Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

HOFU YATANDA KATIBA MPYA


Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba
HOFU imetanda miongoni mwa jamii, kuhusu kupatikana kwa Katiba Mpya itakayoridhiwa na Watanzania wote. Hali hiyo ilijitokeza mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, katika mkutano wa majadiliano ulioandaliwa na Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA) kwa vyama vyote vya siasa vyenye usajili.

Katika mkutano huo, hoja na kauli mbalimbali zilijitokeza zikionyesha shaka kubwa juu ya hatima ya kupatikana kwa Katiba bora itakayozingatia maslahi mapana ya nchi.

Hofu hiyo inajengwa katika mambo makuu matatu, kwanza ni kuhusu idadi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, idadi ya kura zitakazoruhusu kupitishwa kwa Katiba Mpya kabla ya kupelekwa kwa wananchi kupigiwa kura ya ndiyo au hapana, pamoja na ukomo wa Tume ya Marekebisho ya Katiba.

Hoja zilizotawala mjadala huo ni upungufu katika muundo wa Bunge la Katiba, ambao unatarajiwa kuundwa na wabunge 357 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wabunge 81 kutoka Baraza la Wawakilishi Zanzibar na wajumbe 166 watakaotokana na makundi mbalimbali ya kijamii ambao watateuliwa na Rais.

Michango mingi ya wajumbe wa mkutano huo wa juzi ilionyesha kuwa, Bunge Maalumu la Katiba, linaonekana kutawaliwa na CCM kwa asilimia 72. Kwa maana hiyo, baadhi ya wajumbe walisema mawazo ya Watanzania yanaweza kutupwa kwa kuwa CCM watatawala mchakato huo, kwani wataongoza kwa asilimia 72.



Kuhusu upigaji kura, wadau hao wa siasa walipinga kura hizo kuamuliwa na mtindo wa ‘simple majority’.

Wadau hao wa Katiba walisema siyo lazima kila mbunge awe mtunga Katiba, kwani kila chama kinaweza kupewa idadi ya wabunge watakaotakiwa kuingia katika Bunge la Katiba ili kuepuka mchakato huo kuhodhiwa na chama kimoja cha siasa.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Youth Country Wide, Israel Ilunde, alisema Bunge limevunja Katiba, Ibara ya 29 (3, 4), ambavyo vinakataza raia yeyote wa Jamhuri ya Muungano hatakuwa na haki, hadhi au cheo maalumu kwa misingi ya nasaba, jadi au urithi wake.

“Hapa naona wabunge wamejipigia pande, wananchi wakatae kuwa na Bunge dhaifu kiasi hiki, ni wakati sasa wa kuonyesha hadharani kwamba hatutaki waendelee kuwakilisha matakwa yao bungeni,” alisema Ilunde.

Mwenyekiti wa APPT-Maendeleo, Peter Mziray, alisema Bunge limevunja Ibara ya 98, na hali inayoendelea sasa ni matokeo ya makosa hayo.

Naye, Mwenyekiti wa chama cha NLD, Dk. Emanuel Makaidi, alisema tangu awali, Serikali haikuwa na nia njema ya kuandaa Katiba. Kutokana na hali hiyo, alisema haoni faida kwa vyama vya siasa kwenda Ikulu kwa sababu mchakato huo utalazimika kurudishwa bungeni ambako utaharibiwa na watu walewale.

Naye, Mwenyekiti wa NDC, Said Miraj, alisema mchakato wa Katiba upo njia panda na wale wanaoukwamisha wanajitambua na ipo siku watalazimika kukijibu kizazi cha Tanzania.

Msemaji wa Chadema, John Mnyika, alisema vikao kati ya Rais na wapinzani siyo vipya, hivyo kinachotakiwa ni kwa vipi mazungumzo hayo yatakuwa msingi wa hoja zinazobeba maslahi ya Watanzania katika mchakato wa Katiba Mpya.

Alisema ni kazi ya wadau wote wa Katiba kuhakikisha Bunge la Katiba linakuwa na idadi sawa ya uwakilishi, bila kuacha jukumu hilo kuhodhiwa na Bunge la sasa.

“Kama tulivyopendekeza katika kikao na Rais mwaka 2011 yangefanyiwa kazi, huu mkwamo mnaouona sasa usingekuwapo. Kama kupunguza Bunge la sasa haitawezekana, basi tujadili wajumbe kutoka makundi mengine waongezeke hadi kufikia 300 ili kuweka balance (usawa).

Naye, mjumbe wa JUKATA, Hebron Mwakagenda, alionya kama mchakato wa Katiba Mpya ‘utachakachuliwa’ watachukua jukumu la kuhamasisha wananchi waukatae kwa kupiga kura ya hapana, ili iwe fundisho kwa Serikali.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa JUKATA, Deus Kibamba, alisema suala la Katiba ni la kitaifa bila kujali nani au chama gani kipo au kinakaribia kwenda Ikulu.

Alisema, Bunge limeshindwa kuwa eneo la kuongoza mchakato wa Katiba, hivyo imani pekee ya Watanzania imebaki mikononi mwa rais.

“Kimsingi tuko njia panda, ibara ya 98 ilikiukwa, ilitakiwa kabla ya kufanya jambo lolote kuhusu Katiba, tungerekebisha vifungu vya 1, 2, kwani hii dhambi ndiyo inaendelea kuutafuna mchakato na kuuweka njia panda,” alisema Kibamba.

Nape azungumza

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alipoulizwa kuhusiana na chama chake kudaiwa kudhibiti Bunge la Katiba kwa asilimia 72, alisema hali hiyo inatokana na matakwa ya Watanzania walioamua kukipigia kura chama hicho mwaka 2010.

Alisema CCM kina wabunge wengi tofauti na wapinzani, hivyo wingi huo ulitokana na ridhaa ya wananchi ambao walitaka kiendelee kutawala.

MTANZANIA
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top