
KATIBU Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana amesema mtu yeyote, hasa viongozi wanaokerwa na kauli zake au usimamiaji wa chama kwa Serikali, ni bora akaondoka madarakani.
Aidha, amesema CCM ya sasa haitaki upuuzi na utendaji kazi wa mazoea, ndiyo maana imeamua kuelekeza nguvu zake kuondoa kero na matatizo ya wananchi.
Akizungumza jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Nkrumah, Tunduma, wilayani Momba alisema kama kiongozi anakerwa na kauli zake au na chama ajing’atue.
Akishangiliwa na wananchi wa Tunduma, Kinana alisema chama chake hakitaendelea kufumbia macho viongozi wa Serikali na chama ambao wanakiangamiza chama kwa kutotekeleza wajibu wao wa kuondoa kero za wananchi.
“Viongozi hao waliomba kazi mwenyewe, na kila mtu aliyewekwa kwenye ofisi yoyote lazima awajibike kushughulikia matatizo ya wananchi na si vinginevyo,” alisema Kinana.
“Viongozi wa Serikali na chama tumefunga madirisha, tunashindwa kusikiliza wananchi shida zao, badala yake tunawapita bila kusikiliza kujua nini wanakitaka.
“Baadhi ya viongozi wamekuwa wakikasirika wanapoambiwa ukweli kuhusu kutowajibika kwao, na pale wanapoambiwa na watu hao, wanawaita wapinzani kwenye chama,” alisema.
Viongozi hao wamekuwa wakibadilisha maisha yao, badala ya maisha ya wananchi wao, ambao siku zote wamekuwa wakihangaika kuyatafuta.
Alisema vijana hawana haja na vyama viwe CCM, Chadema au TLP, wao wanataka maisha yaende vizuri, wao walijiunga na vyama hivyo vya upinzani kwa sababu ya hasira kutokana na Serikali yao kutosikiliza shida zao.
Kutokana na kutosikilizwa, vijana wengi wamekata tamaa, kwani kila wakijaribu kufanya shughuli zao wanasumbuliwa na urasimu na umangimeza wa viongozi walio madarakani.
Lakini pia vijana wengi wamekuwa wakishindwa kuendesha shughuli zao kwani hata kabla ya kuanza biashara, wamekuwa wakidaiwa kodi, kukata leseni na hata kodi nyingine za kero, kiasi kwamba wanashindwa kuanzisha shughuli hizo.
Alisema viongozi wa Serikali wenye mamlaka ya kodi na leseni na kodi zingine, wanatakiwa kuacha vijana wanaotaka kuanza shughuli zao waanzishe wafanye kwanza shughuli hizo, wakifanikiwa ndipo waanze kuwadai leseni, ushuru na kodi wanazostahili walipe.
Alitaka viongozi hao, kutosumbua akinamama wanaohangaika kutafuta maisha kwa kuuza mboga na bidhaa zingine, kwani wamekuwa wakisumbuliwa kiasi cha kukata tamaa kufanya shughuli hizo za kuwasaidia kuendesha maisha.
Aliwahakikisha kwamba, CCM imeamua kuisimamia Serikali na kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo, na kila kiongozi atakayeshindwa kuwajibika kusemea wananchi shida zao, ni bora kupisha wanaoweza kwani wako wengi. HABARILEO
Post a Comment