SERIKALI imesema, mwakani inatarajia kuajiri walimu wapya 27,000 wa
shule za msingi na sekondari nchi nzima. Taarifa hiyo ilitolewa jijini
hapa jana na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI),
Kassim Majaliwa (pichani) alipokuwa akifunga mkutano wa wadau wa Mfuko wa Pensheni
wa LAPF. Alisema kwamba kitendo cha kuajiriwa kwa walimu hao, kitatoa
fursa ya mifuko ya hifadhi ya jamii nchini, kupata wanachama wengi na
hivyo kuendelea kuboresha shughuli na maisha ya waajiriwa wao.
“Mwakani tunatarajia kuajiri walimu wapatao 27,000 nchi nzima na hii
itakuwa ni fursa nzuri kwa mifuko ya jamii kwani watajiunga katika
mifuko ya jamii iliyopo,” alisema Majaliwa.
Awali, Mkurugenzi
Mkuu wa LAPF, Eliud Sanga alisema, kwa miaka minne mfululizo, mfuko huo
umeongoza kwa utunzaji wa hesabu kwa viwango vya NBAA.
Kwa
mujibu wa Sanga, mwaka jana mfuko huo uliandikisha wanachama 17,840 na
kukusanya michango ya Sh bilioni 119.7 wakati mwaka huu, mfuko
unatarajia kukusanya Sh bilioni 163.
Alisema, LAPF inaendelea
kuongeza uwekezaji katika vitega uchumi kwa kuwekeza Sh bilioni 570,
ambapo imefanikiwa kupata faida ya Sh bilioni 48.7.
Naye Waziri
wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka, akichangia katika mkutano huo,
aliitaka mifuko ya pensheni nchini kushindana katika utoaji wa mafao
bora ili wanachama wa mifuko wafaidike na mafao bora.
Katika
hatua nyingine Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi
za Jamii, Irene Isaka, aliwataka wananchi kujiunga na uchangiaji wa
hiari katika mifuko mingi kadiri wawezavyo, ili utakapofika umri wa
kustaafu wapate mafao bora kuliko mishahara waliyokuwa wakilipwa.
MTANZANIA
Loading...
Post a Comment