*****
Nje ya darasa la pili katika Shule ya Msingi Ilala iliyopo
Manispaa ya Iringa, baadhi ya wanafunzi wanamsimanga mwenzao mmoja kwa
kumwita mtoro.
Mmoja anapaza sauti na kusema: “Sharafi hajui
kusoma’’ Ni kweli Sharafi (jina siyo lake) anayesoma darasa la pili
shuleni hapo, anaelezwa na mwalimu wake kuwa hajui kusoma na pia ni
mtoro aliyekubuhu, japo mwenyewe anakana kuwa siku hizi siyo mtoro tena.
Mwalimu wake Esther Sanga, anasema baadhi ya
wanafunzi darasani mwake wana matatizo ya kutokujua kusoma licha ya kuwa
hivi karibuni watamaliza darasa la pili, akiwamo Sharafi anayesema
anaweza kukaa hata mwezi mmoja hajaonekana shuleni.
Tukiwa darasani namwomba mwalimu huyo tumjaribu
Sharafi kujua uwezo wake wa kusoma. Tunamwandikia ubaoni neno ‘baba’,
kwa sekunde zisizozidi 10 analisoma na kulipatia. Kisha tunamwandikia
neno ‘iba’, akachukua sekunde zaidi kulisoma na kulipatia.
Neno lingine lilikuwa ‘bobu’. Hapa Sharafi
anatafakari zaidi huku akilikazia macho neno hilo. Baada ya sekunde
nyingi kupita anafanikiwa kulisoma kwa usahihi japo anaonyesha
kutokujiamini na alichokisoma.
Darasa analosoma lina watoto karibu 40 ambao licha
ya kubakiwa na muda mchache kujiunga na darasa la tatu, bado hawajaweza
kusoma kwa ufasaha hasa herufi mwambatano,
Mwalimu Sanga anasema wanafunzi hao wanasoma,
lakini kwa kile anachokiita usomaji wa kudonoadonoa. Anasema: ‘’ Hawa
wanasoma kwa kudonoadonoa, hawasomi kwa mfululizo na sababu ni kwamba
wako wengi darasani na walikosa walimu wenye ujuzi.’’
Bila shaka wanafunzi hawa ni ushahidi wa kuwapo
wanafunzi wengi wanaovuka darasa la pili wakiwa hawajui kusoma, kuandika
na kuhesabu, maarufu kwa kifupi cha KKK au K3
Ilivyo mfumo wa elimu wa Tanzania, unamtarajia
mtoto akimaliza darasa la pili awe ana uelewa mkubwa wa stadi hizo
-muhimu katika mchakato wa ujifunzaji.
Kisa cha Shule ya Msingi Ilala kinashadadiwa na
matokeo ya utafiti uliofanywa mwaka 2010 na Uwezo Tanzania, na kubaini
mwanafunzi mmoja kati ya watano wanaohitimu elimu ya msingi, hajui
kusoma japo hadithi ya kiwango cha darasa la pili.
Utafiti huo ulioitwa ‘ Je watoto wetu
wanajifunza? Ulihusisha sampuli ya watoto 42,033 kutoka kaya 22,800
katika wilaya mbalimbali nchini. Watoto hao walipimwa uwezo wa kusoma na
kuhesabu.
Sababu za kutojua kusoma
MWANANCHI
Post a Comment