HATIMAYE
Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi ameanza kuonyesha
makali, baada ya kukipa onyo kali Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kukitaka
kuacha mara moja kutumia viongozi wa kidiplomasia kwenye shughuli za
kisiasa.
Hatua ya Jaji Mutungi, imekuja siku
chache baada ya CCM kumtumia Balozi wa China, Dk. Lu Youping katika
shughuli za kisiasa mkoani Shinyanga wiki iliyopita.(hd)
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari
mjini Dar es Salaam jana, ilisema suala la ushiriki wa raia wa kigeni
ikijumuisha wanadiplomasia katika shughuli za kisiasa nchini,
halikubaliki.
Alisema ofisi yake, inaunga mkono kwa
dhati hatua iliyochukuliwa na Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, kukemea jambo hilo.
"Tamko la Serikali limezingatia sheria na
wajibu wa wanadiplomasia, wakati wa uwepo wao hapa nchini, mimi nikiwa
mlezi wa vyama vya siasa, ninakemea kitendo cha CCM kumshirikisha Balozi
wa China katika shughuli za kisiasa," alisema Jaji Mutungi.
Alisema katika tukio hilo, CCM kuruhusu
raia wa kigeni kutumia jukwaa lake ni dhahiri limezua hali ya taharuki
kwa wananchi, japo sheria ya vyama vya siasa kwa upande wake iko kimya
katika suala hilo.
"Naviasa vyama vya siasa kwa ujumla wake,
kuzingatia na kufuata sheria na taratibu stahiki katika utekelezaji wa
shughuli zao za kisiasa.
"Napenda kuujulisha umma kwamba, ofisi ya
Msajili wa Vyama vya Siasa kwa wakati huu ipo kwenye mchakato wa
marekebisho ya sheria husika ya vyama vya siasa, ambayo imebainika kuwa
na upungufu....lengo ni kukabiliana na changamoto zilizopo likiwemo
suala hili," alisema Msajili, Jaji Mutungi katika taarifa yake aliongeza sasa hivi ofisi yake inaendelea kukusanya maoni ya wadau katika jitihada za kufanikisha marekebisho ya sheria hiyo.
Suala la CCM kumshirikisha Balozi wa
China katika masuala ya kisiasa, lilizua mjadala mkubwa hali
iliyosababisha CHADEMA kutoa tamko na kuandika barua ya malalamiko UN
wakitaka aondolewe kwa kupoteza sifa za kuwa balozi, baada ya kuvunja
mkataba wa Umoja wa Mataifa wa 1961 unaosimamia nchi na nchi.
CHADEMA waliandika barua nyingine kwenda
Serikali ya China na Tanzania, wakitaka msimamo na hatua
zitakazochukuliwa dhidi ya balozi huyo kuvunja mkataba huo ibara ya
41(1-3), kinachokataza balozi kujihusisha na siasa katika Taifa ambalo
yuko.
Chadema imesema inalaani kitendo hicho na
itachukua hatua kwenda Umoja wa Mataifa na pia kupata maelezo toka
Serikali ya China kama imemtuma balozi huyo kujihusisha na mambo ya
siasa za ndani za vyama au kuiwakilisha nchi.
Akijibu tuhuma hizo, Katibu wa Itikadi na
Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema alichofanya balozi huyo ni kitendo
cha kuungwa mkono, maana alikuwepo kwa nia ya kuangalia maeneo ya
uwekezaji wa zao la Pamba katika Mkoa wa Shinyanga.
Alisema uwekezaji kutoka China, utasaidia
kuondoa tatizo sugu la ajira, kupanda kwa bei ya zao la pamba ambacho
kimekuwa kilio kikubwa cha wakulima pamoja na ujengwaji wa viwanda vya
nguo na kuchuja mafuta.
Hivyo ni vema kumpongeza balozi huyo na
kuunga juhudi za CCM za kuwatafuta wawekezaji wa nje, badala ya
kusingizia uvunjaji wa Mkataba wa Vienna ili kupata umaarufu wa
kisiasa:chanzo mtanzania
Post a Comment