DSC01445
Afisa Habari toka Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma Kassim Nyaki (KULIA)akieleza kwa waandishi wa habari juu ya Utekelezaji wa Mchakato wa Ajira katika Utumishi wa Umma wakati wa mkutano uliofanyika leo katika ukumbi wa Idara ya Habari(MAELEZO).Kushoto ni Katibu Msaidizi wa Idara ya Ajira toka Ofisi hiyo Bi. Aurelia Matagi.(Picha na Hassan Silayo-MAELEZO).
*******
Utekelezaji  wa mchakato wa Ajira katika Utumishi wa Umma
Jukumu kubwa na la Msingi la Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ni kuendesha mchakato wa ajira Serikalini. Tangu kuanza kwa majukumu yake Machi, 2010 hadi Juni,2013 imetangaza jumla ya nafasi za kazi zipatazo 8,535 ambapo jumla ya maombi 172, 936 yalipokelewa. Kati ya hizo nafasi 5,037 hadi kufikia mwezi Agosti, 2013 zilikuwa tayari zimejazwa na nafasi 2,291 ujazaji wake upo katika hatua mbalimbali.
Ujazaji huo umenyumbulishwa kwa jinsi na ngazi mbalimbali za elimu. Kati ya nafasi 5,037 wanaume walikuwa 2,836 sawa na asilimia 56.3%na wanawake walikuwa 2,201 sawa na asilimia 43.7%. Wahitimu kutoka Vyuo vikuu ni 2,749 vyuo vya kati 1,999 na wahitimu wa kidato cha nne (4) na sita(6) (supporting staff) ni 289.
Aidha kwa mwezi huu wa Septemba,2013 jumla ya waombaji kazi wapatao 949 waliofanya usaili mwezi Agosti wamepangiwa vituo vya kazi na wakati wowote majina yao yatawekwa kwenye tovuti ya Sekretarieti ya Ajira. Baada ya zoezi hili kukamilika tutakuwa tumewashatuma kwa waajiri waombaji kazi 5,986 na kubakia na nafasi 1,342 ambazo ujazaji wake upo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Suala la pili ambalo ningependa kuliongelea ni upangaji wa wahitimu wanaokwenda kufanya kazi katika maeneo ya pembezoni. Kwa muda mrefu sana mikoa iliyopo pembezoni mwa Nchi yetu ilikosa watumishi wa kutosha kutokana na vijana wengi wenye sifa  waliokuwa wakipangwa kutopenda  kufanya kazi katika maeneo hayo. Miaka ya hivi karibuni Serikali imeboresha miundombinu pamoja na kuharakisha kwa upatikanaji wa huduma muhimu  na za msingi  katika maeneo mengi nchini.
Uboreshaji huo wa mazingira ya kazi pamoja na uhaba wa ajira nchini kumeongeza mwamko kwa waombaji wengi wa fursa za ajira kupenda kufanya kazi katika maeneo hayo ikiwemo Mikoa ya Mtwara, Lindi, Kigoma na Rukwa. Kwa mfano tangu kuanza kwa sekretarieti ya Ajira mkoa wa Mtwara tumepeleka watumishi wapya 234, Lindi watumishi 201, Kigoma watumishi 96 na Rukwa na Katavi watumishi 122.
Mwamko wa waombaji wengi sasa hivi kupenda kufanya kazi serikalini unajidhihirisha si tu kwa Sekretarieti ya Ajira kupokea maombi mengi kila inapotangaza nafasi wazi za kazi bali pia kwa idadi kubwa ya wadau wanaotembelea Tovuti ya Sekretarieti ya Ajira. Tangu kuanzishwa kwake Aprili 2012 hadi kufikia jana imetembelewa na wadau zaidi ya 3,760,000.
Jambo la tatu ambalo ningependa kuzungumzia ni kuhusu utumaji wa maombi ya kazi kwa njia ya mtandao (e-application). Kutokana na changamoto nyingi zinazoendelea kujitokeza kwenye soko la ajira ikiwemo wingi wa waombaji ambao unaleta ushindani mkubwa, ubora wa wahitimu na ukubwa wa eneo la Nchi yetu kijiografia, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma inatarajia kufanya mabadiliko kwenye utaratibu mzima wa mchakato wa ajira nchini ikiwemo utumaji wa maombi ya kazi kwa njia ya Kielectroniki (e-application). Mfumo huu mpya utawawezesha  waombaji wa fursa za ajira kuwasilisha maombi ya kazi zitakazokuwa zikitangazwa katika Utumishi wa Umma. Mfumo huo pia unalenga kuboresha mchakato wa ajira ili waajiri waweze kupata waombaji wenye sifa kwa haraka zaidi.
Kabla ya kumaliza nitoe wito kwa waombaji wa fursa za ajira ambao bado wana mtazamo wa kuchagua maeneo ya kufanyia kazi, hususani wale wanaopangiwa vituo vya kazi na Sekretarieti ya ajira na hawaendi kuripoti bila ya kutoa sababu za msingi kuwa kwa sasa hawana sababu ya kufanya hivyo kama tulivyoeleza hapo awali na kwa wale wanaofanya hivyo Sekretarieti ya Ajira inaandaa utaratibu wa kutowaruhusu kufanya usaili mwingine.                   
Mwisho nimalizie kwa kuwashauri waombaji wa fursa za ajira na wale walioko shuleni kujikita zaidi katika  masomo ya sayansi kwa kuwa kada hizo bado zina upungufu wa wataalam ukilinganisha na fani za sanaa na biashara.