Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

Mapigano Mvomero:Wanafunzi washindwa kufanya mtihani

 

Mapigano ya wakulima na wafugaji Kata ya Hembeti, Wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro yameathiri sekta ya elimu kufuatia baadhi ya wanafunzi kuacha shule na wengine kutofanya mtihani wa kidato cha nne.

Mapigano hayo yalianza Novemba 5 hadi Novemba 6 na kusababisha vifo vya watu watano.

Mratibu wa Elimu kata ya Hembeti, Charles Kikuli, alisema shule moja ya sekondari na saba za msingi ziliathirika kutokana na mapigano hayo.

Shule ya sekondari iliyokumbwa na janga hilo ni Hembeti ambayo hadi sasa imeripotiwa wanafunzi wawili kutofanya mtihani wa taifa wa kidato cha nne wakihofia maisha yao.

Aliwataja wanafunzi hao ambao wanatoka jamii ya wafugaji kuwa ni Elia Rijua na Ibrahim Kijeje.



Alisema wanafunzi hao walishindwa kufanya mitihani hiyo kwa kuhofia kulipizwa kisasi na wakulima ambao ndiyo wanaongoza kwa wingi.

Alisema kwa upande wa shule za msingi, idadi ya wanafunzi imepungua kufuatia wazazi wao kuwachukua na kukimbia nao vijiji vya jirani.

Alitaja shule hizo kuwa ni Hembeti, msufini, Mkindo, Mikindo B, Dihombo, Mpapa na Kambala.

"Pamoja na hali imeanza kutengemaa baada ya mawaziri kuja na kuongea na pande zote mbili, bado watu wana wasiwasi kitu ambacho kinapelekea kutowaruhusu watoto wao kuhudhuria masomo," alisema.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Hembeti, Shida Lukali, alisema tatizo la mahudhurio hasa kwa watoto wanaotoka jamii ya wafugaji limekuwa sugu kwa muda mrefu, lakini mgogoro huo umeongeza tatizo kwa kiwango cha juu.

Alisema wakati mapigano hayo yanaibuka, wanafunzi wa kidato cha nne walikuwa wameanza siku ya kwanza kufanya mitihani ya taifa.

Lukali alisema wanafunzi hao walifanya mitihani wakiwa katika hali ya mashaka na hofu kubwa.

Hata hivyo, wanafunzi hao wawili walikimbia na hawakurudi kuendelea na mitihani.

"Hatujaelewa sababu ya kutorudi kufanya mitihani, lakini naamini hofu iliwakumba na kuona pengine watalipiziwa kisasi, kitu ambacho kisingewezekana," alisema Mwalimu Lukali.

Lukali alisema wanafunzi hao hawakuweza kufanya hata mtihani mmoja, hivyo jitihada za kulifikisha suala hilo katika vyombo husika linafanyika.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Hembeti, Gabriel Mkongwe, amesema mpaka sasa wanafunzi 193 hawajaripoti shuleni.

Alisema shule hiyo yenye wanafunzi 649,  walioripoti na kuhudhuria masomo ni 456 tu. Mkongwe alisema wanafunzi wengi wamejikuta wakishindwa kuhudhuria masomo,  kutokana na kukimbilia vijiji vya mbali pamoja na wazazi wao.

"Hata wale waliorudi wazazi wao wametoa malalamiko ya kupotea kwa sare na vifaa vyao vya shule, waliomba wapatiwe muda zaidi ili watoto wao waweze kuanza  masomo," alisema Mkongwe.

Aliongeza kuwa mapigano hayo yaliathiri mitihani ya Moko kwa wanafunzi wa darasa la nne ambayo tayari ilikuwa umegawanywa kwenye shule hizo.

Hata hivyo, mitihani hiyo itafanyika kwa siku mbili kuanzia Novemba 14 baada ya kuridhishwa na hali ya utulivu inayoanza kurejea kijijini hapo.
CHANZO: NIPASHE
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top