Waziri
wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Magufuli akikagua eneo la Kitonga katika
barabara ya TANZAM mkoani Iringa. Wengine katika picha ni Naibu Katibu
Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Eng. Joseph Nyamhanga (kulia) na Eng.
Chrispianus Ako kutoka Tanroads Makao Makuu (wa kwanza Kushoto) na
Meneja wa Tanroads wa Mkoa wa Iringa Eng. Poul Lyakurwa (wa pili
kushoto) pamoja na watendaji wengine kutoka Wizara ya Ujenzi.
Waziri
wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Magufuli (katikati) akipewa maelezo na
Meneja wa Tanroads mkoa wa Iringa Eng. Poul Lyakurwa wakati alipokuwa
akipita kukagua eneo la Kitonga katika barabara ya TANZAM mkoani Iringa.
Wengine katika picha ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Eng.
Joseph Nyamhanga (kulia) na Eng. Chrispianus Ako kutoka Tanroads Makao
Makuu (wa kwanza Kushoto) pamoja na watendaji wengine kutoka Wizara ya
Ujenzi.
Kujifunga
kwa barabara katika eneo la Kitonga katika barabara kuu ya TANZAM
kumekuwa kukisababisha adha kubwa kwa wasafiri. Eneo hilo liko mkoani
Iringa katika barabara kuu inayoanzia jijini Dar es Salaam ikiunganisha
na mikoa ya kusini magharibi mwa nchi yetu pamoja na nchi jirani za
Zambia, Congo DR na Malawi.
Barabara
katika sehemu ya Kitonga inapita katika muinuko mkali ambapo inapotokea
ajali au gari kuharibika, huwa ni vigumu kwa magari mengine kupita hadi
gari lilizoba njia liondolewe.
Hivi
karibuni Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli alikutana
na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mheshimiwa Dkt. Christine Ishengoma ambapo
pamoja ya mambo mengine yaliyozungumziwa katika kikao hicho,
lilijitokeza suala la kujifunga mara kwa mara kwa barabara ya TANZAM
katika eneo la Kitonga.
Meneja
wa Tanroads mkoani Iringa Injinia Poul Lwakurwa alimfahamisha Waziri wa
Ujenzi kuwa, pale inapotokea ajali au gari kuharibika na kufunga njia,
husababisha msongamano mkubwa wa magari na hata upelekaji wa msaada huwa
mgumu na huchukua muda mrefu kutokana na wembamba wa barabara katika
eneo hilo pamoja na kutokuwepo kwa barabara mbadala jirani.
Mheshimiwa
Magufuli wakati akihitimisha ziara yake mkoani Iringa alitembelea eneo
la Kitona na kujionea hali halisi na kuiagiza Tanroads kumpatia taarifa
mapema iwezekanavyo juu ya hatua za muda mfupi na muda mrefu ambazo
watachukua ili kuondoa adha hiyo ya kujifunga barabara mara kwa mara.
Mwakilishi
wa Mtendaji Mkuu wa Tanroads aliyekuwepo katika ziara hiyo Injinia
Chrispianus Ako alimtaarifu Waziri wa ujenzi kuwa tayari Tanroads
imaenza mchakato wa kupanua barabara katika eneo hilo ikiwa ni pamoja na
kutafuta barabara mbadala jirani na eneo hilo.
Serikali
tayari imekwishatumia fedha nyingi kuijenga kwa zege sehemu hiyo ya
Kitonga kilometa zote 7 badala ya kutumia lami ya kawaida ili kudhibiti
uharibifu uliokuwa ukisababishwa na magari yanayozidisha uzito au
kumwaga mafuta barabarani. Mafuta hasa petrol na diseli yakimwagika
katika barabara za lami huidhoofisha na kusababisha kubomoka. Hata hivyo
kwa upande wa barabara za zege mafuta husababisha utelezi ambao wakati
wa mvua huweza kusababisha ajali hasa katika maeneo yenye miinuko mikali
kama ilivyo kwa sehemu ya hiyo ya Kitonga.
Post a Comment