001fd04cf03a112146fb10
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
********
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Tanzania haiwezi kuendelea kuwa nchi ya kuomba na kupokea misaada na hisani kama kweli inataka kupiga hatua za haraka za maendeleo.
Aidha Rais Kikwete amesema kuwa Tanzania imeanzisha utaratibu za kuteua mabalozi wa heshima katika nchi mbali mbali duniani kama namna ya kujenga na kuendeleza kwa haraka zaidi maslahi ya Tanzania.
Rais Kikwete ameyasema hayo  Jumatatu, Septemba 16, 2013, wakati alipomsimika rasmi Mheshimiwa Ahmed Nassoro Issa Al Qasimi kuwa Balozi wa Heshima wa Tanzania katika Jimbo la California na akafungua rasmi ofisi ya Ubalozi wa Heshima huo katika mtaa wa Redwood Highway katika mji wa San Rafael, eneo la Francisco Bay, ulioko Marin, Jimbo la California.

Hafla hiyo ndiyo ilikuwa shughuli ya kwanza ya Rais Kikwete katika ziara ya siku mbili katika Jimbo la California ambayo ni sehemu ya ziara ya Marekani ambayo miongoni mwa mambo mengine itamwezesha kuhutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York baadaye mwezi huu. Rais Kikwete na ujumbe wake, wamewasili mjini San Francisco, California, mchana wa jana kuanza ziara hiyo baada ya safari ya zaidi ya saa 29 kutoka Tanzania.
Baadaye Rais Kikwete amehudhuria chakula cha usiku kilichoandaliwa na Balozi wa Heshima huyo kwenye Hoteli ya Embassy iliyoko katika eneo hilo la San Rafael na kilichohudhuriwa pia na mamia ya waalikwa wakiwemo Watanzania wanaoishi katika Jimbo la California na hata nje ya Jimbo hilo.
Akizungumza katika sherehe hiyo ya usimikaji wa Mheshimiwa Ahmed Issa na kufunguliwa kwa ofisi ya Ubalozi huo, Rais Kikwete amesema kuwa kamwe Tanzania haiwezi kuwa nchi inayoendelea kuishi kwa kutegemea hisani na misaada bali lazima iwe nchi inayoendelea kwa kutegemea uwekezaji na biashara na mataifa mengine.
“Hatuwezi kamwe kuendelea kuwa nchi inayoishi kwa kutegemea hisani na misaada. Tumeishi hivyo kwa muda mrefu wa kutosha. Lazima tubadilike sasa na kuanza kuishi kwa kutegemea uwekezaji mkubwa na biashara kati yetu na mataifa mengine duniani,”  Rais Kikwete amewaambia wageni waalikwa katika sherehe hiyo.
Rais Kikwete amesema mfano nzuri wa jambo hilo ni ziara mbili ambazo zimefanywa na wafanyabiashara wa Marekani katika Tanzania – Business Executive Tours- ambao miongoni mwa mambo mengine wametembelea mbuga za wanyama nchini na kujionea wenyewe Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar Es Salaam, ziara ambazo matunda yake yameanza kujitokeza.
Kuhusu uteuzi wa mabalozi wa heshima katika nchi mbali kuwakilisha maslahi ya Tanzania, Rais amesema kuwa sera ya sasa kuhusu jambo hili ni kuteuliwa kwa mabalozi wengi kwa kadri inavyowezekana kwa nia ya kuendeleza na kulinda maslahi ya Tanzania katika nchi mbali mbali na hasa nchi zile kubwa ambako balozi rasmi pekee hazitoshi kuendeleza maslahi ya nchi.
Kazi kubwa ya mabalozi wa heshima ni kulinda na kuendeleza maslahi ya Tanzania kwa kuendeleza jitihada za kuvutia uwekezaji na nafasi za kibiashara kati ya Tanzania na nchi ambazo wanakoishi. Ni wateule wanaofanya kazi kwa kujitolea bila kulipwa mishahara wala maslahi yoyote.
“Sera yetu sasa ni kuteua mabalozi wa heshima wengi katika sehemu mbali mbali kwa nia ya kulinda na kuendeleza maslahi ya nchi yetu hasa katika nchi kubwa kama Marekani ambako Ubalozi wetu ulioko mjini Washington, D.C hauna uwezo wa kufika kila mahali katika nchi hii katika kulinda maslahi ya Tanzania,” amesema Rais Kikwete.
Akizungumza kuhusu uteuzi wa Ahmed Issa, Rais Kikwete amesema, “Hakuna shaka kuwa tusingepata mwakilishi bora zaidi kuliko Balozi Ahmed Issa. Ni mtu anaijua vizuri Tanzania na ni mtu anaijua vizuri Marekani. Na sasa napenda kutangaza rasmi kuwa nakusimika rasmi kuwa Balozi wa Heshima wa Tanzania katika Jimbo la California.”
Balozi wa Heshima Ahmed Issa ni raia wa Marekani mwenye asili ya Afrika. Mheshimiwa Issa aliwasili Marekani mwaka 1988 akitokea Tanga. Ni mfanyabiashara ambaye anamiliki msururu wa malori ambayo yanafanya kazi ya usafirishaji.