Msururu
wa malori zaidi ya 80 ukiwa unasubiri kupima uzito kwenye mizani ya
Mikese, Mkoani Morogoro,leo Jumapili, Oktoba 13, 2013. (Picha na Irene
Bwire).
ZIKIWA
zimepita siku tatu tangu Waziri Mkuu Mizengo Pinda aagize malori
yarejee kutumia utaratibu wa zamani wa kupima mizigo kwenye mizani, hali
bado ni tete kutokana na misururu mikubwa iliyokuwepo leo asubuhi
kwenye mizani ya Mikese na Kibaha.
Mwandishi
wa habari hizi alishuhudia msururu wa malori na mabasi zaidi ya 105
kwenye mizani ya Mikese mkoani Morogoro bila kujali idadi ya magari
madogo yaliyokuwepo kwenye foleni ya kutoka Dar es Salaam kuelekea
Morogoro.
Mashuhuda
waliokuwepo kwenye mizani ya Mikese walisema kuwa mizani inayopima
magari ya kutoka Morogoro imeharibika tangu jana ndiyo maana inatumika
mizani ya upande mmoja tu (wa kutoka Dar es Salaam). Kulikuwa na dalili
za mafundi kufanya matengenezo kwenye maegesho ya mzani huo ambapo
malori na mabasi huwa yanasimama.
Katika
mizani ya Kibaha mkoani Pwani hali nako haikuwa shwari sana licha ya
kuwa mizani ya pande zote mbili ilikuwa ikifanya kazi. Magari ya kutoka
Dar es Salaam peke yake yalikuwa zaidi ya 90 bila kuhesabu magari madogo
yaliyokuwa kwenye foleni hiyo ya kuelekea Morogoro.
Jumatano
wiki hii (Oktoba 10, 2013), Waziri Mkuu alitengua uamuzi wa awali wa
Serikali uliotolewa Oktoba Mosi, 2013 na Waziri wa Ujenzi ambao ulikuwa
ukiondoa msamaha wa tozo kwa uzito wa magari uliozidi ndani ya asilimia
tano ya uzito unaokubalika kisheria.
Vilevile,
Waziri Mkuu aliamua kuunda kamati maalum kamati ambayo aliipa muda wa
mwezi mmoja na kuitaka ikutane na wadau ambao ni Chama cha Wamiliki wa
Malori nchini (TATOA) na Chama wa Wamiliki wa Mabasi yaendayo Mikoani
(TABOA) ili kupata ufumbuzi wa mgogoro uliojitokeza.
“Natoa
kipindi cha mwezi mmoja kwa wizara husika na wadau hao kukamilisha kazi
hiyo. Katika kipindi hicho cha mpito, utaratibu ulikuwepo awali kabla
ya tangazo la tarehe 01 Oktoba 2013 lililotolewa na Wizara ya Ujenzi,
utaendelea kutumika,” alisema.
"Kwa
kuwa bado kuna mgogoro kati ya Wizara ya Ujenzi, Wasafirishaji wa
malori na mabasi kuhusu utekelezwaji wa kanuni 7(3), ambao wanasema
haitekelezeki kirahisi, naiagiza Wizara ikutane na wadau. Wakae na
kujadili namna bora ya kutekeleza kanuni hii, Wizara ya Ujenzi, Wizara
ya Uchukuzi, Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, waunde timu ya wataalamu ambao watakutana na wawakilishi
wachache wa TATOA na TABOA ili wapitie kanuni hizi kwa lengo la kupata
mwafaka," alisema Waziri Mkuu.
mtaa kwa mtaa
Post a Comment