*******
Familia ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere
itawakilishwa katika mazishi ya Rais wa Kwanza Mzalendo wa Afrika
Kusini, Nelson Mandela, ambaye atazikwa kesho katika Kijiji cha Qunu,
Mthatha Jimbo la Eastern Cape.
Habari ambazo gazeti hili lilizipata jana mjini
Pretoria zinasema kuwa Mama Maria Nyerere, ambaye ni mjane wa Baba wa
taifa, alialikwa kuhudhuria mazishi hayo kwa kuzingatia uhusiano uliopo
baina ya familia hizo mbili.
Hata hivyo, imethibitika kuwa Mama Maria hataweza
kuhudhuria mazishi hayo kesho, badala yake amewatuma wawakilishi ambao
ni mabinti zake wawili; Anna Nyerere ambaye ni mtoto wa pili na mtoto
wake wa saba, Rosemary Nyerere.
Madaraka Nyerere ambaye ni mtoto wa sita wa
Mwalimu alithibitisha jana kwamba familia yao imealikwa kushiriki
mazishi hayo, lakini akaweka wazi kwamba: “Mama hataweza kwenda kuzika,
atakwenda baadaye kidogo baada ya mazishi kufanyika.”
Madaraka alisema kwa jinsi afya ya mama yake
ilivyo sasa, hataweza kwenda Qunu. “Kwa kawaida mazishi haya ya kitaifa
huwa yana mambo na pilika nyingi, kwa hiyo mama ameona asubiri,”
alisema.
Kuhusu kifo cha Mandela, Madaraka alisema kwamba
kama wanafamilia, wameguswa na msiba huo na kuwa kimewakumbusha uchungu
walioupata wakati walipofiwa na baba yao Oktoba 14, 1999.
“Kwa kweli tumeguswa sana na msiba na tunawapa
pole sana, tunakumbuka kwamba wakati baba alipofariki, Mama Graca
tulikuwa naye, alikuja kabla ya mazishi na alikuwepo kwenye mazishi na
baada ya mazishi aliendelea kukaa kwa siku kama saba,” alisema Madaraka
na kuongeza:
“Pia tunakumbuka kwamba Mzee Mandela yeye alikuja
baadaye mpaka Butiama kutoa pole. Ilikuwa Novemba 26, 1999 kwa hiyo
tunaguswa na msiba huu.” Awali, gazeti hili lilidokezwa kwamba watoto
hao wa Nyerere walikuwa wamefikia katika Hoteli ya Burgers Park,
Pretoria lakini walipotafutwa katika hoteli hiyo wafanyakazi walisema
kwamba tayari walikuwa wameondoka.
MWANANCHI
Post a Comment