Naibu Kamishna wa Madini toka Wizara
ya Nishati na Madini Mhandisi Ally Samaje (KULIA) Akieleza kwa waandishi
wa Habari kuhusu uanzishwaji wa Mradi wa Uchimbaji Madini ya Urani eneo
la mto Mkuju, Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma, wakati wa Mkutano
uliofanyika leo Jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa Idara ya
Habari(MAELEZO).Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Bw.
Assa Mwambene.
Picha na Georgina Misama-Maelezo
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
UANZISHAJI WA MRADI WA UCHIMBAJI MADINI YA URANI ENEO LA MTO MKUJU, WILAYA YA NAMTUMBO
Utangulizi
Kulingana na shughuli za utafutaji
madini zilizofanywa miaka ya nyuma hadi sasa zimebainisha madini ya
urani kuwepo katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Maeneo hayo ni
pamoja na Mto Mkuju (Namtumbo); Madaba (Liwale); Bahi (Dodoma); Gallapo
(Babati); Milima ya Uluguru (Morogoro); na Itigi (Manyoni). Madini hayo
yanaweza kugundulika katika maeneo zaidi kutokana na shughuli za
utafutaji zinazofanywa pamoja na taarifa zaidi za kijiolojia
zinazoendelea kutayarishwa na Wakala wa Jiolojia Tanzania. Hata hivyo,
hadi sasa eneo la Mto Mkuju ndilo limeonekana kuwa na mashapo ya madini
ya urani yanayoweza kuchimbwa kibiashara. Pamoja na matokeo ya awali
kuonesha kuwa yapo madini ya urani yanayoweza kuchimbwa kibiashara bado
utafutaji zaidi unahitajika ili kupata mashapo zaidi yatakayoweza
kuchimba kwa muda mrefu.
Kulingana na utafiti wa kina wa madini
ya urani uliofanywa katika eneo la mradi huu umegundua mashapo
yanayoweza kuchimbwa kibishara. Hadi sasa kiasi cha tani milioni 175.8
za mashapo (Measured, Indicated na Inferred) ya urani kimegunduliwa.
Kiasi hicho ni sawa na pound milioni 115.8 (kilo milioni 52.5) za urani
kwa grade ya 298.8 U3O8ppm. Kulingana na mashapo haya uhai wa mgodi kwa
sasa ni miaka 12.
Mradi wa Mto Mkuju unamilikiwa na
Kampuni ya Mantra Tanzania Limited, Kampuni tanzu ya URMZ ya Urusi.
Kampuni ya URMZ ni Kampuni ya Serikali ya urusi. Mradi wa Mto Mkuju uko
ndani ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Selous (Selous Game Reserve). Pia
eneo hilo ni Sehemu ya Urithi wa Dunia (World Heritage Site). Mwezi
Julai, 2012, World Heritage Committee iliyoko chini ya UNESCO ilitoa
idhini ya kuondoa eneo la Mradi wa Mto Mkuju kwenye Eneo la Urithi wa
Dunia ili uchimbaji wa urani uweze kufanyika. Hata hivyo, eneo hilo
litaendelea kuwa ndani ya eneo la Hifadhi ya Wanyamapori la Selous.
Kutokana na hatua hiyo, uchambuzi wa
masuala ya mazingira ulikamilika mwezi Oktoba, 2012 ambapo Hati ya
Mazingira (Environmental Impact Assessment Certificate) ilitolewa na
Baraza la mazingira la Taifa (NEMC). Baada ya hatua hizo kukamilika,
Wizara ya Nishati na Madini ilitoa leseni ya uchimbaji madini ya urani
tarehe 05 Aprili, 2013. Leseni hiyo inaruhusu shughuli za uchimbaji
kufanyika katika mradi huo. Majadiliano kuhusu mkataba wa kuendeleza
uchimbaji madini kuhusu mradi huo yanaendelea.
Uchimbaji wa madini ya urani katika
mradi wa Mto Mkuju utafanyika hadi hatua ya yellow cake. Baada ya hapo
urani hiyo itasafirishwa kwenda nje ya nchi katika maeneo ambayo
urutubishaji wa madini hayo kwa matumizi mbalimbali kama vile kuzalisha
umeme, kutengeneza vifaa vinavyotumika kwenye sekta za Afya, Kilimo,
Ujenzi na Mifugo utafanyika.
Manufaa mbalimbali yanatarajiwa
kutokana na uchimbaji wa urani katika mradi huo ikiwa ni pamoja na
mrabaha (Dola za marekani zaidi ya milioni 190); Kodi (Dola za Marekani
zaidi ya milioni 363); PAYE (Dola za marekani zaidi ya milioni 50).
Mapato mengine ni pamoja na Kodi ya zuio (Withholding taxes), gawio
(dividend), Import duties, Service levy kwenye Halmashauri ya Namtumbo,
n.k. Hata hivyo, mapato haya yatatokana na hali ya bei ya urani katika
soko la dunia. Manufaa mengine ni ajira kwa watanzania zaidi ya 690.
Udhibiti wa shughuli za urani
Tungependa kuwahakikishia Watanzania
na wananchi wanaoishi karibu na maeneo yaliyogundulika kuwepo na madini
ya urani kwa kiwango cha kuchimbwa kibiashara, kwamba Serikali imechukua
hatua kadhaa za kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya shughuli za
utafutaji, uchimbaji na usafirishaji nje ya nchi madini ya urani. Hatua
hizo ni pamoja na zifuatazo:-
Kuwepo kwa Sheria za Madini, 2010
ambapo madini ya urani na madini mengine yanayotumika kuzalisha nishati,
mfano makaa ya mawe yanatambuliwa kama kundi pekee la energy minerals.
Tofauti na madini mengine, sheria imezuia utoaji wa leseni ya biashara
ya madini (Dealer Licences) kwa madini ya urani kutokana na unyeti wa
madini hayo.Kuwepo kwa Kanuni maalum za the Mining (Radioactive
Minerals) Regulations, 2010 zimetungwa (GN. 407 dated 22/10/2010)
kuhakikisha kuwa kampuni zinazowekeza katika utafutaji na uchimbaji wa
madini ya urani zinafuata maelekezo maalum yanayohusu utafutaji,
uchimbaji, uchenjuaji, usafirishaji na uuzaji wa madini hayo. Vilevile,
Kanuni hizo zinaelezea majukumu ya mamlaka mbalimbali ikiwa ni pamoja na
taasisi za TAEC na NEMC, na Wizara zinazosimamia rasilimali za Maji na
Madini. Madhumuni makuu ni kuhakikisha kuwa shughuli hizo haziathiri
usalama, afya na mazingira yetu na uhusiano wetu na jumuia za kimataifa,
ikiwa ni pamoja na IAEA.
Kuwepo kwa Sheria na kanuni chini ya
Tanzania Atomic Energy Commission (TAEC) ambazo zinahakikisha kuwa
kunakuwepo na uthibiti wa viwango vya mionzi ambavyo vinaweza kuathiri
binadamu. Aidha, watahakikisha kuwa ufungaji katika mapipa na
usafirishaji wa urani unafanyika kwa kuzingatia viwango vya kimataifa
vinavyokubalika.
Kanuni za Usalama, Afya na Mazingira
Migodini zilizotungwa kwa GN Na. 408 ya tarehe 22/10/2010 zimehifadhi
kanuni namba 187 – 190 zilizokuwa kwenye kanuni za mwaka 1999
zinazokusudia kusimamia usalama wa shughuli za utafutaji wa madini ya
urani na mengineyo yenye mionzi ayonisha. Kanuni hizo zimeweka mfumo wa
kushirikisha jamii inayozunguka maeneo yanayofanyiwa utafiti wa madini
hayo.
Taarifa Potofu kuhusu urani
Wapo watu mbalimbali hasa Wanaharakati
kama vile Mtaalam wa Uranium Network Organization ya Ujerumani Bw.
Gunter Wippel ambao wamekuwa wakieneza taarifa potofu kuwa uchimbaji wa
madini ya urani nchini Tanzania utasababisha madhara mbalimbali ikiwa ni
pamoja na:-
a) Kansa ya ini;
b) Kuzaliwa watoto wenye viungo pungufu au zaidi; na
c) Kubadilika kwa DNA.
Madai hayo sio ya kweli ukizingatia
kuwa Tanzania baada ya kuyachimba madini hayo na kuyasafisha kwa kiwango
cha yellow cake haitaendelea na hatua zinazofuata za kurutubisha madini
hayo na kuyafikisha katika kiwango na mfumo wa kuwezesha kuzalisha
umeme ama kutengeneza vifaa vinavyotumika kwenye sekta za Afya, Kilimo,
Ujenzi na Mifugo. Hatua hizi za urutubishaji na matumizi yake katika
kutengeneza vifaa hivyo zitafanyika katika nchi zilizoendelea kama vile
Japan, Ufaransa, Urusi, n.k. Katika hatua hizo ndipo huzalishwa mabaki
(highly enriched uranium wastes) ambayo yasipodhibitiwa kwa kiwango cha
kuridhisha huweza kusababisha madhara yanayoongelewa.
Uchimbaji na usafirishaji wa madini ya
urani katika hali ya yellow cake hayana madhara kwa kiwango hicho
kinachoelezwa na Wanaharakati. Madhara yanayoweza kujitokeza katika
shughuli hizo za uchimbaji na usafirishaji ni madhara ya kawaida kwa
kila eneo ambapo shughuli za uchimbaji madini yawe ya dhahabu, urani,
chokaa ama makaa ya mawe huweza kujitokeza. Ni madhara ya kiusalama kama
vile ajali ama mazingira kuchafuliwa na kemikali ikiwa wawekezaji na
Serikali watazembea katika usimamizi wa shughuli hizo.
Madhara pekee maalum kwa shughuli za
uchimbaji urani ni wizi unaoweza kutokea wa mapipa ya urani wakati wa
usafirishaji na hivyo uzagaaji wa madini hayo nje ya mkondo wa Serikali
na udhibiti wa Kimataifa kupitia Shirika la IAEA. Ndio maana katika
usafirishaji wa madini hayo, Taasisi ya TAEC, Jeshi la Ulinzi, Usalama
wa Taifa, Idara ya Polisi na Idara ya Madini watahusika kwa pamoja
kuhakikisha madhara kama hayo hayatokei na yakitokea hatua za haraka
kudhibiti madhara hayo zinachukuliwa.
IMETOLEWA NA:
WIZARA YA NISHATI NA MADINI
Post a Comment