SIKU
chache baada ya Waziri wa zamani na Mbunge wa Urambo Magharibi, Profesa
Juma Kapuya (CCM) kutuhumiwa kumbaka na kutishia kumuua binti mdogo wa
miaka 16, kiongozi huyo ameibuka na kutoa utetezi wa kujikanganya.
Akizungumza
kupitia kwa wakili wake, Yasin Memba, mbunge huyo alitishia kuliburuza
gazeti hili mahakamani endapo halitamwomba msamaha ndani ya siku saba.
Pamoja na
kukataa kwake kumfahamu binti huyo, Kapuya amekiri kumiliki simu namba
0784993930 ambayo imekuwa ikitumiwa kuwasiliana naye ikiwemo kumtumia
ujumbe mfupi wa maneno (sms) wa vitisho.
Hata
hivyo, katika namna ya kushangaza, Kapuya alidai kwamba simu hiyo
aliishaigawa miezi sita iliyopita, na hivyo hausiki kwa namna moja ama
nyingine na tuhuma alizopewa.
Lakini
wakati Kapuya akikwepa mtego huo, Novemba 9, mwaka huu, gazeti hili
liliwasiliana naye kupitia namba hiyo hiyo anayodai kwamba alishaigawa
miezi sita iliyopita.
Tarehe
hiyo, gazeti hili liliwasiliana na mbunge huyo ili kuthibitisha tuhuma
zilizokuwa zikimkabili wilayani Kaliua za kumpiga makofi kiongozi mmoja
wa CCM.
Kapuya kupitia namba hiyo, alitoa utetezi wake ambapo gazeti hili lina sauti yake.
Utetezi
wake pia unaongeza utata kwani hakufafanua ilikuwaje akagawa namba ya
simu iliyosajiliwa kwa jina lake kwa mtu mwingine, huku ikiendelea
kutuma fedha na vitisho kwa binti huyo.
Katika utetezi wake jana, Kapuya alikana kutomjua binti huyo wala dada yake, na kwamba yeye si mwathirika wa ugonjwa wa ukimwi.
Alilishutumu
gazeti hili kuwa lilijifanya hakimu kwa kuchapisha tuhuma zake bila
kumpa nafasi ya kujitetea kama ilivyo kawaida kwenye tasnia ya habari.
Hata
hiyo, ukweli ni kwamba nafasi hiyo aliipata, lakini hakuitumia kwani
alipopigiwa, simu yake ilipokelewa na mtu aliyejitambulisha kuwa ni
dereva wake na kutaka aelezwe sababu za kutafutwa bosi wake.
Hata
alipoelezwa kuwa anayehitajika ni bosi wake, alisita kisha alitoa namba
nyingine ya simu akitaka atafutwe kupitia namba hiyo.
Lakini muda wote namba hiyo haikupokelewa na hata alipopigwa tena namba ya awali, nayo iliita bila kupokelewa.
Wakili
Memba alidai kuwa mteja wake, alimweleza kuwa habari ile imemletea
madhara na usumbufu mkubwa katika familia yake, jamii na kumvunjia
heshima yake.
"Kwa
sababu hiyo, amenielekeza niwapatie siku saba gazeti la Tanzania Daima,
mitandao ya kijamii ukiwemo wa Jamii Forum, Justina John na Vituko
Mtaani ambao walichapisha habari hiyo, waombe radhi kwa uzito ule ule la
sivyo atavishitaki mahakamani.
"Kama
hawataomba radhi, basi atafungua kesi mbili, moja ni kwa ajili ya gazeti
la Tanzania Daima na hiyo mitandao ya kijamii, na kesi ya pili ni ya
kuhusu huyo mtoto anayedaiwa kubakwa na kuambukizwa ukimwi," alisema.
Aliongeza
kuwa wanataka mtoto huyo aje mahakamani athibitishe aliambukizwaje
ukimwi na alete ushahidi unaoonyesha Kapuya ana ukimwi.
Memba aliuomba umma kuelewa kuwa habari hiyo iliyochapishwa na Tanzania Daima haiusiani na chama chake wala serikali.
Kwa siku
mbili mfululizo gazeti hili lilifichua tuhuma za Kapuya kudaiwa kumbaka
mtoto huyo, na hata baada ya kubaini siri hiyo imevuja, alimpigia simu
mtoto huyo, na baadaye kutuma meseji kadhaa za vitisho.
Tanzania Daima ilishuhudia baadhi ya meseji za simu zilizotumwa na Prof. Kapuya kwenda kwa mtoto huyo.
Juzi alfajiri saa 11:21 kupitia simu yake alituma ujumbe kwa mtoto huyo: "Chagueni kunisubiri tuje tuongee au mnataka kufa?"
Baadaye
saa 1:07 asubuhi, alituma ujumbe mwingine kutoka simu hiyo hiyo kwenda
kwa mtoto huyo, ukisema: "Mkiuawa, itakuwa nzuri, itawapunguzia gharama
za kuishi. Usitake kugombana na serikali, mtoto mdogo kama wewe. Sisi
ndo wenye nchi yetu."
Baadhi ya
mashirika yanayotetea makundi kadhaa yakiwamo Kituo cha Sheria na Haki
za Binadamu (LHRC) na Mtandao wa Kijinsia Tanzania (TGNP) yalijitokeza
kuwasaidia watoto hao, ambao ni yatima.
Mtoto
huyo na dada yake, wakizungumza na gazeti hili kwa hofu mafichoni,
walisema kwa sasa hawana imani tena kama kuna serikali nchini Tanzania
kwa kuwa wamedhalilishwa, wametembezwa hadi bungeni na wabunge bila
hatua kuchukuliwa, licha ya kutoa taarifa katika Kituo Cha polisi
Oysterbay tangu mwaka jana.
Hata
hivyo, kabla ya tukio la watoto hao kuripotiwa ofisi za gazeti hili,
juzi usiku kulikuwa na watu waliokuja wakiwatafuta watoto hao, huku
wakiwatisha kwa simu na kuwatolea maneno ya kejeli, wakidai watawamwagia
tindikali.
Juzi
gazeti hili lilichapisha habari kuhusu mwanafunzi huyo aliyesema kuwa
waziri huyo alimbaka kwenye hoteli moja ya kitalii iliyoko jijini Dar es
Salaam mwaka 2011, na kurudia tena kitendo hicho katika Jengo la
Biashara Complex lililoko Mwananyamala Juni 3, 2012 alipoitwa kwenda
kuchukua ada kwa mara ya pili.CHANZO TANZANIA DAIMA
Post a Comment