Askofu
Godfrey Mdimi Mhogolo wa Kanisa la Anglikana,Dayosisi ya Central
Tanganyika (DCT) akihubiri mbele ya mamia ya waumini wa kanisa hilo jana
wakati wa Ibada ya Krismas. Picha na Israel Mgussi.
……………………………………………………..
Geita. Askofu
wa Kanisa Katoliki Jimbo la Geita, Damian Dallu amesema viongozi wengi
wamekuwa wakijidanganya kwa kuwa wabinafsi na wenye kujirundikia mali na
kutojali watu maskini kwa kuamini kufanya hivyo watajitengenezea
mazingira ya kufurahisha nafsi zao.
Akihutubia kwenye ibada ya
Krismasi iliyoadhimishwa kitaifa mkoani Geita, askofu huyo aliwataka
Watanzania kuacha ubinafsi na kupendana huku akisisitiza kuwa;“Ukiona
mwenye madaraka anajifirikia mwenyewe na kusahau shida zinazowakabili
watu maskini basi huyo siyo kiongozi wa watu.”
Askofu Dallu alisema siku zote
kiongozi ni mtu wa kuwajali watu na anapaswa kuwajibika kwao, lakini
kama inatokea kiongozi anaweka masilahi yake mbele huyo kiongozi hafai,”
alisema Askofu Dallu.
“Mali haitawaletea furaha kamwe.
Hata ikitokea mahali kuna mali mfano hapa Geita tuna dhahabu, Mtwara
wana gesi na watu wanatumia madaraka yao kuwataka watu wa Mtwara
watenganishwe na Watanzania wenzao kwa ajili ya gesi,” alionya.
Alisema kuwa na ubinafsi wa
kujirundikia mali kamwe hauwezi kumletea furaha binadamu mbali ya kuwa
chanzo cha vurugu na mitafaruku.
Alitolea mfano nchi za Uarabuni
namna zilivyobarikiwa kuwa na mali ya asili kama mafuta lakini hata
hivyo pamoja na neema hizo bado nchi hizo zinakabiliwa changamoto ya
ukosefu wa amani.
Askofu Dallu alisema kuwa
viongozi waliopewa dhamana ya kuongaza watu wanatumia vibaya nafasi zao
ikiwa ni pamoja na kuharibu rasilimali za nchi kwa kushiriki kuhamasisha
watu kuwa na utengano.
Alisema viongozi wengi wanatumia
mamlaka ili wapate kutawala rasilimali za nchi kwa manufaa yao binafsi
bila kuwahurumia Watanzania wenzake.
Pia
alikemea vitendo vya baadhi ya viongozi na jamii nzima kuharibu na
kutumia vibaya rasilimali za nchi kwa kuua tembo na kuangamiza vivutio
vya nchi kwa masilahi binafsi.
CHANZO: MWANANCHI
Post a Comment