Na Magreth Kinabo – Maelezo
Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospete Muhongo amesema kwamba kuanzia
sasa hakuna mgodi utakaoanzishwa bila ya serikali kuwa na hisa .
Kauli hiyo imetolewa leo na Profesa Muhongo wakati wa utiaji saini
leo makubaliano ya kukabidhi mgodi wadhahabu wa Tulawaka kwa Shirika la
Madini la Taifa (STAMICO) kutoka kwa Kampuni ya Uchimbaji wa Madini ya
Afrikan Barrick Gold (ABG) katika hafla fupi iliyofanyika kwenye
ukumbi wa mikutano wa wizara hiyo jijini Dares Salaam.
Utiaji saini huo ulifanywa na Mkurugenzi Mkuu wa STAMICO,Gray Mwakalukwa na Makamu wa Rais wa ABG, Deo Mwanyika.
“STAMICO itachimba
katika mgodi huo kwa niaba ya Watanzania, hivyo serikali itaiwezesha
kiutendaji, kifedha,kiutalaamu na kuwa na rasimali watu, alisema
Profesa Muhongo.
Aliongeza kuwa baadae shirika hilo litauza hisa kwa Watanzania.
Alisema
STAMICO imenunua mgodi huo kwa dola za Marekani milioni 4.5, ambapo
kati ya fedha dola milioni 3.5 zimeshalipwa moja kwa moja.
Akizungumzia
kuhusu uuzaji wa mgodi huo, Mwanyika alisema kulingana na sera zao
uchimbaji huo hautakuwa na faida kwao , hivyo eneo hilo linafaa
kuendelezwa na wachimbaji wa kati.
Alisema
STAMICO itachukua mdogi huo na baaadhi ya leseni za utafutaji wa madini
zinazozunguka eneo hilo kwa gharama hiyo na kukubali kutoa asilimia 2
ya mrabaha iwapo uzalishaji utazidi wakia 500,000 zikiwa na kikomo cha
dola za Marekani 500,000.
Mwanyika
alifafanua kwamba STAMICO itachukua umiliki na usimamizi wa mfuko wa
fedha za ukarabati wa mazingira ikiwa kama sehemu ya mpango wa ufungaji
wa mgodi huo na itakuwa na dhamana ya majukumu yaliyopita na ya baadae
yanayohusiana na kufunga mgodi na ukarabati wa mazingira.
Aidha
itawajibika kulipa fidia kwa wahusika wengine wa mkataba huo iwapo
majukumu yao yalioainishwa hayakutekelezwa na ABG itailipa
STAMICO salio lililobakia kwenye mfuko wa kukarabati mazingira ambayo
kwa sasa ni dola za Marekani milioni 17.6,ambapo bei pia ya mauzo kwenye
makubaliano itapunguzwa kutoka kwenye salio.
Katika
hatua nyingine Profesa Muhongo alisema watu wenye maeneo makubwa
ya vitalu vya madini ambayo hawajayafanyia kazi yatachukuliwa
kulingana na Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na watapewa wachimbaji
wadogo.
Alisema
STAMICO itakuwa inawasimamia wachimbaji wadogo, itawasaidia kupata
mikopo kiurahisi kutoka Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB), kutoa elimu
ya uchimbaji na kuhifadhi mazingira kupitia vyama vyao.
Post a Comment