Na Joachim Mushi
CHAMA cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA)
kimetaja mambo ya msingi ya kuzingatiwa katika mchakato wa Katiba Mpya
ili ujio wa katiba hiyo uweze kutokomeza mila kandamizi na vitendo vya
kikatili kwa wanawake.
Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam na mshauri wa masuala ya
jinsia na mwanaharakati wa haki za binadamu, Gemma Akilimali alipokuwa
akitoa mada katika kikao cha wahariri kutoka vyombo anuai vya habari
nchini kilichofanyika makao makuu ya TAMWA Sinza.
Akizungumza, alisema vyombo vya habari havina budi kusimama kidete na kuhakikisha fursa ya ujio wa katiba mpya inayoandaliwa hivi sasa inaweza kuondoa vikwazo na mazingira ambayo yalikuwa kandamizi kwa wanawake.
Akizungumza, alisema vyombo vya habari havina budi kusimama kidete na kuhakikisha fursa ya ujio wa katiba mpya inayoandaliwa hivi sasa inaweza kuondoa vikwazo na mazingira ambayo yalikuwa kandamizi kwa wanawake.
“Tunataka katiba Mpya ibatilishe sheria ambazo bado ni kandamizi;
iendelee kubatilisha sheria zote za ubaguzi wa jinsia, ikiwa ni pamoja
na kukataza mwendelezo wa tabia, taratibu na mila zenye kubagua na
kudhalilisha wanawake na watoto wa kike chini ya mfumo dume unaotawala
jamii zetu,” alisema Bi. Akilimali.
Akifafanua zaidi, alisema katiba haina budi kutamka wazi kuwa elimu
itolewe bila kikomo kwa jamii hiyo huku akishauri pia ibainishe kuwa
nafasi za uongozi ziwe na haki sawa ili kuleta usawa katika makundi yote
hasa wanawake.
Aidha alisema katiba mpya iwajibishe serikali kutekeleza mikataba
yote ya kimataifa iliyoridhia kuhusu haki za wanawake ikiwa ni pamoja na
kuendeleza misingi inayolinda utu wa mwanamke na uwepo wa mahakama ya
kifamilia.
Mambo mengine ambayo mwanaharakati huyo alitaka yawekwe wazi katika
katiba hiyo, ni pamoja na haki ya kunufaika na kumiliki rasilimali za
nchi, haki za uzazi salama, haki za huduma za msingi, haki za wanawake
walemavu, haki za mtoto wa kike na iwepo tume maalumu itakayo hakikisha
uzingatiaji wa haki za wanawake katika nyanja mbalimbali.
Alisema madai yote hayo yamekuwa vikwazo kwa fursha nyingi kwa
wanawake, hivyo vyombo vya habari vinaweza kuendeleza mjadala huo wa
madai ili kumsaidia mtoto wa kike ambaye amekuwa akiminywa na mfumo
uliopo kwa muda mrefu.
Short URL: http://www.thehabari.com/?p=38306
Post a Comment