Msemaji wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari- (MAELEZO) Assah Mwambene akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu mtandao wa kijamii wa nchini Kenya ulioituhumu Serikali ya Tanzania.
--------------
Na Fatma
Salum-MAELEZO
SERIKALI ya Tanzania imetoa
ufafanuzi kuhusu tuhuma mbalimbali dhidi yake zilizotolewa na mtandao wa kijamii
wa nchini Kenya ujulikanao kama www.standardmedia.co.ke unaosadikika kuendeshwa na kampuni ya
gazeti la The Standard la nchini humo.
Akizungumza na waandishi wa habari
leo jijini Dar es Salaam, Msemaji wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari-
(MAELEZO) Assah Mwambene , alisema mtandao huo umeripoti kuwa Serikali ya
Tanzania imekataa kuiuzia Kenya gesi asili ya Songosongo jambo ambalo halina
ukweli kwa kuwa gesi inayozalishwa hivi sasa bado haijafikia kiasi cha kuweza
kuuzwa nje ya nchi.
Mtandao huo pia umeripoti kuwa
Serikali ya Tanzania ilikataa viwanja vyake vya ndege vya kimataifa kutumiwa na
ndege zilizopaswa kutua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyata
wakati wa ajali ya moto iliyotokea kwenye uwanja huo hivi
karibuni.
Mwambene alifafanua kuwa tuhuma hizo
ni za uongo kwani mara baada ya uwanja wa ndege wa Jomo Kenyata kuwaka moto,
ndege zilizotakiwa kutua uwanjani hapo ziliruhusiwa kutua kwenye viwanja vya
ndege vya Tanzania vya Julius Nyerere International Airport (JNIA) na
Kilimanjaro International Airport (KIA).
“Sio kweli hata kidogo kwamba
Tanzania ilikataa ndege za Kenya zisitue kwenye viwanja vyake kwa sababu uwanja
wa Jomo Kenyata ulipoungua ndege nyingi zilizopaswa kutua katika uwanja ule
zilitua kwenye viwanja vyetu na hii pia ilitokana na ukweli kwamba Tanzania na
Kenya zinachangia ndege nyingi za nje ya nchi.” Alisema
Mwambene.
Aidha Mwambene alikanusha tuhuma
nyingine iliyodai kuwa mwaka 2010 Tanzania ilikataa kuiuzia Kenya chakula badala
yake ikaiuzia nchi ya Uganda taarifa ambazo si za kweli kwa kuwa mwaka huo nchi
nyingi za Afrika zilikumbwa na baa la njaa ikiwemo Tanzania
yenyewe.
Hivyo Tanzania ililazimika
kusitisha utoaji wa vibali kwa wafanyabiashara kuuza chakula nje ya nchi na
hakukuwa na taarifa yoyote ya kuuzwa chakula nchini
Uganda.
Kutokana na upotoshaji huo Mwambene
alisema Serikali ya Tanzania imeutaka mtandao huo kuomba radhi na isipofanya
hivyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Katika hatua nyingine Mwambene
alifafanua kuwa zoezi linaloendelea nchini la kuwataka wahamiaji haramu
wanaoishi hapa kinyume cha utaratibu kuondoka kwa hiari haliwahusu wakimbizi
waliopo nchini kisheria.
Pia zoezi hilo linawalenga wahamiaji
haramu wote kutoka nchi za Rwanda, Burundi, Congo DRC, Zambia na Uganda na
hakuna serikali ya nchi yoyote kati ya hizo iliyolalamika kuhusu hatua
hiyo.
“Mpaka sasa zoezi linaenda vizuri
hakuna taarifa yoyote ya malalamiko kutoka Zambia, DRC, Burundi, Rwanda wala
Uganda na tayari Rwanda imetuma taarifa rasmi kuishukuru serikali ya Tanzania
kwa kuendesha vema zoezi hilo.
Kinachoandikwa na baadhi ya vyombo
vya habari ni upotoshaji unaolenga maslahi binafsi.”
Akizungumzia usalama wa Watanzania
nchini Rwanda, Mwambene alisema hakuna taarifa ya Mtanzania yeyote kunyanyaswa
nchini humo na uhusiano wa kidiplomasia kati ya Rwanda na Tanzania
haujakatika.
Post a Comment