Mwandishi wa habari wa
ITV, aliyejeruhiwa kwa risasi jana asubuhi, alilazimika kuvumilia
majeraha ili kujiokoa yeye mwenyewe na wadogo zake watatu waliokuwa
wakipigwa risasi, baada ya mama yake mzazi, Anastazia Saro (58), kuuawa.
Mauaji hayo ya
kusikitisha, yalifanyika katika eneo la Mbezi Kibwerere, nyumbani kwa
mama yake Ufoo ambako alikuwa akiishi na wadogo zake Ufoo ambao ni
Goodluck, Innocent na Jonas.
Matuhumiwa wa unyama huo
ametajwa kuwa ni Anthery Mushi, ambaye ni baba mtoto wa Ufoo, na siku ya
tukio wawili hao walitokea Mbezi Magari Saba nyumbani kwa Ufoo, kwenda
kuzungumza kifamilia na mama mzazi wa mwandishi huyo.
Mushi (40) ni Mhandisi wa
kitengo cha Mawasiliano katika Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) nchini
Sudan na aliwasili nchini juzi na kwenda moja kwa moja nyumbani kwa Ufoo
Mbezi Mgari Saba.
Kwa mujibu wa Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura, Ufoo amejeruhiwa katika
paja na tumboni, mama yake mzazi alikufa papo hapo baada ya kupigwa
risasi ya kifuani na mtuhumiwa Mushi ambaye naye alijiua baada ya
kujipiga risasi kichwani katika eneo la kidevuni.
Walivyowasili nyumbani
Akizungumza na wavuti hii
jana mdogo wake Ufoo, Goodluck alisema; "Walikuja wakiwa pamoja (Ufoo
na Mushi) mapema alfajiri wakiwa ndani ya gari saa 12 kabla ya kuingia
ndani walitusalimia kisha wakaingia sebuleni na kuanza mazungumzo na
mama."
Goodluck alidai baada ya
muda, walisikia milio ya risasi iliyokuwa ikiambatana na sauti ya mama
yao akisema "jamani nakufaa," na walipotaka kufungua mlango ili kujua
kulikoni, mlio wa risasi uliendelea kusikika kutoka sebuleni. "Pengine
muda huo Ufoo ndiyo alikuwa akifyatuliwa risasi," alisimulia.
"Tulipotoka kujua
kulikoni, tulimuona dada (Ufoo) akijiburiza chini kuja katika mlango wa
chumba tulichokuwa tumelala... akatuambia jifungieni atatuua wote huyu."
"Tulifunga mlango lakini
zilipigwa risasi mbili mlangoni huku Mushi akisema tokeni nje
niwamalize. Tulitafuta namna ya kujiokoa na kuamua kupanda juu ya dari
la nyumba," alisimulia Goodluck.
Kwa mujibu wa madai ya
Goodluck, walipanda darini ili kujiokoa kwa kuwa Mushi alifungua ntungi
wa gesi na kusababisha hewa kuwa nzito na nahisi alilenga kulipua nyumba
ili kuteketeza wote.
"Tulipoanza kupanda juu,
alianza kufyatua risasi kupitia dirishani lakini wakati huu alikuwa nje
ya nyumba, tunamshukuru Mungu kwani muda huo wote tayari tulikuwa juu
kwenye dari tukijaribu kutoka nje ya nyumba na tulipofanikiwa
kutoka,tulikmbilia kwa majirani kutoa taarifa," alisema Goodluck.
Hata hivyo alisema majirani walikuja lakini hakuna hata mmoja aliyejaribu kusogelea nyumba hiyo.
Ufoo yuko wapi?
Goodluck alisema
wakiongozana na askari polisi, waliimgia ndani na kumkuta muuaji akiwa
amekaa katika moja ya sofa akiwa tayari amekwisha kufa huku mwili wa
mama yao ukiwa sakafuni.
Alisema walijaribu
kuangalia ndani kumtafuta dada yao bila mafanikio, ndipo walipotoka nje
na na kukutana na mmoja waendesha pikipiki aliyewaeleza kuwa walimuona
dada mmoja akiwa ametapakaa damu akiomba kupelekwa Hospitali ya Tumbi.
Alijiandaa
"Polisi waliingia ndani
na kuchukua bastola iliyotumika kwa mauaji pamoja na kuokota maganda ya
risasi na wapopekua mfuko aliokuja nao Mushi, ndani yake walikuta kuna
pingu,shoka lenye mpini mfupi pamoja na kamba. Hata hivyo hatukujua
alivibeba vitu hivyo kwa sababu gani,"alisema Goodluck.
Alisema baadaye Polisi waliichukua miili ya marehemu wote wawili na kuondoka nayo kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Muhimbili
Ufoo alihamishiwa
katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jana akitokea Tumbi Kibaha, na
alifanyiwa upasuaji na juhudi nyingine zilikuwa zikiendelea kuokoa
maisha yake.
Hapo jana Mwenyekiti
Mtendaji wa IPP , Reginald Mengi aliruhusiwa kumuona Ufoo ambapo alisema
anazungumza na hali yake ilikuwa ikiimarika.
Taarifa zilizopatika leo
hii kutoka Muhimbili zinaeleza kuwa Ufoo anaendelea vizuri baada ya
jitihada za kuondoa risasi mwilini mwake kufanikiwa na hali yake leo
inaendelea vyema.
Aidha askari polisi
wamegawanyika katika timu tatu, moja Muhimbili, ya pili Kibamba na tatu
mtaani kutafuta taarifa muhimu za mauaji.
Imeandikwa na Margreth Itala.
on Monday, October 14, 2013
Post a Comment