Katibu wa Idara ya Hamasa na Chipukizi (UVCCM)
Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi
(UVCCM) umepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha mjumbe
wa tume ya mabadiliko ya katiba Dr Sedondo Mvungi ambacho kimetokea
katika hospitali ya Millpark nchini Afrika kusini.
Uongozi wa UVCCM Taifa unatoa pole kwa familia na
ndugu wa marehemu, pia UVCCM inatoa pole kwa uongozi wa NCCR- Mageuzi
na kwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Warioba pamoja
na Vijana nchini kote ambao wamenufaika na Utaalamu na mafunzo. Kama
vijana tulihitaji sana mchango wa mawazo, hekima na utaalamu kutoka
kwake, hakika tumepoteza kiongozi shupavu, muadilifu na mzalendo ambae
ni mfano wa kuigwa kwa Vijana wa Taifa hili.
Kadhalika, UVCCM inatoa pongezi za dhati kwa hotuba
makini iliyojaa hekima, busara na ushupavu wa Uongozi iliyotolewa na
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.
Hakika vijana tumeridhishwa na maamuzi ya Mheshimiwa
Rais ya Kuendelea kuwa Mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)
na tunapongeza maamuzi hayo yanayolenga kudumisha Umoja na Ushirikiano
wa Nchi za kiafrika katika kujiletea maendeleo. Kwa kutambua nafasi
na manufaa yanayopatikana kwa vijana kutokana na fursa za kiuchumi,
kisiasa, kijamii, ajira nk UVCCM Inamuunga mkono Mheshimiwa Rais kwa
uamuzi wake huo.
Pamoja na kuunga mkono uamuzi huo, UVCCM inatoa angalizo
kuwa ni vyema kwa nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
(EAC) kuendelea kuheshimu taratibu na kanuni za jumuiya hiyo ili kuifanya
endelevu, imara na mfano kwa nchi nyingine za Afrika na Duniani kwa
ujumla. Ni lazima wazingatie kuwa Umoja na Mshikamano ndio nguzo ya
maendeleo ya kweli ya Afrika.
Pamoja na kusikitishwa, UVCCM inazo taarifa juu ya
mgogoro unaoendelea katika Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
na kwamba inamtaka Lema kutoelekeza tuhuma kwa UVCCM na viongozi wake
bali waangalie namna bora ya kushughulikia na kutatua migogoro yao ya
ndani ambayo imesababisha kuzushiana, kuchafuana na kuvujishiana siri
katika mitandao hasa ya kijamii.
UVCCM na Viongozi wake inakana kwa namna yeyote ile
kuhusika na usambazaji huo na kwamba Jumuiya hii ni ya Vijana makini
na wanaojitambua na inajielekeza katika kufanikisha malengo ya kuundwa
kwake ya kukisaidia Chama kushika dola mwaka 2015.
Na kwamba UVCCM inalaani tabia ambayo imeasisiwa
na Vijana wa CHADEMA ya kukashifu, kuzomea na hata kutukana Viongozi
wa CCM na Serikali yake na kwamba yaliyomkuta Mhe Lema ni matunda ya
kazi waliyoiasisi wenyewe.
Imetolewa na:
PAUL MAKONDA
KATIBU WA IDARA YA HAMASA NA CHIPUKIZI
UVCCM
13/11/2013
Post a Comment