JAMHURI YA MUUNGANO
WA TANZANIA
WIZARA
YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
TAARIFA KWA
VYOMBO VYA HABARI
OPERESHENI
KIMBUNGA AWAMU YA KWANZA YAFIKIA KILELE KWA MAFANIKIO
Operesheni Kimbunga iliyoanza Septemba 6,2013
imemaliza utekelezaji wa Awamu yake ya Kwanza Septemba 20,2013 kwa kutimiza
malengo yake kwa mafanikio makubwa.
Hadi kufikia mwisho wa Awamu ya Kwanza wa Operesheni
hii, Timu ya Operesheni imefanikiwa kukamata wahalifu wa unyang’anyi wa kutumia
silaha pamoja na washirika wao na kuhakiki uraia wa watuhumiwa wa Uhamiaji
haramu kwa kutumia maofisa wa Idara ya Uhamiaji kwa kuzingatia Sheria za
Uhamiaji. Aidha, suala la Haki za Binaadam limezingatiwa katika Operesheni hii.
Jumla ya Wahamiaji haramu 12,704 wamekamatwa, kati yao
Wanyarwanda 3,448 Warundi 6,125, Waganda 2,496, Wakongo 589 Wasomali 44, Yemen
1 na India 1.
Jumla ya Wahamiaji Haramu 194 walirudishwa na
kupokelewa nchini baada ya kukataliwa na nchi zao. Watu hao wanasubiri hatua za kisheria kuchukuliwa kwa kuwa hawana
sifa ya kuwa Raia wa Tanzania na pia wamekosa sifa ya kuwa raia wa nchi jirani
ambapo Serikali iliwapeleka baada ya vigezo vya kuthibitisha kuwa ni raia wa
nchi hizo kukamilika.
Wakati Operesheni kimbunga inafanyika katika Awamu
yake ya Kwanza kuanzia Septemba 6, 2013, jumla ya wahamiaji haramu 2,129
walikubali kuondoka nchini kwa hiari yao na Wahamiaji Haramu 8,696 waliondoshwa nchini kwa amri ya
Mahakama baada ya kupewa hati ya kufukuzwa nchini. Watuhumiwa wa Uhamiaji
Haramu 1,852 waliachiwa huru baada ya Serikali kuthibitisha uraia wao wakati
wengine 2,286 wanaendelea na mahojiano ili kuthibitisha uraia wao.
Operesheni Kimbunga pamoja na kushughulikia wahamiaji
Haramu ilifanikiwa kukamata jumla ya Watuhumiwa 212 wa unyang’anyi wa kutumia silaha
na Majangili wa Tanzania 23. Mabomu 10 ya kutupwa kwa mkono, bunduki/silaha 61
zikiwemo bunduki aina ya SMG 5, Shot Gun 8, Mark IV 1, Riffle 1, Pistol 1, Pisto
za kienyeji 3 na Magobole 42 pamoja na mitambo Miwili 2 ya kutengeneza silaha
aina ya Magobole.
Risasi 665 zilikamatwa zikiwemo za bunduki aina ya SMG
na SAR risasi 561, Shot Gun risasi 22, Gobole risasi 82 na Fataki 8, Suruali
Sare za Jeshi na Kibuyu cha Maji vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania.
Jumla ya Ng’ombe 8,226 walikamatwa wakiwa wanachungwa
katika maeneo ya Tanzania hususan katika hifadhi za misitu. Pia kiasi cha Tsh. 32,510,000/=
zimepatikana ikiwa ni tozo za faini ya ng’ombe walioachwa kwenye hifadhi ya
Taifa.
Ngozi za wanyama aina ya Duma(1), Swala (2), Nyati (1)
na vipande 10 vya Nyama vinavyodhaniwa kuwa Nyara za Serikal, Vipande viwili
vya meno ya Tembo pamoja na Mbao 2,105, Magogo 86, Mkaa Magunia 467,Gongo Lita
375, Mtambo wa Gongo mmoja (1), Bangi Kilo 77 na Makokoro yanayotumika kuvuna
Samaki kinyume cha sheria vilikamatwa
katika kipindi cha Wiki Mbili za Awamu ya Kwanza ya Operesheni Kimbunga.
Takwimu zinaonyesa kuwa Mkoa wa Kagera unaongoza kwa
kukamata wahamiaji haramu 7,001 ukifuatiwa na Mkoa wa Kigoma ambaPo wahamiaji
haramu 5,005 walikamatwa wakati mkoa wa Geita wamekatwa Wahamiaji Haramu 698.
Changamoto
Pamoja na mafanikio yaliyopatikana kumekuwepo na
changamoto zilizojitokeza ikiwa ni pamoja na hali ya maisha mchanganyiko ya
Watanzania asilimia 60% na Wahamiaji asilimia 40% katika mikoa ya mpakani hii
ni kwa mujibu wa tafiti mbali mbali za masuala ya kiuhamiaji zilizowahi
kufanyika katika mikoa hiyo.
Changamoto nyingine ni baadhi ya wananchi wenye nia
mbaya au kulipizana visasi walitaka kutumia zoezi hili kuweza kukomoana kwa
kuwataja baadhi ya watu kuwa ni wahalifu kumbe ni uongo na baadhi ya wahamiaji
baada ya kukamatwa walikosa sifa za uraia wa Tanzania na hata waliporudishwa
kwenye nchi wanazodhaniwa kutoka walikosa sifa za uraia na kuleta mgongano
kuhusiana na uraia wao yaani kwa kiingereza (Stateless citizenship) .
Changamoto nyingine zilizojitokeza ni pamoja na
ukosefu wa Vitambulisho vya Uraia (Utaifa) ambako kulileta tatizo katika
kuwatambua Wahamiaji Haramu na kutokuwepo kwa uzio wa kuzuia mipaka ya nchi
yetu hivyo Wahamiaji Haramu wanapopelekwa kwao wanarudi kupitia vipenyo visivyo
halali yaani njia za panya.
Sheria ya Maliasili na Utalii (The Forest Act &
Wild Life Conservation Act) kutoendana na hali halisi ya uhalifu wa uhujumu wa
Maliasilia, mfano kifungu cha 81 (2) kinatoa adhabu ya faini kuanzia shilingi Elfu
Thelathini (30,000/=) hadi Milioni Moja na uzoefu unaonyesha kwamba wanaotenda
makosa hayo hupigwa faini chini ya Shilingi Laki Tano (500,000/=) bila kujali
thamani ya mali aliyokamatwa nayo, isipokuwa maamuzi hutegemea utashi wa
Mahakama.
Matarajio
Baada ya kukamilisha Awamu ya Kwanza ya Operesheni Kimbunga
tunatarajia Serikali kushughulikia changamoto zilizojitokeza ili kupunguza
baadhi ya matatizo katika mikoa ya Kagera, Kigoma na Geita hususan yanayohusia
na uhalifu na masuala ya kiuhamiaji.
Tunatarajia kuanzisha kikosi kazi kila mkoa kwa ajili
ya kufanya ufuatiliaji wa wahalifu sugu wanaotumia silaha za kivita na wale
wanaowafadhili.
Aidha, uhamasishaji utafanyika kuanzia ngazi ya
familia, Kitongoji, Mtaa/Kijiji, Kata/Shehia, Tarafa, Wilaya Mkoa na Taifa
kuhamsisha jamii kuimarisha misingi ya ulinzi na usalama kupitia kwenye kamati
zilizopo na kutoa taarifa mara moja pindi panapojitokeza jambo lolote
linalohusu ulinzi na usalama katika maeneo yao.
Aidha, tunatarajia kujipanga kimkakati ili kuona namna
ya kushughulikia baadhi ya Wahamiaji Haramu waliokosa sifa za uraia na
kurudishwa nchini mwao ambao bado wanang’ang’ania kwa kusema wao ni Watanzania
(stateless citizenship).
Washiriki
Operesheni Kimbunga ilishirikisha Vyombo Vya Ulinzi na
Usalama wakiwemo Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Polisi, Usalama wa
Taifa, Uhamiaji, Magereza, TAKUKURU, Taasisi nyingine za Serikali zikiwemo
Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Idara za Mifugo, Ardhi, Kilimo, Uvuvi, Misitu, Afya na Idara
ya Wanyama Pori.
Hitimisho
Opereshi Kimbunga ilifanyika kwa kufuata Sheria,
Kanuni na Taratibu za nchi. Aidha, suala la Haki za Binaadam lilizingatiwa na
hadi sasa hakuna malalamiko yeyote yaliyopokelewa.
Hata hivyo,
juhudi na nguvu zaidi zitaelekezwa katika kukamata Majambazi, Silaha Haramu,
Majangili na Wahamiaji Haramu.
Mafanikio yaliyofikiwa yametokana na ushirikiano wa
Maofisa Wakuu Waandamizi, Maofisa wa Kati, Wakaguzi na Askari wote wa vyeo
mbali mbali walioshiriki kwenye utekelezaji wa operesheni hii. Kila mtendaji
alitimiza wajibu na majukumu yake na ndiyo maana malengo ya utekelezaji wa
operesheni hii yamefikwa kwa kiasi kikubwa. Hata hivyo huu ni mwisho wa Awamu
ya Kwanza ya operesheni na mwanzo wa Awamu ya Pili ya Operesheni Kimbunga kwa
maana nyingine Operesheni inaendelea mpaka hapo hali ya usalama ya mikoa hii
Mitatu itakapokuwa shwari.
Taarifa hii imetolewa na:
Naibu Kamishna
wa Polisi Simon Sirro kwa niaba ya Kamanda wa Operesheni Kimbunga Mwanza, Septemba22,2013
Post a Comment