Baba wa Taifa la Tanzania Mwalimu Julius Nyerere (kulia) akiwa na Baba wa Taifa la Kenya Jomo Kenyatta.
********
WAKATI taifa likiadhimisha miaka 14 baada ya kifo cha Baba wa
Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, mmoja wa wateule wake amefichua
siri kwamba kabla ya uhuru, Rais wa kwanza wa Kenya, Jomo Kenyatta
alilala baharini kumwombea aitawale Tanganyika.
Akizungumza na Tanzania Daima nyumbani kwake Sinza jijini Dar es
Salaam mwishoni mwa wiki, Mzee Iddi Nhende alitoboa siri hiyo akisema
kuwa ndiyo maana utawala wa Nyerere uliogopwa na watu wengi duniani.
Kwa mujibu wa mzee huyo wa miaka 81, siku tatu kabla ya kupandishwa
kwa bendera ya uhuru wa Tanganyika, Kenyatta ambaye alikuwa Mwenyekiti
wa Chama cha African National Union (KANU), alikuwa akilala baharini
mbele ya jengo la Ikulu.
“Ilikuwa ikifika saa mbili usiku watu wote tuliokuwa naye tunabeba
mikeka na soda tunakwenda kulala ufukweni mbele ya jengo la Ikulu.
Tulikuwa tunatandika mikeka yetu, anayetaka anakunywa soda na Kenyatta
analala katikati… kushoto na kulia wanalala wale wajukuu zake wa kike.
“Hapo anauchapa usingizi hadi saa sita usiku, akawa ananiambia muda
huo ukifika nimpige mateke kwenye unyayo ili kumuamsha… sio jambo rahisi
kwa mlinzi kumpiga teke bosi wake, lakini Kenyatta alikuwa jeuri bwana
(anasema kwa msisitizo na mshangao).
“Basi nikawa nafanya hivyo, akiamka tu anatuambia tukunje suruali zetu
tuingie baharini kumwombea Nyerere ili atawale vizuri Tanganyika,
tukawa tunaingia kwenye maji hadi usawa wa magoti, anachukua usinga wake
na kuanza kutumwagia maji vichwani,” alisema mzee Nhende.
Kuhusu utawala wa Nyerere, alisema watumishi wa serikali walifunzwa
ujamaa, kupendana kwa dhati na kuheshimiana huku akisisitiza kwamba
haikuwa rahisi kufanya hujuma kama ilivyo sasa.
Alisema hivi sasa wananchi wamechoshwa na rushwa iliyomea mizizi
kwenye wizara, idara, taasisi na mashirika ya umma, na kubainisha kwamba
wachache wanaopata nafasi wanazitumia vibaya bila kujali maslahi ya
Watanzania wengine.
Mzee huyo anaiomba serikali kuwarejeshea heshima ya taifa watu wake na
kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa kupunguza pengo kati ya masikini na tajiri
alilodai ndiyo chanzo cha maovu yanayoendelea sasa. (Kwa maelezo zaidi
soma makala ya mzee huyo ukurasa wa 14)
Lembeli alipuka
Mbunge wa Kahama, James Lembeli (CCM), amesema kuwa Watanzania
wanavuna walichopanda baada ya kumdhalilisha na hatimaye kuzika mema
yote aliyowaachia Nyerere.
Lembeli alitoa kauli hiyo wakati akitoa maoni yake juu ya kumbukumbu
ya miaka 14 baada ya kifo cha muasisi huyo, akisema kuwa Azimio la
Arusha, miiko ya uongozi, misingi ya umoja vimezikwa na kuruhusu rushwa
kutamalaki, ikiwa ni pamoja na kuifanya fedha kuwa kigezo katika kusaka
uongozi.
“Nchi yetu sasa inakabiliwa na fujo, wizi, ujangili, Watanzania
kubaguana kwa misingi ya dini, kabila na hata rangi, rasilimali za taifa
kutoroshwa na kukithiri kwa ufukara. Tumeruhusu makundi yasiyo halali
ya kibepari kujipenyeza ndani ya jamii, hivyo kuvuruga kabisa ustaarabu
aliotuachia Nyerere,” alisema.
Kwa mujibu wa Lembeli, wananchi wote pamoja na viongozi wanatakiwa
kutubu mbele za Mungu kutokana na kuyazika mema aliyowaachia Nyerere.
TANZANIA DAIMA
Post a Comment