Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta
ametangaza kuwa majeshi ya Kenya yataendelea kukaa Somalia hadi usalama
utakapoimarishwa katika nchi hiyo iliyokumbwa na vita vya miaka mingi.
Rais Kenyatta amesema kuwa nchi yake haitashurutishwa na magaidi walioteka jengo la maduka la Westgate kwa siku 4.
Rais Kenyatta alihutubia umati
uliokusanyika kwa maombi ya pamoja ya dini mbali mbali, kwa ajili ya
watu 67 waliouawa katika shambulio la Westgate.
Shambulio hilo ndio baya zaidi kuwahi kutokea nchini Kneya tangu majeshi yake yaingie nchini Somalia mwaka wa 2011.
''Hawa wauaji waliokuja kutenda
ukatili wao ulio na woga hapa nchini kwetu, walikuwa wanadai kuwa
wanafanya hivyo kwasababu majeshi ya Kenya yapo nchini Somalia. Nataka
niwaeleze bayana kuwa, majeshi yetu yatakaa huko hadi kuwepo amani
katika nchi hiyo.''
Mmoja wa makasisi walioongoza maombi
hayo, alisema,'' Baba tunakuomba utawale nchi hii. Na uwaoneshe maadui
wote wa taifa hili kuwa wewe unaipenda nchi hii na jina lako
litatukuzwa.''
Wapiganaji hao wa Al Shabaab wamesema
kuwa walifanya shambulio hilo kulipiza kisasi kwa namna majeshi ya Kenya
yaliingia na kuwapiga nchini Simalia.
Rais Kenyatta pia ametangaza kuwa
serikali itaunda tume maalum kuchunguza upungufu mkubwa uliojitokeza kwa
vyombo vya usalama kufuatia shambulio la Westgate.
''Tutaunda pia tume maalum kuangalia
ni wapi tulikosea, ili tujirekebishe kuendelea mbele. Tuone ni wapi
kumetokea upungufu na ni vipi tutarekebisha.''
Ushirikiano
Aliyekuwa waziri mkuu nchini Kenya
Raila Odinga, alikuwa miongoni mwa waliohudhuria maombi hayo. Bwana
Odinga ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kuisaidia Kenya kukabili
ugaidi.
Aliongeza kuwa ni makosa kwa mataifa
ya magharibi kutoa tahadhari kwa raia wao kutotembelea Kenya huku kwa
upande mwingine zikishinikiza Kenya kufayia mabadiliko idara zake za
usalama.
Bwana Odinga amesisitiza kuchukuliwa hatua za kuimarisha usalama nchini Kenya.
''Shambulio hili ni ishara kuwa
tunaingia katika makabiliano makali zaidi. Ni lazima tubadilishe mbinu
zetu za kukusanya intelijensia na uharaka wa kuchukua hatua. Ni lazima
pia tuweke adhabu kali kwa maafisa wanaolinda mipaka yetu ambao
wanakubali mlungula na kuruhusu maadui kuingia nchini na kutuumiza.''
Mwandishi wa BBC anasema kuwa wakenya
walivyojitokeza kwa wingi, walitaka kuonesha ishara ya utangamano wa
dini mbali mbali licha ya tofauti za imani.
Wiki moja baada ya shambulio la Westgate kumalizika, watu 39 wameripotiwa kutoweka
BBC
Post a Comment