Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

RIPOTI kamili kuhusu mauaji yaliyofanyika juzi nchini Kenya pamoja na hali ilivyo kwa sasa

 



VILIO vimeendelea kutikisa nchini Kenya, baada ya kundi la magaidi wa kundi la Al-Shabaab kufanya mauaji ya kutisha jijini Nairobi. Wakati vilio hivyo vikiendelea, jana Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta alilihutubia taifa na kusema wahusika wote watakamatwa na kuchukuliwa hatua zinazostahili.

Akihutubia katika Ikulu ya Nairobi, Rais Kenyetta alisema vita dhidi ya ugaidi siyo ya Wakenya peke yao bali ni ya dunia nzima, kwa kuwa magaidi yanaua watu katika maeneo mbalimbali duniani. Alisema kwamba, Kenya haitarudi nyuma kupambana na ugaidi kwani Serikali yake haitakubali raia wa Kenya wauawe bila sababu.

“Viongozi wote tumesimama hapa tukiomba amani na tunawahakikishia wananchi kuwa tumeweka usalama wa kutosha.

“Hakuna anayependa kusikia ndugu yake amefariki katika shambulio la kutisha kama lile, mimi nimepoteza jamaa zangu wawili, mpwa wangu na mchumba wake.

“Napenda niwahahakishie Wakenya wote, kuwa wana usalama wetu na intelijensia yetu wanafanya kazi kwa umakini, mnachotakiwa ni kuwapa ushirikiano.

“Hatutarudi nyuma katika kupambana vita dhidi ya ugaidi na tunaomba dunia ituunge mkono katika hilo,” alisema Rais Kenyatta.

Wakati wa hotuba hiyo, viongozi mbalimbali wa vyama vya upinzani walikuwapo akiwamo Musalya Mudavadi na Raila Odinga aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo.

Viongozi hao wote, walipewa fursa ya kuzungumza ambapo walilaani tukio hilo kwa nyakati tofauti.

Katika hatua nyingine, Jeshi la Israel jana lilijitosa kusaidiana na askari wa Kenya kuwakabili wanamgambo hao wa Somalia waliojichimbia katika jengo la maduka ya kisasa la Westgate mjini Nairobi.

Hadi gazeti hili linakwenda mitamboni, taarifa zilisema waliopoteza maisha walikuwa ni 57 na wengine zaidi ya 175 walikuwa wamejeruhiwa.

Katika eneo la tukio, milio ya risasi na mizinga ilisikika wakati askari wakijaribu kuwaua au kuwakamata washambuliaji waliokuwa wamesalia ili kumaliza umwagaji damu uliodumu kwa saa karibu 30 katika duka hilo lililopo Barabara ya Mwanzi huko Westlands, karibu na duka jingine maarufu la Sarit.

“Waisrael ndio wameingia na wanawaokoa mateka na watu waliojeruhiwa,” chanzo cha habari cha jeshi la Kenya kilisema.

Hata hivyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel, ilikataa kukanusha au kuthibitisha ushiriki wa jeshi lake katika operesheni hiyo.

Wapiganaji hao wa Al-Shabaab wenye uhusiano na mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda, walidai kushiriki shambulio hilo katika jumba hilo ambalo Waisrael wana sehemu ya hisa.

Wanamgambo hao walisema shambulio hilo ni ulipaji kisasi ili kupinga uwepo wa jeshi la Kenya nchini Somalia ambako jeshi la Umoja wa Afrika (AU) linapambana na makundi ya wanamgambo wa Kiislamu.

Msemaji wa Al-Shabaab, Sheikh Ali Mohamud Rage, alidai walikuwa wameionya Kenya, lakini ikapuuza na kuendelea uvamizi wa ardhi yao kwa nguvu, huku wakiwaua raia wasio na hatia.

Alisema kwamba, wataendelea kufanya mashambulizi nchini Kenya hadi itakapoviondoa vikosi vyake Somalia.

“Iwapo mnataka Kenya iwe na amani, itatokea iwapo tu vijana wenu wataondoka katika ardhi zetu,” taarifa yake katika mtandao wa Twitter ilisema.

Hata hivyo, mtandao huo wa kijamii baadaye uliifunga akaunti yao hiyo.

Ujumbe kutoka Twitter ulisomeka kuwa akaunti hiyo imefungiwa, ikiwa ni mara ya tatu mwaka huu kwa kundi hilo kufukuzwa kutoka mtandao huo.

Kwa mujibu wa Twitter, watumiaji hufungiwa kuutumia iwapo wanatumia akaunti zao kwa malengo mabaya au kulenga shughuli zisizo halali.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya, Joseph Ole Lenku alisema watu 59 walithibitika kufariki huku Shirika la Msalaba Mwekundu likisema idadi ya waliojeruhiwa ni takribani watu 200.

Lenku alisema kulikuwa na wanamgambo kati ya 10 hadi 15 katika kituo hicho cha biashara. ‘Tunaamini kuna idadi ya watu isiyojulikana wasio na hatia katika jengo na ndiyo maana operesheni hii imekuwa ngumu,” alisema.

Kwenye tukio raia wa kigeni kadhaa waliuawa akiwemo mwanadiplomasia mmoja wa Canada.

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, anabiliwa na changamoto yake kuu ya kwanza ya usalama tangu achaguliwe Machi mwaka huu.

Katika hotuba yake katika televisheni juzi, Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta alisema alipoteza mmoja wa jamaa zake katika shambulio hilo.

Hata hivyo, baadaye ilifahamika dada mkubwa wa Kenyatta, Christine Wambui Pratt (61), alinusurika.

Pratt alikuwa mmoja wa wateja waliokuwapo katika kituo hicho cha biashara wakati wa shambulio hilo.

Alionekana akikimbia akiwa amevaa kitopu cheupe, sketi ya khaki, akiwa pekupeku na mikononi ameshika viatu vyake vyeusi na begi huku akiongozwa na mlinzi.

Pratt alipokewa na marafiki na kusindikizwa katika gari aina ya Mercedes, iliyokuwa ikimsubiri kwenye Barabara ya Peponi. Hata hivyo hakuwa amejeruhiwa.

Jengo hilo la maduka ya Westgate, maarufu kwa Wakenya wa kipato cha juu na wataalamu wa kigeni lilikuwa limejaa wateja takribani 1,000 wakati magaidi hao walipolivamia mchana wa juzi.

Wanamgambo hao walirusha maguruneti na kuanza kumimina risasi kiholela lakini saa chache baada ya makabiliano ya risasi, duru za usalama zilisema polisi na jeshi walifaulu kuwazingira magaidi katika eneo moja na kufaulu kuwaokoa mamia ya wateja na wafanyakazi wa jumba hilo.

Mashirika ya usalama ndani na nje ya nchi kwa muda mrefu yalikuwa yakihofia kuwa kituo hicho siku moja kitalengwa na makundi yanayohusishwa na Al Qaeda kutokana na wingi na aina ya wateja wake wanaohusisha mataifa ya magharibi na Israel kama mwana hisa.

Shambulio hilo ni baya zaidi kutokea nchini hapa tangu Al-Qaeda walipoulipua ubalozi wa Marekani na kuua watu 200 mwaka 1998.

Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya, liliomba msaada wa damu na mamlaka ziliwahimiza wakazi wa karibu na eneo hilo kuwa waangalifu.

“Bado tunapambana na washambuliaji na majeshi yetu yamefanikiwa kuwadhibiti katika moja ya ghorofa,” alisema msemaji wa jeshi la Kenya, Kanali Cyrus Oguna. “Tuna matumaini kumaliza kadhia hii leo (jana),” alisema.

“Nilisikia kelele na milio ya bunduki eneo lote, niliogopa sana, nilijaribu kushuka ngazi na niliona mtu akikimbia kuja juu, niligeuka kurudi nilikotoka na kujificha nyuma ya moja ya magari,” Umar Ahmed mwenye umri wa miaka 18 alisema.

Saa chache baadaye, shambulio lilianza na kuwashtusha watu wa rika na rangi zote ambao waliweza kuonekana wakikimbia kutoka jumba hilo, huku wengine wakiwa wamewakumbatia watoto wao na wengine wakitambaa kutani kuepuka kudunguliwa risasi.

“Walizungumza lugha inayoonekana kama Kiarabu au Kisomali,” alisema mwanaume mmoja aliyenusurika ambaye alijitambulisha kwa jina moja tu la Jay.

“Niliona watu wakiuawa baada ya kuulizwa waseme kitu fulani,” Jay alisema.

Baadhi ya mashuhuda walisema wakati walipovamia, kabla ya kuanza mashambulizi yao, wanamgambo waliwaambia Waislamu waondoke na wasio Waislamu watalengwa na mashambulizi.

“Walikuja na kusema, “Iwapo wewe ni Muislamu, simama, tumekuja kuwaokoa,” Elijah Lamau alisema.

Alisema Waislamu waliondoka huku mikono yao ikiwa juu na kisha wanamgambo wakawapiga risasi watu wawili na kuwaua.

Watu hao wawili waliopigwa risasi na kufa inasemekana walishindwa kujibu swali kuhusiana na dini ya Kiislamu.

Naye, Charles Karani, 41, mhandisi wa Teknolojia ya Habari alikuwa na haya ya kusema: ‘Nilijificha ndani ya gari nikiwa na binti yangu. Niliwaona wanaume wapatao 40 wakiwa mstalini.

“Waliulizwa nani ni Muislamu, walioweza kuthibitisha kwa kutaja jina la mama wa Mtume waliachiwa, lakini wale waliokosea walipigwa risasi,” alisema.

Shuhuda mwingine, Fred Ngoga Gateretse, ambaye ni Ofisa wa Umoja wa Afrika (AU) alisema, “Naamini, watu hawa ni walengaji wazuri sana wa shabaha kwa sababu ukijionea jinsi wanavyoachia risasi, utajua wamefunzu mafunzo ya kijeshi,”alisema.

Baada ya uvamizi huo, polisi wa Kenya, wanajeshi na vikosi maalumu viliwasili na moja kwa moja kwenda katika maeneo mbalimbali ya kituo hicho wakipita duka moja baada ya jingine.

Maofisa usalama wa kigeni mbali ya Israel, pia walikuwapo Wamarekani na Uingereza ambao walionekana wakati wote wa tukio hilo.

Mwandishi mmoja wa Televisheni ya Shirika la Habari la Ufaransa (AFPTV), alisema aliona watu takribani 20 wakiokolewa kutoka duka la wanasesere, baadhi yao wakiwa watoto waliobebewa kwenye machela.

Kenneth Kerich, ambaye alikuwa akifanya ununuzi wakati shambulio likitokea, alieleza hali halisi ilivyokuwa ya kutisha na kushtusha mno.

“Ghafla nilisikia milio ya bunduki na niliona kila mtu akikimbia huku na kule na hivyo tulilala chini. Niliona watu wawili wakiwa sakafuni wakivuja damu, nadhani walipigwa risasi,” alisema.

“Wanamgambo walijaribu kulenga kichwa change, lakini walinikosa, niliona watu wapatao 50 wakipigwa risasi,” mmoja wa wafanyakazi katika kituo hicho, Sudjar Singh aliiambia AFP.

Miongoni mwa waliokufa ni mshairi maarufu wa Ghana na mwakilishi wa zamani wa Umoja wa Mataifa (UN), Kofi Awoonor (78), huku mwanae akijeruhiwa, kwa mujibu wa maofisa wa Ghana.

Hii si mara ya kwanza kwa maslahi ya Israeli nchini Kenya kushambuliwa.

Novemba 2002, kulikuwa na mashambulizi mawili mjini Mombasa, la kwanza likiwa la kombora lililolenga ndege ya kukodi ya Israeli wakati ikiruka kwenye uwanja wa ndege wa mji huo wa bandari, lakini liliikosa.

La pili lilihusisha gari lililokuwa limesheheni mabomu ambalo liliparamia Hoteli Paradise, hoteli pekee inayomilikiwa na Israel mjini Mombasa, huku watalii wa Israeli waliowasili mahali hapo muda mfupi, wakiwa eneo la mapokezi ya hoteli hiyo.

Wakenya 10 na Waisrael watatu walikufa katika shambulio hilo.

Mkuu wa Sera ya Kigeni ya Umoja wa Ulaya (EU), Catherine Ashton, alieleza kushtushwa na shambulio hilo la kinyama dhidi ya raia wasio na hatia mjini Nairobi.

Ufaransa imethibnitisha raia wake wawili ni miongoni mwa waliokufa katika kile ilichokiita shambulio la uoga.

Waziri Mkuu wa Canada, Stephen Harper, alisema raia wawili wa Canada, akiwamo mwanadiplomasia, walikuwa miongoni mwa waliokufa, huku Shirika la Habari la China (Xinhua) likisema mwanamke raia wa taifa hilo alikufa na mtoto wake kujeruhiwa.

Raia wawili wa India na mmoja wa Korea Kusini pia ni miongoni mwa waliofariki.

Marekani ilisema raia wake ni miongoni mwa walioripotiwa kujeruhiwa katika shambulio hilo.

Ikulu ya Marekani (White House) ililitaja tukio hilo kuwa la kikatili. Aidha Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, alisema nchi yake imetoa msaada kwa Serikali ya Kenya ili kusaidia kuikabili hali hiyo.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, William Hague, alisema wana uhakika raia wa Uingereza walikuwa wakishikiliwa mateka na hivyo wanapaswa kujiandaa kwa habari zozote mbaya.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki Moon, alikuwa akifuatilia shambulizi hilo kwa karibu huku akililaani vikali.


-Mtanzania.
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top