba alisema maoni yaliyomo katika Rasimu
ya Katiba yametokana na maoni ya wananchi, hivyo lazima yalindwe ili
kudumisha amani... “Kilichomo katika Rasimu ya Katiba ni maoni ya
wananchi, wasije wakafanya makosa ya kutoa maoni haya. Haya yametoka kwa
wananchi na wao ndiyo watakuwa na sauti ya mwisho kuhusu mchakato huu,”
alisema na kuongeza: “Wahakikishe kwamba mawazo yaliyotolewa na
wananchi yanaingia katika Katiba Mpya, wasithubutu kuyatoa maana
wananchi wanaweza kukataa hali hiyo.”
Wakati Warioba akieleza hayo, viongozi wa vyama
mbalimbali vya siasa wameunga mkono kauli ya Jaji Warioba ya kuwataka
kukaa meza moja na kuweka tofauti zao kando.
Vyama vya siasa
Wakati Jaji Warioba akisema hayo, vyama vya siasa vimeendelea ‘kurushiana madongo’ na kushikilia misimamo yake.
CCM kimeonya kuwa mikutano ya hadhara, maandamano
au kumshinikiza Rais Jakaya Kikwete asisaini Muswada wa Sheria ya
Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba mwaka 2013, si ufumbuzi wa
kupatikana Katiba Mpya.
Makamu Mwenyekiti wa CCM, Tanzania Bara, Philip
Mangula alisema jana kwamba muswada huo ulipitishwa na wabunge kwa
mujibu wa sheria baada ya wapinzani kushindwa kujenga hoja na kukimbia,
hivyo kitakuwa ni kitu cha ajabu usisainiwe na kuwa sheria.
“Demokrasia ni wengi wape na wachache wasikilizwe,
ikiwa wengi wameamua wana haki ya kusikilizwa na kuheshimiwa, uchache
wa wapinzani hauwezi kuzuia matakwa ya wengi kukwama,” alisema Mangula.
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John
Mnyika alisema mchakato wa kudai Katiba Mpya uliozinduliwa na vyama vya
upinzani hautarudi nyuma na utazidi kusonga mbele... “Tunamwomba Rais
asisaini muswada huo kama kweli ana nia njema na wananchi wake na sisi
haturudi katika suala hili. Tutarudisha jukumu hilo kwa wananchi waamue
wenyewe.”
Naibu Katibu Mkuu wa (CUF), Julius Mtatiro
alisema: “Tunaunga mkono kauli ya Jaji Warioba, lakini asiseme tuache
kutumia majukwaa kuzungumzia mchakato wa Katiba kwani Katiba siyo jambo
la siri.”
Alisema wanachokifanya ni kuwaelimisha wananchi ili wafahamu mambo yanayoendelea na uchakachuaji unaofanywa na CCM.
Naibu Katibu Mkuu wa NCCR Mageuzi, Samuel Ruhuza
alisema, mikutano wanayoifanya isieleweke vibaya kwani wanatumia njia
hiyo kuwaelimisha wananchi.
MWANANCHI
MWANANCHI
Post a Comment