**********
Rais Jakaya Kikwete jana aliyateka mazishi ya Rais wa kwanza
mzalendo wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, alipotoa salamu mbele ya
maelfu ya waombolezaji na wageni wa kimataifa walioshiriki katika
mazishi hayo.
Rais Kikwete aliweka bayana jinsi Tanzania
ilivyoshiriki katika vita ya ukombozi si kwa Afrika Kusini pekee bali
kwa nchi nyingi za Kusini mwa Afrika zikiwamo Angola, Msumbiji, Zimbabwe
na Namibia.
Kadhalika alizungumzia jinsi wapigania uhuru wa
ANC walivyoweka kambi zao na kufungua ofisi za chama hicho nchini
Tanzania ambako walipewa makazi na vifaa, maelezo ambayo yalishangiliwa
na umati wa watu uliohudhuria.
“Kwa hakika ANC walipata makazi mapya Tanzania
ambayo waliyatumia kuendesha mambo yao, kujipanga na kuendeleza vita ya
ukombozi. Kutoka Tanzania ANC waliweza kuwafikia makada wake na
wanachama waliobaki Afrika Kusini kwa kutumia mawasiliano ya siri,”
alisema Kikwete na kuongeza:
“Kimsingi Serikali ya Tanzania ililazimika
kuanzisha redio maalumu kwa ajili ya vita ya ukombozi ambayo ANC
waliitumia kupaza sauti ambazo walikuwa wamenyimwa na utawala wa ubaguzi
wa rangi.”
Rais Kikwete aliyekuwa na kazi ya kumwelezea
Mandela kama mpigania uhuru, alieleza jinsi Mandela alivyofika Tanzania
Januari 1962 bila kuwa na hati ya kusafiria na kwamba katika mazungumzo
yake na Hayati Mwalimu Nyerere alieleza mpango wa kudai uhuru kwa njia
ya mapambano.
“Mwalimu Nyerere alikuwa na maoni tofauti kuhusu
mpango wa kuendesha mapambano kwa kutumia silaha, lakini baadaye
walikubaliana na Tanzania ilikubali kuanzishwa kwa kundi hilo na mwalimu
(Nyerere) aliwapa sehemu ya kuendeshea shughuli zao na vifaa,” alisema
Kikwete na kuongeza:
“Kwa hiyo, kwa wale walioshiriki katika vita vya
ukombozi na askari wa MK (Jeshi la ANC), majina kama Kongwa, Mgagao,
Mazimbu na Dakawa hayawezi kuwa mageni na pengine mtakumbuka enzi zile
maisha yalivyokuwa.”
Kikwete alisema wakati akiwa Tanzania, Mandela
alikuwa akiishi kwa aliyekuwa Kada wa TANU, Marehemu Nsilo Swai na
kwamba baada ya kusaidiwa kupata nyaraka za kusafiria kwenda Nigeria,
Morocco na Ethiopia, aliacha buti zake nyumbani kwa mzee huyo.
“Familia hii iliendelea kutunza buti hizo
wakitaraji kwamba Mandela atarudi, lakini wakati anatoka katika safari
yake hakupita tena Tanzania na kwa bahati mbaya alipofika Afrika Kusini
alikamatwa na kufungwa,” alisema Kikwete katika hotuba iliyorushwa na
vituo vyote vya televisheni vya kimataifa.
Aliongeza: “1995 ikiwa mwaka mmoja tangu Mzee
Mandela aingie madarakani, viatu vile vililetwa na mjane wa marehemu
Swai, Vicky Nsilo Swai ambaye nimekuja naye leo ili ashirikiane nanyi
katika msiba huu ninyi mlio ndugu zake.”
Alisema vita ya ukombozi haikuwa rahisi kwani
wakati mwingine Tanzania mbali na kuwasaidia wapigania uhuru hati za
kusafiria, ililazimika pia kuwapa majina ya bandia ili waweze kutekeleza
majukumu yao vizuri.
MWANANCHI
Post a Comment