Shujaa wa kukabili siasa za ubaguzi wa rangi, Nelson Mandela
amezikwa huku aliyekuwa rafiki yake, Ahmed Kathrada akisema wakati
wakiwa kifungoni, yeye na wafungwa wengine walikuwa wanamheshima kwa
kumuita “Kaka mkubwa.”
“Tumempoteza kaka yetu mkubwa,” alisema Kathrada
kwenye mazishi hayo ambayo yalihudhuriwa na zaidi ya watu 4,500,
wakiwamo wageni wa mataifa mbalimbali.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Uingereza
(BBC), Kathrada alisema waliishi katika kifungo na Mandela kwa miaka
kadhaa kwenye Gereza la Robben Island.
Mtandao wa News24, ulimnukuu Kathrada akisema:
“Nilikutana naye (Mandela) kwa mara ya kwanza miaka 67 iliyopita, akiwa
wa afya, mwanaume mtanashati… mwanamasumbwi na mfungwa ambaye alikuwa na
uwezo mkubwa wa kufanya mambo hasa yale ambayo yalikuwa yametushinda.”
Kathadwa alisema Mandela alikuwa ni mtu makini na
hata alipotoka gerezani na kuendeleza harakati za siasa, uongozi wake
mahiri uliweza kuwang’arisha wengine waliofanya kazi karibu naye.
Miongoni mwa viongozi mahiri ambao ni zao la
Mandela, Kathrada anawataja kuwa ni Thabo Mbeki, Albert Luthuli, Walter
Sisulu na wengine ambao wameendeleza kukiimarisha Chama cha ANC hadi
sasa.
Katika hatua nyingine, usiku wa kuamkia jana,
katika Kijiji cha Qunu, ndugu wa familia walishiriki mkesha ambao mambo
mengi ya kiutamaduni yalifanyika.
Katika kijiji hicho ambacho Mandela jana alizikwa,
mazingira yalikuwa safi na barabara nyingi zilikuwa zimetengenezwa,
jambo ambalo linaashiria kuwa Serikali ilijipanga kikamilifu kukiandaa
kwa mazishi hayo.
MWANANCHI
Post a Comment