Laiti
kama Bunge juzi hapa lingepitisha mapendekezo ya Serikali juu ya
vipengele vya sheria ya magazeti ya 1976, basi, nayo ingelikuwa ni
habari nyingine ya huzuni kubwa kwa Watanzania. Ni habari ya aibu.
Kwamba
miaka 50 baada ya Uhuru, pamoja na kuminyika sana kwa wanahabari, bado
kuna watendaji Serikalini wanaofikiria kuwaminya zaidi wanahabari.
Ndio,
bado kuna wanaofikiria Wanahabari hawa wenye kufanya kazi kwenye
mazingira magumu sana wapewe adhabu kali zaidi wanapofanya makosa wakiwa
kazini.
Na
wakati mwingine inaonekana, kuwa mahusiano ya Serikali na Wanahabari ni
kama ya mzazi na mtoto. Kwamba Serikali ni mzazi, ambaye kila anapoona
mtoto amekosea, anachofikiria ni kutafuta bakora ya kumchapa. Na mtoto
anapoonekana kulifanya tena kosa, basi, mzazi anafikirikia kuongeza
idadi ya bakora. Ni mzazi anayetaka kutuhumu na kuhukumu hapo hapo. Ni
viboko tu. Hataki na haioni haja ya mtu mwingine aingilie kati
kuwasikiliza mzazi na mtoto kwenye kutofautiana kwao.
Na
imeripotiwa kwenye Mwananchi, kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG),
Jaji Frederick Werema juzi ameangukia pua baada ya Bunge kukataa
mapendekezo ya Serikali ya kubadili baadhi ya vipengele vya Sheria ya
Magazeti ya mwaka 1976, ya kuongeza adhabu kwa waandishi wa habari
watakaopatikana na hatia ya makosa ya uchochezi.
Mwananchi
linaendelea kuandika, kuwa Spika wa Bunge, Anne Makinda, aliungana na
wabunge wengine kukataa mapendekezo hayo na kudai kuwa wakati umefika
kwa Serikali kupeleka bungeni muswada wa sheria ya vyombo vya habari,
badala ya kutoa ahadi zisizo na majibu kila wakati.
Kukataliwa
kwa mapendekezo hayo ni pigo kwa Serikali na Jaji Werema ambaye juzi
wakati akijibu hoja za wabunge alijigamba kwamba yeye anasimamia amani
ya nchi kwa hiyo vifungu hivyo haviwezi kuondolewa, kwani anafanya kazi
kwa masilahi ya taifa na hategemei magazeti kwa ajili ya kuwa mbunge. Ni
kauli ambayo iliwachefua wabunge. Linaandika gazeti Mwananchi, Ijumaa,
Novemba 9, 2013.
Ndugu zangu,
Nahofia,
kuwa wakati mwingine wanasiasa wetu wanatunga sheria kwa kuziona
‘hatari zilizo mbele yao’ zinazotishia maslahi yao binafsi, ya vikundi
vyao na ya vyama vyao. Na wala si kwa hatari iliyo mbele yetu kama
taifa. Hivyo basi, kauli za kulinda maslahi ya taifa wakati mwingine
hutumiwa kama koti la kulivaa kuficha dhamira halisi za hao wenye kuiona
‘ hatari iliyo mbele yetu’.
Tutafanya
makosa kama taifa, kama tutafika mahali hata sheria zetu tutakuwa
tukizitunga kutokana na ‘ hofu’ za kisiasa. Hofu za kisiasa ni hisia za
kuja na kupita, lakini, yenye kuhusu maslahi ya taifa ni mambo
tunayotakiwa kuyajengea msingi na yakabaki hata kama sisi hatutakuwepo
duniani.
Majuzi
tu hapa alikuja Spika yule wa Bunge la Uswisi na akashangaa kusikia
kwenye nchi hii bado kuna magazeti yanafungiwa kwa sheria ya mwaka 1976.
Akatwambia kuwa kule kwao anakumbuka mara ya mwisho gazeti kufungiwa
ilikuwa ni baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia.
Ndio,
Wanahabari wa nchi hii si malaika, nao, kama wanataaluma wengine,
wanafanya makosa. Lakini tufike mahali, nasi tufikirie taratibu nyingine
za kusahihishana na kupeana adhabu bila kufikiria kwanza adhabu za
vifungo vya magerezani. Na kazi ya kusahihishana na kupeana adhabu
inaweza kabisa kuachwa kufanywa na wanahabari wenyewe kupitia vyombo
vyao husika vya kurekebishana na kuadhibiana. Ndivyo wanavyofanya
madaktari, mainjinia, walimu na wengineo. Ikishindikana huko ndiko
mahakama zitumike.
Maana,
inasikitisha leo kuliona gazeti la Kitanzania likitoka huku likionyesha
siku ambazo zimebaki kabla ya gazeti dada kufunguliwa. Maana, kwa
maisha ya magazeti ya sasa, hakuna ajuaye amebaki na siku ngapi kabla ya
kufungiwa. Mungu tu ndiye ajuaye!
Na
katika dunia hii tusiishi tukasahau kanuni za maisha. Kuwa kuna kupanda
na kushuka. Kuna leo na kesho. Ya leo unayajua na ya kesho huyajui.
Usiyemhitaji leo utamhitaji kesho. Ni kwa vile wewe ni mwanadamu.
Na
hapa nitamalizia na kisa cha Mbunge Eliakim Simpasa. Julai 3 mwaka huu,
wakati nikitembea kwa miguu Mtaa wa Shaaban Robert jijini Dar,
nilikutana na ndugu zangu wawili kwenye familia ya wanahabari; Boniface
Makene na John Mapinduzi. Wawili hawa nao walikuwa wakitembea kwa miguu
wakiongozana na Mbunge Mstaafu, Mzee Eliakim Simpasa. John na Boniface
kwa sasa wako Ofisi ya Makamu wa Rais.
Basi,
tukaongea kidogo, na ilibaki kidogo tu nimkumbushe Mzee Simpasa juu ya
ugomvi wake na wanahabari, enzi hizo akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge
ya Haki na Maadili.
Maana,
nakumbuka siku moja akiwa bungeni, Simpasa alimwomba Spika amwamuru
mwandishi wa habari, silikumbuki jina lake, aingie Bungeni na ajieleze
mbele ya Bunge juu ya habari potofu aliyoiandika juu ya ‘ Bunge Tukufu’.
Eliakim Simpasa alikuwa kama ‘ Dikteta’ fulani hivi.
Naam, nilisita kumkumbusha Mzee Simpasa, maana, yawezekana mwandishi huyo alikuwa ni John Mapinduzi au Boniface Makene!
Na leo hii ndio hao anaotembea nao mitaani kwa miguu, kama ndugu!
Ni Neno La Leo.


Post a Comment