Wakati vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi vikiendelea na shinikizo la kutaka Rais Jakaya Kikwete asitie saini Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe amemwomba mkuu huyo wa nchi auridhie ili kuepusha vurugu ambazo zinaweza kujitokeza katika kikao kijacho cha Bunge.
Ameonya kuwa muswada huo ukirudi bungeni unaweza kusababisha vurugu kubwa zaidi ya zile za mara ya kwanza kutokana na tofauti kati ya wabunge wa CCM na wale wa vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Chikawe alisema kelele zinazopigwa na wapinzani hivi sasa hazisaidii kwa kuwa muswada huo ulipitishwa baada ya taratibu zote kukamilika.
Alisema kuwa kutokana na hali hiyo, atamshangaa Rais Kikwete ikiwa atasikiliza kelele za wapinzani kwa sababu walishirikishwa kupitia kamati na hata bungeni kabla ya kupitishwa kwake.
“Nitamshangaa sana Rais Kikwete kama atashindwa kusaini muswada huo kwa sababu ya kelele za wapinzani. Tuliwashirikisha katika kila mchakato kabla na baada ya kuuwasilisha bungeni,” alisema Chikawe.
Alisema kitendo cha wapinzani hao kujiunga pamoja na kuanzisha kampeni za kuwahamasisha wananchi ili waukatae muswada hakisaidii lolote, kwa sababu sheria zote zinatungwa bungeni na siyo kwenye Viwanja vya Jangwani wala Ikulu.
Vyama vyampinga JK
Wakati Chikawe akisema hayo, viongozi wa Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi wameshikilia msimamo wao kwamba wataendelea kupinga muswada huo uliopitishwa na Bunge, Septemba 6, mwaka huu.
Wakizungumza Dar es Salaam jana walipokutana na Shura ya Maimamu ikiwa ni mwendelezo wao wa kukutana na asasi za kiraia, viongozi wakuu wa vyama hivyo, walisema kamwe kasi yao ya kutaka kutosainiwa kwa Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba haiwezi kupunguzwa kwa namna yoyote kwa kuwa wanatetea masilahi ya Watanzania na siyo mtu binafsi.
Kauli yao imekuja siku moja baada ya Rais Kikwete kusema kuwa baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakisema uongo kuhusu mchakato wa Katiba unavyokwenda.
Wanasiasa pia hao wamepinga matumizi ya kauli za kibabe kwenye mchakato huo na kuonya kuwa nguvu ya dola haiwezi kushindana na nguvu ya umma.
Mbali na hayo, wanasiasa hao walisisitiza kwamba hawatapiga magoti kuomba Katiba Mpya, kwani ni ya Watanzania wote na si mali ya wanasiasa, chama cha siasa wala wabunge.
Post a Comment