“Viongozi
wa kisiasa wamekuwa hatari, wanajitahidi kutafuta uongozi kwa gharama
yoyote ile, hasa kwa kuwarubuni wananchi kwa kuwapa zawadi jambo ambalo
si jema na mtu anayefanya hivyo hafai kuwa kiongozi kwa taifa na mbele
za Mungu,” Askofu Zacharia Kakobe
………………………………………………………………..
Dar
es Salaam. Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship,
Zacharia Kakobe amesema mawaziri mizigo ni matunda ya uteuzi mbovu
unaofanywa na mamlaka husika ambao hauzingatii vipawa vya uongozi.
Pia ameonya ukabila na kuvitaka
vyama vya siasa vinavyodaiwa kuendeshwa kwa misingi hiyo vifutwe haraka
kabla havijachafua hali ya hewa. Akizungumza jana kwenye ibada ya
Sikukuu ya Krismasi iliyofanyika katika kanisa hilo Mwenge, Dar es
Salaam, Askofu Kakobe alisema si rahisi kwa mtu ambaye hana kipaji cha
kuongoza akawa kiongozi, kwani hataweza kumudu nafasi atakayopewa.
“Siku zote uongozi ni kipaji,
sasa matatizo yanayotukumba ya kuwa na viongozi mizigo ni kutokana na
uteuzi mbovu ambao hauangalii suala la vipaji vya watu,” alisema na
kuongeza: “Tumekuwa tukijichagulia tu viongozi tena kwa kuangalia maeneo
wanayotoka jambo ambalo siyo jema na la hatari, mifano hai tunaiona
sasa. Wanachokifanya viongozi mizigo ni kujihudumia wao na kuwatelekeza
wananchi ambao ndiyo wangekuwa wa kwanza kuhudumiwa.”
Hivi karibuni, Katibu Mkuu wa
CCM na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye walitaja
orodha ya mawaziri wanaoelezewa kuwa mizigo. Mawaziri hao ni pamoja na
Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa, Waziri wa Kilimo, Chakula na
Ushirika, Christopher Chiza na Naibu wake Adam Malima.
Orodha hiyo iliongezeka baada ya
Bunge kumtaja Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), Hawa Ghasia
pamoja na Manaibu wake, Aggrey Mwanri na Kassim Majaliwa kupima na
kutafakari kama wanatosha kusimamia wizara hiyo baada ya ripoti ya
Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kufichua ufisasi
kwenye wizara hiyo.
Viongozi wanaotoa zawadi
Akizungumzia suala la viongozi
wa kisiasa kutoa zawadi kwa wananchi alisema ni hatari, kwani ipo siku
watataka kurudisha walichokitoa. Alisema wananchi wamekuwa wakirubuniwa
kwa khanga, vitenge, fulana na chakula cha siku moja ili kuwapa watu hao
nafasi ya uongozi, lakini baada ya hapo kinachofuata ni mateso, kwani
wananyonywa na maisha yanazidi kuwa magumu kwao.
“Viongozi wa kisiasa wamekuwa
hatari, wanajitahidi kutafuta uongozi kwa gharama yoyote ile, hasa kwa
kuwarubuni wananchi kwa kuwapa zawadi jambo ambalo si jema na mtu
anayefanya hivyo hafai kuwa kiongozi kwa taifa na mbele za Mungu,”
alisema Askofu Kakobe.
Alisema wananchi wanatakiwa
kuwakataa viongozi wa aina hiyo, kwani hawana vipaji vya uongozi, bali
wanatumia fedha kutafuta nafasi wanazozitaka na kwamba wakipata
watawatelekeza kwa kurudisha walichokitoa.”
Ukabila.
Akizungumzia ukabila, Askofu
Kakobe alisema miaka ya nyuma taifa lilikuwa halina vitendo vya ukabila,
lakini kwa sasa hali imekuwa mbaya, kwani unaonekana waziwazi.
Alisema
baadhi ya vyama vya siasa nchini vimekuwa vikidaiwa kuendeshwa
kikabila, huku sheria za nchi zikikataza… “Kama kuna chama cha siasa
kinaendeshwa kikabila kifutwe haraka, kwani ni hatari kwa nchi na taifa
kwa jumla.”
Aidha,
Askofu Kakobe alisisitiza kuwa ni aibu kwa kiongozi wa chama cha siasa
kuendekeza ukabila na kwamba hawawezi kukubali kuona mtu ambaye ni
mkabila anakuwa kiongozi wa nchi.
CHANZO: MWANANCHI
Post a Comment