Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya
Mwananchi Communications Limited (MCL), Tido Mhando (katikati),
akifurahia jambo na Meneja Uendelezaji Biashara, Theophil Makunga na
Mwanasheria MCL, Doris Marealle nje ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
Dar es Salaam jana, kabla ya kuanza kwa kesi ya uchochezi inayomkabili
Makunga na wenzake wawili. Picha na Venance Nestory
****
Mshtakiwa wa kwanza katika kesi ya
makala inayodaiwa kuwa ya uchochezi, Samson Mwigamba (38), amekana
kuandika makala ya uchochezi alipokuwa akijitetea katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi wa Kisutu Dar es Salaam.Mshtakiwa wa pili, Absalom Kibanda,
ambaye alikuwa Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Free Media inayomiliki
gazeti la Tanzania Daima, naye alisema makala hiyo ilikuwa sahihi ndiyo
maana Serikali kupitia Idara ya Habari (Maelezo) haikutoa onyo kwao.
Mshtakiwa wa tatu, Meneja Uendelezaji
Biashara wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL), Theophil
Makunga, ambaye aliunganishwa kwenye kesi hiyo kutokana na gazeti hilo
lilichapishwa Kiwanda cha Uchapaji cha Kampuni ya MCL, wakati alipokuwa
akikaimu nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, atajitetea Septemba 23,
mwaka huu.
Akitoa utetezi huo jana katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mwigamba alidai makala hiyo ililenga kutoa
maoni kwa kuwaelimisha askari wote nchini, ili wasivunje haki ya katiba
kwa raia.
Akiongozwa na wakili wake, Nyaronyo
Kicheere, Mwigamba alidai waraka alioandika ulilenga kutoa maoni kwa
askari wasivunje haki ya katiba kwa raia katika mambo mawili; haki ya
kuishi na haki ya kuandamana.
Naye Kibanda alidai makala hiyo
haikuwa habari ya kawaida, bali ni maoni ya mwandishi, kama ambavyo
msomaji yeyote anaweza kutoa gazetini.
Kibanda alidai makala hiyo ingekuwa na
tatizo msajili wa magazeti nchini, angefungia gazeti au angeandika
barua ya wito wa onyo. "Makala hiyo inaangukia katika kundi la maoni na
haya ni maoni ya mwandishi," alidai Kibanda na kuongeza:
"Makala hiyo ilikuwa ni mahususi kwa ajili ya kupasha na kuelimisha jamii, lakini ni maoni siyo habari." alidai.
Post a Comment