Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

SAMWEL SITTA AZUNGUMZIA HARAKATI ZA URAIS 2015

   


*Asema ni hatari tajiri kuingia Ikulu
KWA mara nyingine tena, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, ameibuka na kusema watu wanaotajwa kuwania urais mwaka 2015, wasifikiri ni mashindano.

Sitta ambaye ni mmoja wa wanasiasa wanaoheshimika nchini, kwa nyakati tofauti amewahi kutangaza wazi kuwa atawania urais mwaka 2015, alisema kumekuwa na mambo mengi ya kushangaza dhidi ya watu wanaotaka nafasi hiyo nyeti.

Akizungumza katika kipindi cha Medani za Siasa, kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha Star Tv cha jijini Mwanza jana, Sitta alisema wanasiasa wengi wanadhani urais ni kama mashindano ya mbio za kukimbia kwa miguu.

“Nasema urais si mashindano kama watu wengi wanavyofikiria, hii ni taasisi nyeti ambayo inahitaji watu makini na wenye uwezo, si kila mmoja anaweza kushika nafasi hiyo.

“Miaka ya nyuma, hatukuwa na utamaduni wa aina hii, sijui taifa letu linataka kuelekea wapi, watu wanageuza urais kama mtaji, hawa hawawezi kuwasaidia Watanzania pindi watakapopewa nafasi ya kuongoza nchi yetu,” alisema Sitta.

Alisema anashangazwa zaidi na wengi wao ambao wanajivunia utajiri mkubwa walionao, jambo ambalo halina tija katika maslahi ya wananchi na walalahoi.

“Nawashangaa mno watu wanaotaka urais huku wakishabikia utajiri wao, wameutoa wapi ndugu zangu, lazima tuwe nao macho tusipoangalia tutajikuta tunawapatia uongozi matajiri ambao kazi zao mnazifahamu,” alisema Sitta.



Alisema ni jambo la hatari nchi kupata rais anayebeba wafanyabiashara, kwani atalazimika kuwalipa fadhila wafanyabiashara hao ili kukidhi matakwa yao.

“Ni jambo la hatari kupata rais wa nchi mwenye uchu wa kubeba matajiri, unafikiri huyo ni kiongozi kweli? Lazima turudi kwenye misingi ya utawala ambao una malengo ya kuondoa umasikini unaowakabili Watanzania walio wengi,” alisema Sitta kwa kujiamini.

Bila kutaja majina ya watu wenye nia ya kugombea urais, Sitta alisema miaka ya nyuma, wanasiasa walikuwa wakiulizwa utajiri walionao, lakini utamaduni huo umeondoka ghafla, jambo ambalo limetoa mwanya kwa wenye fedha kushika nafasi nyingi za uongozi.

Alisema enzi za utawala wa awamu ya kwanza, chini ya Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, mwanasiasa alipokuwa akiulizwa kama ana nyumba, alikuwa akijibu ana kibanda.

“Enzi za utawala wa Mwalimu Nyerere, ulikuwa ukiulizwa kama una nyumba, lazima ujibu una kibanda, maana ukisema una nyumba utaulizwa umeipataje.

“Ulikuwa ukiulizwa kama una gari, unajibu nina mkweche (gari chovuchovu), lakini sasa hivi watu wanashabikia utajiri, hili ni jambo hatari kwa nchi, lazima turudi kwenye mstari, mimi ni muumini mzuri wa siasa za Mwalimu Nyerere,” alisema Sitta.

Akizungumzia muundo wa Serikali uliopendekezwa kwenye Rasimu ya Katiba Mpya, Waziri Sitta alionyesha kutofautiana nao kutokana na dosari zilizopo.

“Nimepitia mapendekezo ya Rasimu ya Katiba Mpya na namna ilivyopendekeza muundo wa Serikali tatu, mimi binafsi sikubaliani nao kwa sababu sisi ni nchi changa, tutatoa wapi fedha za kugharamia Serikali tatu?

“Kumbuka Serikali tatu ni mzigo ambao unajumuisha viongozi wengi, tutalazimika kutumia fedha za walipa kodi wa nchi hii jamani, sijawahi kuona duniani nchi masikini kama hii ikawa na Serikali tatu,” alisema.

Kuhusu Katiba Mpya, alisema inapaswa kutanguliza maslahi ya taifa zaidi kuliko kuvutia watu wachache na kuacha kundi kubwa likibanwa.

MTANZANIA
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top